HEADER AD

HEADER AD

RC SIMIYU AAGIZA AFISA AFYA, MAZINGIRA BUSEGA AONDOLEWE


>> Asema uamuzi huo unalenga kuimalisha uwajibikaji

>>Ni baada ya kushindwa kusimamia usafi mji wa Lamadi
 
Na  Samwel Mwanga, Busega
 
MKUU wa mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi amemwagiza Katibu Tawala wa mkoa huo kumhamisha Afisa Afya na Mazingira Msaidizi wa wilaya ya Busega, Anord Batenga kwa kumbadilishia kituo cha kazi kutokana na kushindwa kusimamia usafi katika mji wa kibiashara wa Lamadi ulioko wilayani humo.
 
Uamuzi wa kuhamisha Afisa huyo unalenga kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha kuwa mji huo unakuwa safi na kuvutia, hususan kwa kuwa ni eneo la kibiashara katika wilaya hiyo.

      Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi akizungumza na wananchi wa mji waLamadi katika wilaya ya Busega katika mkutano wa hadhara.
 
Agizo hilo limetolewa Novemba 19,2024 katika mji wa Lamadi ikiwa ni muendelezo wa mikutano ya hadhara inayofanywa na mkuu huyo wa mkoa wa kusikliza na kutatua kero za wananchi katika mkoa huo.
 
Rc Kihongosi amesema kuwa hii ni mara ya pili wananchi wa mji huo wamekuwa wakilalamikia dampo la takataka lililoko katika makazi ya watu na chanzo cha maji ambacho ni mto lakini Wataalam wa Afya na Mazingira wameshindwa  kulipatia ufumbuzi suala hilo.
 
Amesema kuwa wapo watumishi wa serikali wameshindwa kutekeleza majukumu yao licha ya kulipwa mishahara kutokana na kazi walizoajiriwa jambo ambalo linamfanya kuamua kuchukua maamuzi kama hayo ya kinidhamu.

     Sehemu ya wakazi wa mji wa Lamadi wilaya ya busega waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero uliohitishwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi(hayupo pichani).

“Mwambie RAS amwandikie barua huyu bwana amtoe hapa ,mwambie amtafutie sehemu nyingine ya kufanyia kazi wilaya nyingine na tofauti na hapa mjini,umenielewa vizuri na hilo agizo litekelezwe ndani ya siku tatu mtafutie kituo,sasa nitoe maagizo nikute hajatekeleza.
 
“Wewe tukupeleke sehemu ukatusaidie  naona hapa pamekushinda leo ni siku ya pili mazingira ni machafu, mishahara mnalipwa ya nini sasa,baadaye ije ionekane viongozi wanawafokea watumishi wa Umma kwa uzembe wa makusudi,”amesema.
 
Amesema kuwa hatua kama hizi mara nyingi huchukuliwa ili kuimarisha utendaji kazi wa watumishi wa umma na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
 
Awali Juma Joseph ambaye ni mkazi wa Lamadi alitoa kero yake kwa mkuu huyo wa mkoa kwa kualalmikia kutozwa fedha za ushuru na halmashauri ya wilaya ya Busega katika biashara zao lakini wamekuwa wakiachiwa takataka zilizorundikana kwenye dampo ambalo liko kwenye makazi ya watu na pia karibu na chanzo cha maji ambacho ni mto.

       Mkazi wa Lamadi,Juma Joseph akitoa malalamiko yake mbele ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi(hayupo pichani).
 
Naye Afisa Afya na Mazingira,Batenga amesema kuwa kwa sasa wametenga eneo la Mwalukonge katika mji wa Lamadi kwa ajili ya kuweka dampo la takataka na hivyo kuwazuia wananchi kutotupa tena taka kwenye eneo hilo ambalo linalalamikiwa ambalo liko kwenye makazi ya watu na pia ni chafu.

“Tuliandika barua kwenye uongozi wa kijiji cha Lamadi kutupatia eneo jingine kwa ajili ya kuwela Dampo na wakatuonyesha eneo la Mwalukonge   na tuliwaeleza ya kuwa watu wasitupe tena kwenye eneo la dampo la awali ambalo kiukweli liko kwenye makazi ya watu na ni chafua hata kwa sasa,”amesema.
 
       Sehemu ya wakazi wa mji wa Lamadi wilaya ya busega waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero uliohitishwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi(hayupo pichani).

No comments