Home
/
AFYA
/
HALMASHAURI TARIME VIJIJINI YAELEZA SABABU YA KUPUNGUA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI
HALMASHAURI TARIME VIJIJINI YAELEZA SABABU YA KUPUNGUA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI
Na Dinna Maningo Tarime
IMEELEZWA kuwa sababu ya kupungua maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika halmashauri ya wilaya ya Tarime, mkoani Mara, kutoka asilimia 1.7 mwaka 2023 hadi kufikia asilimia 1.5 mwaka 2024 imetokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na halmashauri ili kupunguza kiwango cha maambukizi
Akisoma taarifa ya maadhimisho siku ya UKIMWI Duniani yaliyoadhimishwa Desemba, 01, 2024 katika viwanja vya Ingwe Sekondari- Nyamongo, Mratibu wa UKIMWI halmashauri ya wilaya ya Tarime Geofrey Peter Mkenda amesema jitihada hizo ni pamoja na kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua (PMTCT).
" Jitihada zingine ni Tohara salama kwa wanaume, uhamasishaji wa jamii kujitokeza kupima afya ya akili ili kujua hali zao kwa wale ambao wanakidhi vigezo vya upimaji kwa kufuata mwongozo wa upimaji wa VVU na kutoa elimu juu ya kuchukua tahadhali na kujikinga dhidi ya UKIMWI." amesema Geofrey.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa dawa za kurefusha maisha (ARV ) kwa ajili ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, amesema upatikanaji wa dawa za ARV hadi kufikia Novemba, 2024 ni asilimia 98.
" Jitihada zaidi zinaendelea kufanyika kuhakikisha kiwango cha upatikanaji wa dawa kinaongezeka ikiwa ni pamoja na kufanya uagizaji wa dawa za ARV kwa wakati toka MSD, sambamba na kuomba wadau kuchangia dawa na vitendanishi kwa ajili ya upimaji mara fursa hiyo inapopatikana" amesema.
Dkt. Godfrey amesema kuwa Serikali inatambua kwamba moja ya makundi yaliyopo kwenye hatari ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI ni pamoja na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Amesema katika mapambao dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI halmashauri imewasogezea huduma wananchi mipira ya kiume (kondomu) kwenye kumbi za starehe , nyumba za wageni, ofisi za serikali ambapo jumla ya mipira ya kiume 112,000 imesambazwa kuanzia Julai 2024.
Amesema changamoto inayoikumba idara ya afya ni uhaba wa watumishi wa kada ya afya . Mikakati imewekwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya kusaidia kutoa mafunzo kwa watumishi waliopo.
Amesema serikali imeweka utaratibu wa kuwawezesha kwa kuyapatia wananchi mikopo isiyo na riba kwa lengo la kuboresha na kuimarisha biashara/shughuli zao kama njia ya kuimarisha vipato na ajira.
Ameeleza kuwa kwa mwaka 2024/2025 kwa robo ya pili Oktoba-Desemba jumla ya Tsh 500,000.00 zinatarajiwa kutolewa . Hadi sasa halmashauri ina jumla ya Tsh 2,480,201,492.75 kwa mikopo ya wanawake , vijana na watu wenye ulemavu.
" Tunaendelea kusisitiza watu wote walio katika makundi hayo wajitokeze ofisi za serikali za vijiji kwa ajili ya kuomba mikopo na kuachana na vitendo viovu na hata wakati mwingine kwenda kukopa kwenye Taasisi zisizo rasmi" amesema.
Ameongeza kuwa serikali katika kuhakikisha wajasiriamali hasa mtu mmoja mmoja ananufaika na fursa za kiuchumi na kuondokana na vitendo viovu, imeweka utaratibu wa utambuzi wa wajasiriamali mmoja mmoja kutambuliwa na kusajiliwa kidigirali na baadae kuweza kukopa mikopo husika kwa masharti nafuu.
Jumla ya Tsh 18,400,000.00 zimetengwa nchi nzima kwa mikopo hiyo itakayotolewa kupitia Benki ya NMB kwa riba ya asilimia 7 tuu ambapo wajasiriamali 325 wamesajiliwa kidigirali na kati ya hao wajasiriamali 80 wamepata vitambulisho.
Hata hivyo Dkt. Godfrey amewapongeza wadau mbalimbali katika mapambao dhidi ya virusi vya UKIMWI wakiwemo PSI wa huduma ya Kinga kupitia utoaji wa kondoma, AMREF, NYP na CDF, BARRICK, RIN CO.LTD.
Katibu Tawala wa wilaya ya Tarime, Mwl.Saul Mwaisenye aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo, Meja Edward Gowele amewahimiza wananchi kujenga desturi ya kupima afya zao kila mara na wakigundulika watumie dawa.
"Wanafunzi jiepusheni na vitendo vya uzinifu. Chagua njia sahihi kutokomeza UKIMWI, pia kupata ugonjwa kuna visababishi vingi hivyo tusiwanyanyapae watu" amesema Mwl. Saul.
Afisa Rasilimali watu Kampuni ya ujenzi ya RIN, Peter Nyambushwa amewatia moyo watu ambao wamejigundua kuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kuwa sio mwisho wa maisha dawa zipo za kurefusha maisha.
Meneja mkuu wa mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara , Apolinary Lyambiko amesema wao kama mgodi wamejitokeza kusaidia jitihada za kuboresha maisha na kuelimisha jamii na kwamba upimaji ni muhimu.
" Kwa pamoja tunaweza kuondoa unyanyapaa .Nipende kuhimiza kuendelea kuwa na uwazi na kila mtu apate rasilimali anazohitaji. Niwashukuru kwa kuungana nasi katika kujenga maisha bora ya baadae kwa wote" amesema Meneja.
Diwani wa Viti maalumu Felister Range ameishukuru Serikali,mgodi wa Barrick North Mara na Kampuni zingine zilizofanikisha maadhimisho hayo.
" Nimefurahi kusikia maambukizi yamepungua lakini tusijiachie kisa maambukizi yamepungua , ikiwezekana yapungue zaidi ya hapo.Tuzidi kutoa elimu ya UKIMWI" amesema Felister.
Mganga mkuu halmashauri ya wilaya ya Tarime , Amini Vasomana ameushukuru mgodi wa North Mara kudhamini maadhimisho siku ya UKIMWI Duniani.
Pia amemshukuru mlezi wa idara ya afya katika halmashauri hiyo ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya ujenzi ya RIN kwa ushirikiano na kujitoa kusaidia masuala mbalimbali ya afya.
Ugonjwa wa UKIMWI ni ukosefu wa Kinga mwilini baada ya virusi vya UKIMWI kushambulia chembeche nyeupe za damu zenye uwezo wa kuukinga mwili usishambuliwe na magonjwa mbalimbali.
Post a Comment