HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : HONGERA EDWIN SOKO


Kiongozi una ngozi, yang'ara yameremeta,

Mbele umeweka kazi, mahusiano yapita,

Wazungumza kwa pozi, siyo kwa kusitasita,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeaminiwa.


Mpenda demokrasia, usiyekuwa mtata,

Wajumbe wawajulia, wakitakacho wapata,

Misingi shajifanyia, kote kule unapita,

Hongera Ediwn Soko, jinsi umeaminiwa.


Busara uzojaliwa, mkunaji zimepata,

Izidi kufanikiwa, ikizidi kutakata,

MISA-TAN twaelewa, mbele itazidi peta,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeaminiwa.


Alopita amepisha, kiti umeshakipata,

Moto wako sasa washa, tuweze mema kupata,

Hapo walokufikisha, kuwalipa iwe chata,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeaminiwa.


Sasa Klabu ya Mwanza, mkubwa imekupata,

Kazi ndiyo unaanza, mengi sasa utapata,

Siyo pekee ya Mwanza, siende mwendo wa guta,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeaminiwa.


Vyombo vyetu vya habari, Uhuru vema kupata,

Kazi iwe bila shari, habari tukizipata,

Na maslahi uturi, wengi waweze kupata,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeanimiwa.


Maendeleo ya sasa, changamoto utapata,

Ni kugangamala hasa, MISA-TAN zidi peta,

Usijefanya makossa, taasisi ikatota,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeaminiwa.


Novemba nayo Desemba, Bingo kaka umepata,

Kwanza mke umesomba, kujipikia mefuta,

Kwa wazee unatamba, na wewe unayo chata,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeaminiwa.


Desemba na MISA-TAN, mwenyekiti tumepata,

Ni kweli siyo utani, kura zisizo utata,

Sasa ingia kazini, injini ina mafuta,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeaminiwa.


Na Salome Kitomari, maua ya kwako chota,

Umeongoza vizuri, heshima tunaipata,

Sasa kazi ushauri, wageni waweze pata,

Hongera Edwin Soko, jinsi umeaminiwa.


Mtunzi wa Shairi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)


No comments