HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : MWEZI WA VICOBA

 

MALAIKA wa Desemba, utukumbuke na sisi,

Wanaume tunaomba, kwa wake tupe nafasi,

Hali zetu zinayumba, matemate yawe nasi,

Huu mwezi wa vicoba, na sisi usitupite.


Wenzetu, wanakutana, sasa wanajinafasi,

Ya kugombanagombana, hayo yasiwe na sisi,

Amani tuweze ona, japo tupewe nanasi,

Huu mwezi wa vicoba, na sisi usitupite.


Wapole tutabakia, tusilete mambo hasi,

Vyombo tutasaidia, kuosha tuna nafasi,

Lengo tuweze ingia, kwenye mgao na sisi,

Huu mwezi wa vicoba, na sisi usitupite.


Mbona kama waishia, huu mwezi mambo hasi,

Wake zetu metulia, wala hamchezi nasi?

Vile mmejipatia, hebu tukumbuke nasi,

Huu mwezi wa vicoba, na sisi usitupite.


Ni tarehe za mwishoni, subira kama mkasi,

Tunavyokatwa moyoni, ni kama tuna mkosi,

Kujitolea nyumbani, ni kama tunawaghasi,

Huu mwezi wa vicoba, na sisi usitupite.


Wandugu angalieni, Januari iko nasi, 

Ni ada ziko njiani, zinaleta ukakasi,

Hali hii hamuoni, tukae tupange nasi?

Huu mwezi wa vicoba, na sisi usitupite.


Mtunzi wa Shairi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments