WAGANGA WAKUU SHINYANGA WATAKIWA KUHAKIKISHA FEDHA ZA UTEKELEZAJI LISHE ZINATOLEWA KWA WAKATI
Na Suzy Butondo, Shinyanga
KATIBU Tawala wa mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni amewataka Waganga wakuu wote wa halmashauri za wilaya, mkoani Shinyanga kuhakikisha fedha za utekelezaji wa shughuli za lishe zinatolewa kwa wakati.
Pia kuhakikisha wa kusimamia utekelezaji wa mkataba wa lishe, ikiwa ni pamoja na utoaji wa chakula mashuleni.
Agizo hilo amelitoa Alhamisi, Desemba, 19, 2024, wakati akifungua rasmi warsha ya siku mbili ya kutathmini uboreshaji wa huduma za lishe kwa afya ya mama na mtoto, iliyoandaliwa na Shirika la World Vision Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kivulini.
Warsha hiyo pia imewahusisha wadau na asasi za kiraia zinazojihusisha na masuala ya lishe na afya ya mama na mtoto mkoani Shinyanga.
CP Hamduni amesema fedha za utekelezaji wa lishe bado hazijatolewa kwa wakati kwani kati ya kiasi kilichopangwa cha shilingi 384,404,110, kwa kipindi cha Juni 2024 hadi Desemba 17, 2024, kiasi cha Tsh. 165,881,531, kimetolewa, sawa na asilimia 43 tu. hali ambayoinaonyesha kutokuwepo kwa ufanisi katika utekelezaji wa shughuli hizo.
"Nimetoa agizo hili baada ya kuona taarifa ya fedha za kutekeleza afua za lishe zimepokelewa kwa asilimia 43 pekee. Hivyo nawaelekeza halmashauri zote kupitia waganga wakuu kuhakikisha fedha za utekelezaji wa shughuli za lishe zinatolewa kwa wakati," amesisitiza CP. Hamduni.
Amesema ijapokuwa asilimia ni ndogo lakini inaonyesha kuna mafanikio, kwani udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano umepungua kutoka asilimia 32.1 hadi asilimia 27.5, na ukondefu umeshuka kutoka asilimia 4.3 hadi 1.3.
"Hii inaonesha kuwa juhudi zetu za kupambana na utapiamlo zinaanza kuzaa matunda, ijapokuwa kiwango cha udumavu bado ni kikubwa, hivyo tunapaswa kuendelea kusimamia utekelezaji wa afua za lishe," amesema.
CP. Hamduni amelishukuru shirika la World Vision kwa kushirikiana na shirika la Kivulini katika kusaidia mkoa wa Shinyanga kutekeleza afua za lishe na afya ya mama na mtoto kupitia Mradi wa Grow Enrich na Nourish.
Ameishukuru Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kuendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua mbalimbali za afya, ikiwa ni pamoja na lishe na afya ya uzazi.
Mwakilishi kutoka TAMISEMI, Riziki Mbilinyi akizungumza wakati wa Warsha ya Siku mbili ya kutathmini uboreshaji wa huduma za lishe kwa afya ya mama na mtoto
Meneja wa Mradi wa Grow Enrich kutoka Shirika la World Vision Tanzania, Shukrani Dickson, ameeleza kuwa shirika lake linashirikiana na serikali kutekeleza mradi wa miaka mitano, kuanzia mwaka 2023 hadi 2027.
Mradi huo unalenga kuimarisha hali ya afya na lishe kwa wavulana, wasichana, wanaume, na kukuza usawa wa kijinsia katika halmashauri za Wilaya ya Shinyanga na Kishapu.
Meneja wa Mradi wa Grow Enrich kutoka Shirika la World Vision Tanzania, Shukrani Dickson, akizungumza wakati wa Warsha ya Siku mbili ya kutathmini uboreshaji wa huduma za lishe kwa afya ya mama na mtoto, iliyoandaliwa na Shirika la World Vision Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kivulini.
"Mradi wetu huu unafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la World Vision Germany , ambao wanatuwezesha kutoa mafunzo mbalimbali kwa asasi za kiraia ili nazo zikaweze kuhamasisha masuala yalishe katika jamii"amesema shukrani.
Afisa Lishe wa mkoa wa Shinyanga, Yusuph Hamisi, amesema mkoa umeendelea kushirikiana na wadau kupambana na utapiamlo, hasa kwa watoto chini ya miaka mitano, na kupunguza udumavu kwa kutoa elimu ya lishe kwa mama wajawazito na wanaonyonyesha kupitia vituo vya afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yasin Ally, amesema kwamba kikao hicho cha warsha kina lengo la kutathmini utekelezaji wa afua za lishe, afya ya mama na mtoto.
Pia kujadili mipango ya kuboresha huduma hizo mkoani Shinyanga na kujadili utekelezaji wa ahadi za ukuaji wa afua za lishe zilizowekwa na serikali ya Tanzania kwenye mkutano wa Kimataifa wa Tokyo mwaka 2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yasin Ally akizungumza wakati wa Warsha ya Siku mbili ya kutathmini uboreshaji wa huduma za lishe kwa afya ya mama na mtoto, iliyoandaliwa na Shirika la World Vision Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kivulini.
"Licha ya jitihada zinazofanywa, bado kuna changamoto ya ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya lishe na afya ya mama na mtoto, ingawa wanaume wanashiriki katika kilimo, wakati wa mavuno, wengi wanauza mazao, kununua pombe, na kuoa wake wengine, hali inayochangia ugumu katika utekelezaji wa afua za lishe"amesema Ally.
"Baada ya kufanya tathimini yetu katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga tumeona kuna uhusiano kati ya ukatili wa kijinsia na lishe, hivyo kuna umuhimu wa kuwaelimisha wanaume kuhusu mchango wao katika masuala haya.
"Hata hivyo naipongeza serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele cha kipekee masuala ya lishe na afya ya mama na mtoto, na kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa kuboresha sekta hizi muhimu " amesema. Ally.
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo akiwemo Veronica Masawe kutoka Asasi ya kiraia Shinyanga amesema uwepo wa warsha hiyo wameona ni fursa kubwa kwao, hivyo ni wakati mzuri wa kuelekeza nguvu zao kwa jamii ili iweze kuona umuhimu wa lishe na wataendelea kuhamasisha ili jamii itambue makundi ya chakula yaliyopo.
Lukas Daud ambaye ni kiongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali Shinyanga Tanzanian Youth and Children (TYC) wanayashukuru mashirika hayo kwa kuungana na kutoa warsha ya kuwajengea uwezo,hivyo wataendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya lishe ili kuhakikisha utapia mlo na ukatili unaofanywa na wanaume kwa kuuza mazao unatoweka kabisa.
Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Bagelela Kagiye Magana akizungumza wakati wa Warsha ya Siku mbili ya kutathmini uboreshaji wa huduma za lishe kwa afya ya mama na mtoto
Post a Comment