HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : SAKUBIMBI HUNA HAYA

SAKUBIMBI huna haya, ukome kusema watu,

Jinsi unawayawaya, kuongelea ya watu,

Utakuja vunjwa taya, mwilio upate kutu,

Uzushi uongo wako, tavunja ndoa za watu.

Waamka asubuhi, mbio kwa nyumba za watu,

Na jinsi unavyowahi, kama ni muhimu kitu,

Kwa maneno wajeruhi, mahusiano ya watu,

Uzushi uongo wako, tavunja ndoa za watu.

Kuzisikia salamu, kaka na mke wa mtu,

Unajigea jukumu, kumsaka mume mtu,

Kwamba wale ni haramu, wamfanyizia kitu,

Uzushi uongo wako, tavunja ndoa za watu.

Hali ingelikuwaje, asingekuwepo mtu,

Mume ngefikiriaje, wafanyayo hao watu,

Sakubingi ngekuwaje, wangeumizana watu?

Uzushi uongo wako, tavunja ndoa za watu.

Macho yako juu juu, unatafuta ya watu,

Watengeneza nukuu, hata wasosema watu,

Wewe mzushi mkuu, hunao wowote utu,

Uzushi uongo wako, tavunja ndoa za watu.

Ulivyo mbaya wewe, unafwatilia watu,

Wachunguza kama mwewe, kwenye vifaranga vyetu,

Kisha unarusha mawe, ili kuumiza watu,

Uzushi uongo wako, tavunja ndoa za watu.

Nakuonya sakubimbi, unowatendea watu,

Mbele ya Mungu ni dhambi, una laana za watu,

Kwako yatapiga kambi, mapigo ya Mungu wetu,

Uzushi uongo wako, tavunja ndoa za watu.

Hebu ufikie mwisho, kuwasemasema watu,

Acha kuwatoa jasho, zako nia na kiatu,

Wawe na maadhimisho, na maisha yalokwatu,

Uzushi uongo wako, tavunja ndoa za watu.

Shairi limetungwa na  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments