SHAIRI : CHAMCHELA
Usitake usimame, ya kwamba utasalia,
Hata utake ugome, wewe itakufagia,
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Umekaa kwa amani, upepo unakujia,
Waweza toka kusini, hujawahi usikia,
Au wa kaskazini, mkali wa kutishia,
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Jina hilo Chamchela, pengine hujasikia,
Ni upepo unakula, kila kitu wafagia,
Hata kama umelala, nyumba wakuezulia,
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Upepo kisulisuli, ndivyo unaitwa pia,
Unapopiga mahali, inabakia kulia,
Vyote vinasombwa mbali, hakuna cha kubakia,
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Chamchela ni madhara, yanatujiatujia,
Kuharibu mazingira, huko nako kwachangia,
Ni wenyewe twajikera, haya tunajifanyia,
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Lingine kinyamkera, jina umelisikia?
Kimbunga kinatuchora, twabaki twalialia,
Tukitunza mazingira, havitatujiajia.
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Kuharibu mazingira, katika yetu dunia,
Toka bara hadi bara, ambako tunasikia,
Ni chanzo mengi madhara, ambayo yanatujia,
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Matetemeko kadhaa, ambayo twayasikia,
Juzi tulivyochakaa, Uturuki na Syria,
Yameshaleta balaa, watu wengi kujifia,
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Kimbunga cha Msumbiji, hata mafuriko pia,
Vinaleta uhitaji, shida kutuzidishia,
Sababu wetu mtaji, mazingira twajilia,
Ni hata mabadikilo, katika tabianchi.
Chamchela usiombe, bakia ukisikia,
Vitu vyote kivisombe, masikini twabakia,
Waharibifu wachambe, wasijewakarudia,
Ni haya mabadiliko, katika tabianchi.
Mtunzi wa Shairi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment