ASIMULIA AJALI ILIVYOTOKEA NA KUSABABISHA VIFO VYA WATU SABA KARAGWE
Na Alodia Babara, Bukoba
DEREVA wa gari aina ya Toyota Haice, Benedicto, mkazi wa Igayaza wilaya ya Misenyi ambaye alijeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu na kusababisha vifo vya watu saba na wengine tisa kujeruhiwa amesimulia jinsi ajali ilivyotokea.
Kama ilivyoripotiwa katika chombo hiki cha habari, Desemba, 3, 2024 , ajali hiyo ilitokea Kihanga wilaya ya Karagwe iliyohusisha magari matatu ambayo ni lori aina ya scania, costa pamoja na toyota haice.
Ajali ilihusisha lori aina ya scania yenye namba T621 AJQ na Trela namba T472 EAQ likiwa linatokea Kayanga lilipofika Kihanga katika kizuizi cha barabarani yalikuwepo magari mawili na hivyo kuyagonga kwa nyuma na kusababisha ajali.
Katibu Tawala msaidizi mkoa wa Kagera Bwai Biseko, aliyevaa koti nyeusi akiwa na mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa, Bukoba Dkt. Mselata Nyakiroto wakiwapa pole wagonjwa waliopata ajali iliyotokea wilaya ya Karagwe na kusababisha vifo saba na majeruhi tisa.
Benedicto amesema alianza safari vizuri kutoka Omurushaka- Karagwe alipofika katika kizuizi cha Kihanga maafisa uhamiaji walisimamisha gari kwa ajili ya ukaguzi wa kawaida kwa abiria.
Amesema wakati maafisa hao wakiendelea na ukaguzi ndipo lori la mizigo liliwakuta katika eneo hilo na kugonga haice aliyokuwa anaendesha pamoja na costa iliyokuwa mbele yake.
"Nilisimamisha gari kwa ajili ya maafisa uhamiaji kukagua ndani ya dakika kama tatu hivi niliangalia kwenye setimila ya gari upande wangu wa kulia nikaona lori linakuja kwa mwendo wa kasi, limewasha taa na kupiga honi likitokea nyuma, ndipo mtu alifungua kizuizi ili lipite" amesema Benedicto.
Ameongeza kuwa, msimamizi wa kizuizi alikifungua upande mmoja wa kushoto walipokuwa tumeegesha magari ndipo dreva wa Lori alijaribu kukwepa magari yetu bila mafanikio kwani kichwa cha roli kilipita wakaja kugongwa na trela ya lori hilo ambalo lilikuwa limebeba magunia ya parachichi.
Ameeleza kuwa baada ya kutokea ajali dreva huyo mguu wake ulibanwa na vyuma kiasi kwamba bila msaada wa waokoaji asingeutoa na kuwa mguu wake ulikatika.
Amesema baada ya ajali walikimbizwa hospitali ya wilaya na baadaye walipewa rufaa na kwenda hospital ya mkoa, Bukoba ambapo yeye na wenzake saba wanaendelea na matibabu.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa, Bukoba Dkt. Mselata Nyakiroto amesema wamepokea majeruhi wanane, ,wanaume wanne na wanawake wanne na miongoni mwa wale wanaume mmoja ni mtoto wa miaka sita.
"Majeruhi wote waliolazwa wako wodini wanaendelea na matibabu na miongoni mwa majeruhi hao wanne walivunjika mifupa miguu na mikono mmoja ambaye ni mtoto alipata maumivu ya kichwa na wengine watatu walikuwa na michubuko na maumivu sehemu mbalimbali za mwili na wote hali zao zinaendelea vizuri" amesema Dkt Nyakiroto .
Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Kagera, Bwai Biseko ametoa salama za rambirambi kutoka kwa mkuu wa mkoa huo na kutoa pole kwa wafiwa na wote waliojeruhiwa na kwamba wameishawasiliana na baadhi ya ndugu wa marehemu miili miwili imetambuliwa na miili sita bado haijatambuliwa.
Aidha amesema serikali imeandaa rambirambi itawashika mkono ndugu wa marehemu ili shughuli za msiba zifanyike katika hadhi stahiki anazostahili kupata marehemu.
Post a Comment