HEADER AD

HEADER AD

BITEKO AWAHIMIZA WAZAWA KUWEKEZA KAGERA

Na Alodia Dominick, Bukoba

NAIBU Waziri mkuu na Waziri wa Nishati hapa nchini Doto Biteko amehamasisha wazawa wa Kagera walioko ndani na nje ya mkoa huo kutumia fursa zilizopo mkoani humo na kurudi kuwekeza nyumbani.

Biteko ameyasema hayo Desemba, 19, 2024 wakati akiwa mgeni rasmi katika kongamano la wafanyabiashara pamoja na tamasha la utamaduni matukio ambayo yamefanyika katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

       Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko akizungumza katika kongamano la wafanyabiashara mjini Bukoba

Amesema kuwa, mkoa wa Kagera unazo fursa mbalimbali za kiuchumi ambazo ni utalii, ujenzi wa hoteli za kitalii, kumbi za mikutano, ujenzi wa viwanda vya samaki na dagaa, maeneo ya kilimo cha kahawa na fursa nyinginezo hivyo akawataka wazawa wa Kagera na wawekezaji wengine kuja kuwekeza Kagera.

"Ijuka omuka ilianzishwa kwa ajili ya kuwahamasisha wazawa wa mkoa wa Kagera wanaoishi ndani na nje ya mkoa huo kurudi kuwekeza nyumbani warudi na kuhamasishana kwa ajili ya kuwekeza kuleta maendeleo katika mkoa wa Kagera kama ilivyo tafsiri yake kumbuka nyumbani.

"Mtakubaliana na mimi kwamba wapo wanakagera wanaishi nje ya Kagera na nje ya nchi na wamefanya mambo makubwa huko wanakoishi tofauti na nyumbani ndo maana kwa kipindi fulani mkoa wa Kagera kasi ya maendeleo ilikuwa si ya kuridhisha kwa sababu ya kukosa mipango ya wazawa wenyewe" amesema Biteko 

Amewaasa wananchi wa mkoa wa  Kagera kuunga mkono  jitihada za mkuu wa mkoa na kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa amesema chimbuko la Tamasha la ijuka omuka (kumbuka nyumbani) ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati alipotembelea mkoa wa Kagera na kuzungumza na wazee wa mkoa huo ameagiza ifanyike tathmini ili kujua sababu za kudorora kwa uchumi na maendeleo ya mkoa wa Kagera.

       Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Innocent Bashungwa akizungumza katika Kongamano la wafanyabiashara

“Wananchi wa Kagera tuna bahati ya kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Rais Samia na utashi wake wa kisiasa kuhusu mkoa wetu kutupa miradi mbalimbali ya maendeleo na hivyo inatupa fursa zaidi ya kukuza uchumi wetu,” amesema Bashungwa.

Ameeleza sababu za kijiografia kwa mkoa wa Kagera pia zinauweka katika nafasi ya kimkakati kuleta maendeleo. Amemshukuru Mungu kwa kuwa mkoa huo upo eneo la kimkakati na unazo rasilimali watu wa kutosha.

Amewakumbusha wengine waliopo maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kukumbuka nyumbani licha ya majukumu waliyonayo huko walipo.

Bashungwa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi ambalo linatarajiwa kuzinduliwa mwezi Februari 2025, ujenzi wa barabara, miradi ya umeme na akazungumzia hitaji la mkoa wa Kagera la kujengewa uwanja wa ndege wa Kajunguti.

Mkuu wa mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema kuwa lengo la Tamasha hilo la pili la uwekezaji la mkoa wa Kagera ni kutoa fursa kwa serikali na mrejesho kwa wadau juu ya  mafanikio na  mipango ya serikali kuhusu uchumi wa mkoa huo.

      Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akizungumzia fursa zilizopo mkoani humo

Akielezea wasilisho lake la miradi na fursa zilizopo mkoani humo, ametaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kuwa ni ujenzi wa barabara za kimkakati zenye urefu wa km 265.4 zinazogharimu Tsh. Milioni 340.49 na ujenzi wa madaraja matano utakaogharimu shilingi bilioni 45.2.

Katika sekta ya kilimo, Mwassa amesema mkoa wake una mikataba miwili ya miradi ya umwagiliaji inayogharimu Tsh. Bilioni 2.9.

Halikadhalika, mkoa huo  unatekeleza miradi mikubwa ya maji minne itakayogharimu kiasi cha Tsh. Milioni 191 na kunufaisha wananchi zaidi 500,000.

        Wafanyabiadhara na viongozi mbalimbali wakiwa katika kongamano la wafanyabishara ni katika wiki ya tamasha la ijuka omuka (kumbuka nyumbani)


Amesema mkoa huo umepakana na nchi jirani nne na mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria na hivyo kuwahakikishia soko la uhakika wa bidhaa.

Amewapongeza wawekezaji mkoani humo kwa kujenga viwanda baada ya kuvutiwa na fursa zilizopo mkoani humo na akahamasisha uwekezaji wa hoteli za kitalii na kumbi za mikutano  mkoani humo.

 “Mikutano hii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki haifanyiki hapa Kagera kwa sababu hatuna uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu, hatuna ukumbi wa kuhifadhi watu 3,000 kwa pamoja hivyo wanalazimika kuifanyia mahali pengine” amebainisha Mwassa.

Vilevile, Mwassa ameonesha kiu yake ya  kuona uwanja wa ndege wa Omukajunguti ukijengwa na kukamilika ili kutoa huduma kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.

       Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati Doto Biteko akikagua banda lenye vitu vya asili ikiwemo zana mbalimbali pamoja na vyakula

Mhandisi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Emannuel Mayanga amesema kuwa kupitia Miradi ya Kupendezesha Miji (TACTIC) kwa manispaa ya Bukoba ni ujenzi wa barabara zenye urefu km 10.75, uwekaji wa taa za barabarani zaidi ya 800 zitakazosaidia kuangaza Bukoba wakati wa usiku, uboreshaji wa kingo za mto Kanoni pamoja na uboreshaji wa soko.

Tamasha la Ijuka Omuka kwa mara ya kwanza lilifanyika mwaka jana na la mwaka huu ni la pili na tamasha hilo litakuwa linafanyika Desemba kila mwaka lengo ni kuonyesha fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Kagera

No comments