HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI : TWIGA NI FAHARI YETU

Hakunaga kama Twiga, wanyama wa duniani,

Wengine wote wazuga, kwa urefu duniani,

Tena apendeza Twiga, ukimuona njiani,

Twiga fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Apenda kula vya juu, usafi huko si duni,

Anaona toka juu, anategemewa chini,

Wanamwangalia juu, wanyama walio chini,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Hutembea kwa madaha, mpole huyu mwituni,

Atembeavyo kwa raha, sifa iko mitaani,

Mwanamke wa madaha, Twiga jina mtaani,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Twiga ana shingo ndefu, rahisi kula mitini,

Tena miguu mirefu, anavutia mwituni,

Kwa huo wake urefu, hali hovyo vitu chini,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Kama atembea Twiga, hata kukimbia chini,

Mwendo tofauti Twiga, anapokuwa njiani,

Upande mmoja Twiga, anatembea njiani,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Pia anaweza Twiga, kuruka ruka njiani,

Miguu ya mbele Twiga, na nyuma kiwa mbioni,

Hakuna kulegalega, anapokuwa mwituni,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Ili kusukuma damu, ifike hadi kichwani,

Moyo msukuma damu, moyo mkubwa jamani,

Kilo moja mbili tamu, zafikia ukubwani,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Tena ulimi wa Twiga, ni mrefu kama nini,

Anasaidika Twiga, kupata chakula mitini,

Vivyo maadui Twiga, huona mbali nyikani,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Tembelea mbuga zetu, ufurahie machoni,

Jinsi Twiga hawa wetu, wanavyotamba porini,

Kwa mwendo ni kama watu, madaha yao njiani,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Kwa mimba wanyama wetu, miezi mitano dini,

Hawanao utukutu, hata wakiwa nyikani.

Tusijejangili katu, tuishie gerezani,

Twiga ni fahari yetu, ni nembo ya Tanzania.

Fika kwenye mbuga zetu, waone Twiga nyikani,

Huo utajiri wetu, na wa pekee nchini,

Wengi kwenye mbuga zetu, waleta fedha za kigeni,

Twiga fahari yatu., ni nembo ya Tanzania.

Mtunzi wa Shairi ni  Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments