HEADER AD

HEADER AD

WATU SABA WAPOTEZA MAISHA KWA AJALI YA GARI KARAGWE


Na Alodia Dominick, Karagwe

WATU saba wamepoteza maisha huku wengine tisa wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu ya haice, kosta pamoja na Lori aina ya scania katika kizuizi cha barabarani kilichopo kijiji cha Kihanga kata ya Kihanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda amehibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema imetokea Desemba 03,2014 saa 5:00 asubuhi na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva.

Amesema ajali hiyo inahusisha lori aina ya scania yenye namba T621 AJQ na Trela namba T472 EAQ likiwa linatokea Kayanga wilaya ya Karagwe kwenda Kyaka lilipofika Kihanga katika kizuizi cha barabarani yalikuwepo magari mawili.


Magari hayo ambayo ni kosta namba T367 ECP pamoja na toyota  haice yenye namba za usajili T973 DGD yakiwa yamesimama yakiendelea kukaguliwa na maafisa uhamiaji mita kama kumi kutoka kwenye kizuizi ndipo Scania iliyagonga kutokea nyuma na kusababisha ajali hiyo.

"Gari hilo limetokea Mbeya likiwa limebeba mchele kuupeleka Mtukula na baada ya kushusha mchele lilipata mzigo mwingine Karagwe wa kurudi nao Mbeya ambao ni maparachichi.

" Huyu dreva ni mgeni katika eneo hilo kwa uzembe na kutokuchukua tahadhari alikuja katika mwendo ambao ni mkali akaigonga toyota haice pamoja na kosta" amesema Chatanda 

Katika ajali hiyo vimetokea vifo saba wanawake wanne, mwanaume mmoja na watoto wawili huku majeruhi wakiwa tisa wanaume wanne na wanawake watano.

"Uzembe wa dreva umesababisha ajali kutokana na mwendo mkali lakini ajali haikusababishwa na kufeli breki kwani huko nyuma alikotoka alipita katika mlima wa Kishoju na kwenye kona hivyo ingekuwa breki ule mteremko asingeumaliza.

"Ni wazi kwamba tahadhari za alama barabarani hakuzichukua kwani barabara hiyo inazo alama za barabara na hata kabla ya kizuizi kuna alama pia" amesema Chatanda 

Mmoja wa mashuhuda Adamu Alon mtengeneza majokofu kutoka Kayanga amesema kuwa, ameitwa na mteja Kyaka wilaya ya Misenyi na kupanda Kosta ambayo imehusika kwenye ajali walivyofika Mgakorongo walikuta hilo lori likiwa limesimama dreva anaongea na askari wa usalama barabarani wakapita.

Amesema wakati gari hilo limefika Kihanga katika kizuizi cha barabarani ndipo Scania hiyo imegonga gari lao likiwa linakaguliwa na maafisa uhamiaji.


" Nilikuwa nimekaa kiti cha mbele na dreva huku afisa uhamiaji akinitaka kuonesha kitambulisho, ndipo nikasikia kishindo kikubwa na gari alilokuwemo likahama na kwenda mbele.

Ameeleza kuwa yeye na afisa uhamiaji wamedondoka chini baadaye alipopata fahamu alikuta scania waliyoipita Mgakorongo ndiyo iliwagonga.

Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Karagwe iliyopo Nyakanongo pamoja na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo.

No comments