AUAWA KWA KUNYONGWA BAADA YA KUGONGANISHA WANAUME
Na Alodia Dominick, Bukoba
MKE ameuawa kwa kunyongwa na mtandio baada ya kugonganisha wanaume watatu mmoja mme wake wawili michepuko katika mtaa wa Kashenye kata ya Kashai manispaa ya Bukoba.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Kagera, Blasius Chatanda akizungumza na waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari Desemba 28,2024 amesema kuwa, jeshi hilo limefanya oparasheni ya siku mbili Desemba 26 na Desemba 27,2024 na kukamata watu 15 wakiwemo watuhumiwa wawili wa mauji ya mama huyo.
Chatanda bila kutaja jina la mume wa marehemu amesema alikuwa afisa usafirishaji (boda boda) katika mtaa wa Kashenye kata ya Kashai manispaa ya Bukoba.
Amemtaja aliyeuawa kuwa ni Editha Anderson (32) ambaye aliuawa Desemba 12,2024 katika mtaa wa Kilimahewa kata ya Kashai manispaa ya Bukoba.
Watuhumiwa hao ni pamoja Answari Mutalemwa (25) na Keneth Muganyizi (25) wote wakazi wa mtaa wa Kashenye kata ya Kashai manispaa ya Bukoba.
"Chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi ambapo mtuhumiwa Answari Mutalemwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Editha na wakiwa katika mahusiano alibaini mpenzi wake huyo ana uhusiano na mtu mwingine"
"Kitendo hicho kilimchukiza na kwa kushirikina na mwenzake waliamua kumuua Editha na kuchukua simu yake ya mkononi kisha Keneth Muganyizi kwenda kuificha simu hiyo ili isipatikane hewani tena" amesema Chatanda.
Aidha ametaja matukio mengine kuwa ni Jafesi Rusolela (52) mkazi Kata ya Kyebitembe wilaya ya Muleba ambaye alikamatwa na silaha aina ya gobole na nyara za serikali ambapo amekuwa akijihusisha na uwindaji haramu wa wanyama pori katika hifadhi ya Burigi Chato.
Wakati huohuo, Chatanda amesema katika oparasheni hiyo pia jeshi hilo limekamata watu watatu kwa tuhuma za wizi wa mashine za kuendesha boti (engine boat) , mitumbwi miwili pamoja na nyavu za kuvulia samaki baadhi zikiwa zimeibwa kwa wavuvi na nyingine haziruhusiwi kuvulia samaki.
Pia ameeleza kuwa, Desemba 25, 2024 hadi Desemba 27,2024 watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa kwa usalama walikamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kemondo Bukoba vijijini, mwalo wa Igabiro kata ya Kishanje Bukoba vijijini pamoja na Muleba.
Mali zilizokamatwa ni pamoja na mashine 10 za kuendesha boti, nane aina ya Yamaha, moja aina ya Mariner na nyingine aina ya Suzuki pamoja na nyavu 184.
Jeshi hilo limesisitiza wale wanaoweza kuthibitisha mali zao zilizokamatwa wakiwa na ushahidi waende kuzitambua.
Katika oparasheni hiyo madereva tisa wamekamatwa na kufungiwa leseni zao kutokana na kuendesha gari wakiwa wamelewa pamoja na mwendo kasi na wote watafikishwa mahakamani.
Madereva hao ni pamoja na Frenk Judika Samwel mwenye leseni namba 4001427021, Hashimu Mikidadi Kitwe leseni namba 4006135351, Rajabu Rashid Mwenda leseni namba 4000114312, Gerald Israel Suluba leseni namba 4006985519.
Wengine ni pamoja na Aizack Stanslaus Henrico hakuwa na leseni, Iddi Juma Ramadhan leseni namba 4001103998, Focus Rwehumbiza Bernad leseni namba 4006957098 na Wilfred Rweyendera Rwegasira leseni namba 4000328053.
Jeshi la polisi mkoani Kagera katika oparasheni ya siku mbili limekamata watu 15 kwa matukio tofauti ya mauaji, wizi pamoja na makosa ya usalama barabarani.
Post a Comment