HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : CHANGAMOTO NDIYO CHACHU

MAISHA ni changamoto, lazima kuzikabili,

Kama huna changamoto, hiyo moja ya dalili,

Bado waishi kitoto, kichwani mwako jadili,

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Wewe hunacho kiwanja, mwenye nyumba kwako dili,

Jinsi anavyokupunja, luku isiyo halali,

Utatafuta kiwanja, nawe uwe na mahali,

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Kodi umechelewesha, tajiri awa mkali,

Hapo analianzisha, umechacha huna hali,

Tazidi jishughulisha, uondoe udhalili,

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Nyie mwakimbia mbio, muweze fika mahali,

Mwenzako atoka mbio, azunguka wewe chali,

Ninakuuma sikio, jichunguze yako hali,

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Yeye ana boda boda, nawe mko sawa hali,

Mepita kidogo muda, ana kiwanja mahali,

Kwa pesa za bodaboda, hujifunzi kitu kweli?

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Wakaanga maandazi, unauzia mahali,

Mwenzako na maandazi, yanaisha hayalali,

Hilo lifanyie kazi, kwa njia zote halali,

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Maendeleo kuiga, hiyo imo ni halali,

Usikae unazuga, huku waumia kweli,

Wala usiende kuroga, huwezi kufika mbali,

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Yale leo ulishindwa, mwaka kesho ni halali,

Hivi ndivyo unafundwa, ili ufanyie kweli,

Vyakutosha umetendwa, mbele hakuna kufeli,

Changamoto ndiyo chachu,kufanya mabadiliko.

Waliojenga daraja, kuvuka iwe halali,

Walichoka na vioja, vya kuopoa miili,

Wao mmoja mmoja, kwake mamba kuwa mali,

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Changamoto acha zije, zituamshe akili,

Tutajua tufanyeje, kuondoa hii hali,

Mabaya na tuyachuje, mema ndiyo yawe mali,

Changamoto ndiyo chachu, kufanya mabadiliko.

Mtunzi wa Shairi ni  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments