HEADER AD

HEADER AD

WATU 5216 WAPIMA UKIMWI , KATI YAO TISA WANA MAAMBUKIZI TARIME DC




>> Dkt. Vasomana asema idadi hiyo ni ambao wamepima ndani ya siku 14

> >Waliopima UKIMWI  Desemba 1 katika vijiji vinavyozunguka mgodi ni 269, hakuna mtu aliyekutwa na VVU

>>Watu 1793 ni wagonjwa wa macho

Na Dinna Maningo, Tarime

WATU 5216 katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilaya ya Tarime, mkoani Mara, wamepima afya zao kufahamu kama wana virusi vya ukimwi ambapo kati yao waliopatikana na maambukizi ni watu tisa.

Akizungumza na DIMA ONLINE , Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Dkt. Amin Vasomana amesema  upimaji wa virusi vya ukimwi umefanyika kwa siku 14 ambapo wanaume 5 na wanawake 4 wamepatikana na maambukizi.

       Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Dkt. Amin Vasomana akizungumza 

Amesema katika kilele cha maadhimisho ya siku ya ukimwi Duniani yaliyoadhimishwa Desemba, 01 katika viwanja vya Ingwe sekondari -Nyamongo, watu 269 wamepima afya zao na hakuna mtu aliyekuwa na maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.

Dkt. Amin amesema kabla ya siku 14 za maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, takwimu zinaonesha hali ya ya ugonjwa wa ukimwi imepungua kutoka asilimia 1.7 mwaka jana hadi asilimia 1.5 mwaka huu.

" Idadi  ya waathirika wa ukimwi ni 3584, wanaotumia dawa ni 3443 sawa na asilimia 96% .Tulikuwa na zoezi la upimaji wa ukimwi kwa siku 14 . Watu wamejitokeza kupima maana siku ya kilele iliyofanyika jana , watu 269 wamepima ukimwi na hakuna mtu aliyekutwa na maambukizi mapya" amesema Dkt. Amin.

Dkt. Amin amesema maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi yanapungua  na  sababu moja wapo inayopelekea kupungua kwa maambukizi ni upimaji wa mara kwa mara unaofanyika.



 " Wateja wote wapya wanaopatikana wanaanzishiwa dawa, pia kufanya uchunguzi wa magonjwa " amesema Dkt. Amin.

Mratibu wa ukimwi halmashauri ya wilaya ya Tarime, Geofrey Peter Mkenda ameongeza kuwa kupungua kwa maambukizi ya VVU ni kutokana na jitihada za halmashauri na wadau mbalimbali wa afya ukiwemo mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara kutoa elimu ya kujikinga na ukimwi.

      Mratibu wa ukimwi halmashauri ya wilaya ya Tarime, Geofrey Peter Mkenda akisoma taarifa wakati wa maadhimisho siku ya ukimwi duniani

Amesema jitihada hizo ni pamoja na kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua (PMTCT).

" Jitihada zingine ni Tohara salama kwa wanaume, uhamasishaji wa jamii kujitokeza kupima afya ya akili ili kujua hali zao kwa wale ambao wanakidhi vigezo vya upimaji kwa kufuata mwongozo wa upimaji wa VVU na kutoa elimu juu ya kuchukua tahadhali na kujikinga dhidi ya ukimwi amesema Geofrey.

Diwani wa Viti maalumu Felister Range amesema " Nimefurahi kusikia maambukizi yamepungua lakini tusijiachie kisa maambukizi yamepungua , ikiwezekana yapungue zaidi ya hapo.Tuzidi kutoa elimu ya Ukimwi" amesema Felister.

                Diwani wa Viti maalumu Felister Range akizungumza

Meneja mkuu wa mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, uliopo Nyamongo , Apolinary Lyambiko amesema wao kama mgodi wamejitokeza kusaidia jitihada za kuboresha maisha na kuelimisha jamii na kwamba upimaji ni muhimu.

" Kwa pamoja tunaweza kuondoa unyanyapaa .Nipende kuhimiza kuendelea kuwa na uwazi na kila mtu apate rasilimali anazohitaji. Niwashukuru kwa kuungana nasi katika kujenga maisha bora ya baadae kwa wote" amesema Meneja.

Wakati huo huo,   Zoezi la upimaji wa VVU limeenda sambamba na upimaji wa damu, macho, lishe, malaria na uzito ambapo chupa 66 za damu zimepatikana .

       Wataalam wa afya wakiwapima wananchi uzito wakati wa maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani

Waliopima macho ndani ya siku 14 kuelekea siku ya ukimwi Duniani, watu  1793 wamekutwa na ugonjwa wa macho, kati yao waliopata dawa 602, waliopata miwani 167 na watu 14 watafanyiwa upasuaji na wengine 1,011 watafuatiliwa hali zao baada ya miezi 6 au 8.

Dkt. Amin amesema idadi ya watu waliopimwa hali yao ya lishe kwa kutumia uwiano wa uzito kwa urefu (BMI) ni 114.

" Kati ya hao uzito pungufu (underweight)ni mmoja. Hali nzuri ya lishe(normal nutritional status) ni 70,

uzito uliozidi (overweight) ni 33, uzito uliopitiliza/uliokithiri(obesity) ni 10. Waliopima Malaria jumla ni 115 kati yao aliyekutwa na Malaria ni mmoja" amesema Dkt. Amin.


No comments