SHAIRI : UKWASI NA UKATA
MAANA ni tofauti, matumizi tofauti,
Ila kuna tashtiti, matumizi siyo fiti,
Sasa wetu mkakati, uelewa uwe fiti,
Ukwasi ni utajiri, ukata umasikini.
Hayo maneno mawili, sawa mwanzo na tamati,
Maana zake ni mbili, ziko pande tofauti,
Ni matumizi kamili, ya hiyo misamiati,
Ukwasi ni utajiri, ukata umasikini.
Ukwasi upo wa mtu, mali iko katikati,
Hata taifa la watu, laweza kujaa noti,
Huo ni jawabu kwetu, kutimiza mikakati,
Ukwasi ni utajiri, ukata umasikini.
Ukwasi wa Bakhresa, amiliki hadi boti,
Huwezi fanya makosa, ukipanda zake boti,
Nilishapata fursa, na nikapiga saluti,
Ukwasi ni utajiri, ukata umasikini.
Ukikumbwa na ukata, wa kununua gazeti,
Ni shida imekupata, huwezi kula chapatti,
Bila kazi kuipata, bilabila kwenye neti,
Ukwasi ni utajiri, ukata umasikini.
Bora wania ukwasi, uvae tai na suti,
Hakuna wa kukughasi, kama avaaye shati,
Ni kama bwana harusi, unafunguliwa geti,
Ukwasi ni utajiri, ukata umasikini.
Ni ukwasi na ukata, ya kwetu misamiati,
Maelezo umepata, usifanye utafiti,
Maana ilokupita, itamke kwa sauti,
Ukwasi ni utajiri, ukata umasikini.
Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment