HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: KITIMAGURU


Kiite kitimaguru, ukipenda kitimwendo,

Hicho si kwa watu huru, ambao mwendo mdundo,

Bali kwa wasio huru, afya pia na vifundo,

Hitaji kitimaguru, muhimu sehemu nyingi.


Kama afya mgogoro, huwezi mrefu mwendo,

Wala hakuna godoro, la kupumzika kando,

Moyo usiwe na kero, kama kuna kitimwendo,

Hitaji la kitimaguru, muhimu sehemu nyingi.


Kwa wagonjwa wa dharura, ni muhimu kitimwendo,

Kwa sababu ya kuhara, hawezi kwenda mwendo,

Kuipuka hasara, wakalie kitimwendo,

Hitaji la kitimaguru, muhimu sehemu nyingi.


Kitimaguru sambamba, kuurahishisha mwendo,

Ujenzi wetu wa nyumba, ngazi zisiwe utando,

Kutumia utayumba, mhitaji awe kando,’

Hitaji la kitimaguru, muhimu sehemu nyingi.


Huu wito wetu sote, kukijali kitimwendo,

Tukijenga nyumba zote, ziweze ruhusu mwendo,

Kwa sababu sisi sote, twaweza pata kishindo,

Hitaji la kitimaguru, muhimu sehemu nyingi.


Ni vizuri tuamke, tuvijali vitimwendo,

Mazingira tusichoke, yasapoti wake mwendo,

Watu wasiadhirike, wasiumalize mwendo,

Hitaji la kitimaguru, muhimu sehemu nyingi.


Mtunzi wa Shairi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments