HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : SHUMBURERE


INAYOSUKWA kofia, kwa kutumia minyaa,

Na ukindu wavalia, pana kama ukivaa,

Usije kufikiria, jina lake lazagaa,

Inaitwa shumburere, hicho Kiswahili hasa.


Hiyo ni pana kufia, njema juani kuvaa,

Jua linapozidia, kichwa kivuli chakaa,

Tena inapitizia, kwenye mabega yajaa,

Inaitwa shumburere, hicho Kiswahili hasa.


Malighafi Tanzania, na mafundi wamejaa,

Ukipenda jivalia, kwingikwingi zazaagaa,

Shilingi ya Tanzania wajipatia wavaa,

Inaitwa shumburere, hicho Kiswahili hasa.


Vema tukijifanyia, na wageni wakavaa,

Dola zaweza ingia, kihengeni zikajaa,

Shida dola ya dunia, tutabaki twashangaa,

Inaitwa shumburere, hicho Kiswahili hasa.


Dada kofia valia, nywele zisije chakaa,

Na kaka nakuambia, hiyo shumburere vaa,

Kweli mtafurahia, mkitokeza mwang’aa,

Inaitwa Shumburere, kofia ya Tanzania.


Jitahidi nakwambia, nyumbani iweze kaa,

Kama ukihitajia, wachukua unavaa,

Uache kulialia, kwa jua ukichakaa,

Inaitwa shumburere, kofia ya Tanzania.


Shairi hili limetungwa na  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments