GARI LA SAMIA LAWAPATANISHA WAITARA NA MASWI
>>DC Tarime amshukuru Rais Samia asema gari limeleta upatanisho
>>Maswi asema hana ugomvi na Waitara atampatia kompyuta akazikabidhi shuleni, atema Nyongo
>> Waitara afupisha maneno amfuata na kuketi nae, wateta jambo
>>DC Chacha amwomba Waitara na Maswi kuwapuuza wanaowaletea taarifa za uchonganishi
>>Katibu CCM Tarime awanyooshea kidole wapambe
Na Dinna Maningo, Tarime
WASWAHILI wanasema kwamba wagombanao ndio wapatanao, msemo huo umejidhirisha kwa vigogo wawili kati ya Katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na sheria nchini, Eliakim Maswi na Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini ,Mwita Waitara ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawaelewani na hivyo kujikuta wakiwa maadui.
Habari zinasema kuwa kutoelewana kwa vigogo hao ni kutokana na bifu za kisiasa, inadaiwa kuwa Waitara anadhani Maswi anaweza kugombea jimbo la Tarime vijijini jambo linalompa shaka mbunge Waitara na hivyo kujikuta wakichukiana huku wapambe wao wakidaiwa kuwa ndio wanaowachonganisha viongozi hao.
Desemba, 27, 2024, Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele alifika katika Kituo cha afya Magoto Kata ya Nyakonga, kukabidhi gari la wagonjwa wa dharura jambo lililobainika kuwa ujio wa gari hilo lililotolewa na serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umesababisha vigogo hao wawili Maswi na Waitara kupatana na kuketi pamoja.
Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele akikata utepe wakati akikabidhi gari la wagonjwa kituo cha afya Magoto lililonunuliwa na serikali.
Wananchi na mkuu wa wilaya wakiwa wanasubiri kuanza kikao cha makabidhiano ya gari, punde si punde mbunge Waitara akawasili, baada ya dakika chache wazawa wa Kata ya Nyakonga ambao ni viongozi serikalini na wapo kijijini rikizo nao wakafika kwenye makabidhiano.
Viongozi hao wazawa ambao ni Katibu Mkuu Eliakim Maswi na Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma , Simon Chacha kwa nyakati tofauti wakatinga katika tukio la kituo cha afya kukabidhiwa gari la wagonjwa .
Wakati wazawa hao wanawasili walikuta Mbunge Waitara akihutubia wananchi waliofika kushuhudia makabidhiano , ambapo Maswi alitangulia kufika kisha DC Chacha nae akawasili.
Wananchi wakiwasikiliza viongozi wakati walipofika kukabidhi gari la wagonjwa kituo cha afya Magoto.
Ukistahajabu ya Musa utaona ya firauni Mbunge Waitara alipomuona DC Chacha amefika kikaoni alionekana mwenye furaha na ndipo akamtambulisha DC Chacha na kumpa nafasi kuzungumza na DC akawasalimu wananchi.
Hali hiyo ikaleta mshangao kwa wananchi baada ya Mbunge Waitara aliyekuwa akizungumza kumtambulisha DC Chacha huku akiacha kumtambulisha Katibu mkuu aliyekuwa amewasili kabla ya DC Chacha na kuishia kuwatambulisha viongozi wengine na kumuacha kiongozi huyo mkubwa wa kitaifa.
Akitoa salamu za Chama, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM ) wilaya ya Tarime, Noverty Kibaji akampongeza Rais Samia kwa kutoa gari kwa ajili ya kuhudumia wananchi kituo cha afya Magoto huku akiwaonya wanaccm na wananchi wanaowachonganisha Waitara na Maswi na kuwataka kuacha mara moja.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM ) wilaya ya Tarime, Noverty Kibaji aliyesimama mwenye kipaza sauti akizungumza.
" Namshukuru sana Rais Samia kutoa gari, hili gari leo limewakutanisha Waitara na Maswi uso kwa uso, kukaa meza moja ilikuwa ni shughuli pevu kwao. Niwaambie mimi nitaendelea kusimamia Katiba ibara ya 83 kifungu cha 6.
" Wale wanaotengeneza uchonganishi wakiwemo wanaccm na wananchi waache, tuwasaidie hawa viongozi wa Tarime washikamane. Nimeyasema haya kwasababu nimewakuta takribani wote wapo hapa, wakunielewa amenielewa" amesema Katibu wa CCM.
Ameongeza na kusema " Naomba watu tunaochukua taarifa upande A kupeleka upande B au kuchukua taarifa upande B na kupeleka upande A tuache , hawana ndio watu hatari kuliko kitu chochote" amesema Noverty.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Simon Chacha, ameipongeza serikali inayoongozwa na Rais Samia kwa jitihada inazofanya kuboresha sekta ya afya na kwamba amefika na kukuta gari hivyo shukrani zake anazielekeza serikalini.
Akizungumzia kutoelewana Maswi na Waitara amesema viongozi ndio wana makosa kwa kupokea taarifa zisizo na ukweli na kuzifanyia kazi.
" Wakati mwingine sisi viongozi ndio tuna makosa kwanini tuyapokeee na kuyafanyia kazi tunayoletewa na watu?. Ukiwauliza kila mmoja sababu ya kukosana hakuna majibu. Naomba viongozi akili za kuambiwa changanya na zako.
" Adui namtengeneza mimi mwenyewe, adui hatengenezwi na mtu naomba Maswi na Waitara tufanye kazi, Maswi aheshimiwe. Kama serikali imemuheshimu ikampa kazi basi aheshimiwe. Na Waitara ndiye aliyechaguliwa na wananchi tumuheshimu hadi pale chama kitakaposema Waitara ubunge umekoma" DC Chacha.
Maswi atema nyongo
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Simon Langoi akampatia kipaza sauti Katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria nchini, Eliakim Maswi ili awasalimu wananchi.
Katibu mkuu amesema yeye hana ugomvi na Waitara na anamuheshimu kama mbunge na kwamba yeye hajawahi kutangaza kokote kuwa anataka kugombea ubunge na endapo muda ukifika na akitaka kugombea atagombea kwani si dhambi yeye kugombea ubunge Tarime vijijini.
Katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria nchini, Eliakim Maswi aliyevaa kofia akisalimiana na mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele.
" Mimi sina ugomvi na Waitara kwasababu Magoto ni nyumbani kwetu mimi sijawahi kusimama mbele yenu nikasema nataka ubunge isipokuwa wamenitangaza wao . Malema anajua, Katibu wa chama anajua sijawahi kusimama tawi hata moja, Kijiji hata kimoja au Kitongoji nikasema nataka ubunge.
"Lakini wamenitangaza na mimi nimefurahi kwasababu sasa hivi nimejulikana jimbo zima. DC mimi ni mwana Tarime naipenda Tarime na nikitaja vitu nilivyovifanya hata mbunge mwenyewe anajua hawezi kusimama mbele yangu, hivyo ni lazima tushirikiane sisi wananchi wa Tarime kujenga jimbo letu" amesema Eliakim.
Katibu mkuu huyo amewataka wakurya kuacha wivu huku akimwomba mbunge Waitara kushirikiana pamoja kama vile wabunge waliotangulia walivyokuwa wakishirikiana nae na kwamba anaumia anapotaka kuleta maendeleo Tarime lakini anapingwa.
" Baadhi yetu Wakurya tuna wivu wa kijinga sana mimi nilipaswa tukae na Waitara tupange jinsi ya kuendeleza hapa sio kutafutana , alipokuwa Chacha Wangwe tulikuwa tunakaa pamoja tunapanga miradi na Tarime ilisonga, alipokuja Mwera tulikuwa tunakaa nae tunapanga maendeleo miradi ikakimbia kwa kasi.
" Barabara ni mbovu imeshindwa kupitika kwasababu ya ubishi wa hapa kwetu Mwenyekiti Kilesi ni shahidi niliomba Milioni 378 ili kituo hiki cha afya kipanuke lakini matokeo yake mbunge Waitara akapiga simu pesa zisije Magoto" amesema.
Eliakim ameongeza kusema " Huku ni kwetu lazima niumie, kwenye uongozi wangu nilileta umeme huku, nikatukanwa mpaka bungeni , kwahiyo mimi naumia, naomba niseme leo naumia kwasababu nachotaka kije Tarime hasa kwetu nina pingwa.
" Mimi sina hela ila kwenye uongozi wangu niliomba hela serikalini nikasema pelekeni sola Manga, Mbogi, Magoto, Bungurere, nilikuwa naangalia Tarime yetu si kwa ajili yangu. Mimi ni mteule wa Rais na mimi ninapenda nikifika nyumbani angalau nipewe heshima kuwa mimi nae ni mwenzenu nisaidie ninachosaidia.
" Shule ya sekondari Magoto nilipambana mpaka ukaletwa umeme wa Tsh Milioni 100 hakuna mwananchi aliyechanga. Nilikaa na wazee nikasema shule ya sekondari ya wasichana ya Borega ikijengwa kama madarasa yatakuwa Bukira basi nyumba za walimu ziweze Nyabasi hamtapigana na hawajawahi kupigana tena" amesema.
Ameongeza kusema " Sasa ukifanya hivi watu wanaona wivu , kwanini tuoneane wivu kwetu? Tarime itajengwa na wanatarime tusioneane wivu . Nikuhakikishie mbunge Waitara nina kuheshimu , nitakutii mpaka bunge litajapovunjwa kama kuna shida niambieni.
" Lakini nikifanya kitu anasema nataka Ubunge. Hivi nani asiyejua hapa nilivyokulia kwa shida mimi nilidharauliwa kwasababu ya umasikini, sasa mimi sipendi ndugu zangu walionilea wawe masikini kama nilivyokuwa mimi nikisaidia kosa.
" Mimi naumia sana maana wakurya hatubebani, wachaga wao wakikutana wanakaa pamoja wanajadiliana maendeleo lakini sisi tukikaa tunatukanana , asiyeezeka nyumba yake mvua itamnyeshea .
" Nikifanya hivi nataka ubunge hata nikionekana nimekuja kusalimia ndugu zangu wanasema nataka ubunge, kwani nikitaka ubunge ni kosa ?hapa ni kwetu imeandikwa wapi ni kosa mimi kugombea? isipokuwa ninamheshimu mbunge kwa sababu ndiye mwenye mamlaka kwa sasa ila nao waniheshimu" amesema.
Amesema kuna viongozi wenye vyeo vikubwa serikalini wanaotoka Tarime lakini wameshindwa kufanya maendeleo Tarime kwasababu wakionekana wanawatuhumu kuwa wanataka ubunge na hivyo kushindwa kusaidia maendeleo.
"Kuna watu wakubwa sana serikalini wanatoka Tarime , kuna mkurugenzi mkubwa sana huko serikalini anatoka kwenye kata hii Kijiji cha Kebweye .Wakurugenzi wanaotoka hapa Tarime wenye vyeo si chini ya 30 ninao wajua mie, lakini hawaji kwasababu kila ukionekana eti unatafuta kitu.
" Kuna tajiri mkubwa sana mzawa wa pale Nyamwaga Waitara anamjua lakini wanaogopa wakija itaonekana wanataka vyeo sisi wenyewe tunajipinga maendeleo. Waitara naomba tufanye kazi mimi sitakugusa na sikugusi , Katibu wa chama upo hapa sijawahi kusimama mahali kokote nikasema Waitara mbaya" amesema Eliakim.
Eliakim amemhakikishia mkuu wa wilaya kuwa watashirikiana kuleta maendeleo Tarime " Ningefurahi sana nikisema kuna kitu fulani kinaenda mahali mh. mbunge atangulie mimi kazi yangu ni kumsindikiza.
" Nitanunua kompyuta tano na fotocopy mashine ( mashine ya kudurufu) nitakupa mbunge uzipeleke uzikabidhi kwenye Tarafa tatu, shule ya Magoto nimeichagua mimi shule zingine wewe utaona unapelekea shule gani " amesema Eliakim .
Waitara asema akijibizana hapatatosha
Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara amemuomba Katibu mkuu kushirikiana na kwamba hayo mambo mengine ni mambo ya kupita kisha wakaketi pamoja na kuteta jambo.
Kushoto ni mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara akiteta jambo na Katibu mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi.
" Nikisema na mimi nijibu hapa hapatatosha ndio maana nimeona nikae kimya , tupeane ushirikiano haya mengine ni mambo ya kupita wewe ukituita tuunganishe tufanye kazi vizuri wananchi wakupongeze.
" Kila mtu aache alama kwa nafasi yake , wewe ni Katibu mkuu lakini na mimi niliwahi kuwa Naibu Waziri, Katibu mkuu anaagizwa na Naibu Waziri na mimi nilikuwa na cheo kikubwa tutabishana tu bure tufanye kazi" amesema Waitara.
Diwani akerwa na wachumia tumbo
Diwani wa kata ya Nyakonga ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Simon Kilesi amekerwa na waandishi wa mitandaoni wakazi wa Nyakonga wanaondika vitu wasivyovijua huku akimshauri Katibu mkuu kuachana na wachumia tumbo wanaompatia taarifa za uongo.
"Kuna watu wanaandika vitu kwenye mitandao ambavyo hawavijui, kuna watu wanatumiwa ndani ya Nyakonga ndio maana hata mimi sishughuliki nao. Sisi maendeleo tunayapenda wakishirikiana na sisi ni furaha kwetu. Mbunge na Maswi washirikiane tukipata maendeleo Nyakonga nani atakataa? hakuna wa kukataa sisi tunachohitaji ni maendeleo.
Ametoa tahadhali kwa viongozi wa chama Kata ya Nyakonga na kata zingine " Viongozi wa chama mkishirikiana vizuri na viongozi wetu mkaongea lugha moja na viongozi wa serikali tutafanya mambo makubwa sana ndani ya Kata zetu .
" Mh. Maswi umesema kuna matajiri wakubwa ambao ni watumishi tunaomba mtukumbuke hapa nyumbani kwa maendeleo, tuache propaganda za wachumia tumbo , wale wachumia tumbo wanakudanganya kwa maneno unawapa vihela wanakula alafu wananchi wanahangaika.
" Wale wachumia tumbo ukiachana nao tukakubaliana tukafanya kazi kwa kuungana hakika tutafanya maendeleo. Hatuwezi kusumbuliwa na wachumia tumbo wawili au watatu , hao wachumia tumbo wasipokaa vizuri wakaungana na sisi kwa ajili ya maendeleo hata mimi mwenyewe nitapambana nao wanatusumbua sana." amesema Diwani.
DC Tarime amshukuru Rais Samia
Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele, amempongeza Rais Samia kwa kutoa gari na kwamba gari hilo limesababisha mbunge Waitara na Katibu mkuu kupatana.
" Raha sio Raha? wananchi wakajibu Raha. Naomba kila mmoja ajue jina halisi la Samia Suluhu na ndio maana unaona haya yote yametokea leo ,yawezekana ilikuwa vigumu sana kuwakutanisha viongozi hawa wote lakini mama Samia leo katukutanisha kupitia gari hili.
" Mama kwa kumleta ndama huyu amefanya hata viongozi wamekuja hapa kila mmoja ameongea na nina amini tunaenda kwenye Suluhu ya pamoja kama jina la Dkt. Suluhu lilivyo. Rais amekuja na 4R yaani R nne ikamaanisha , maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na tujijenge upya yaani tuanze upya " amesema DC .
DC Edward ameongeza kusema" Hapa niliacha kila kiongozi afunguke kwahiyo leo yawezekana tumekuja kutengeneza Suluhu kubwa hapa . Nafurahi kumuona mbunge wangu na Katibu mkuu wanaongea vizuri.
Gari lililotolewa na serikali kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa likiwa kituo cha afya Magoto lililokabidhiwa na mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele.
" Labda kuna watu walikuwa wanawachonganisha washindwe na walegee, leo wameaibika kwasababu wananchi wangu hawataki marumbano wanataka maendeleo. Nimpongeze mbunge anafanya kazi nzuri anatusemea vizuri bungeni ndio maana tunaona maendeleo yanakuja.
" Nimpongeze Diwani wa kata kwa kazi unayofanya. Nakushukuru DC Tunduru kuna mambo umeyazungumza nilikuwa siyajui kuja kwako hapa ni neema kwangu . Nikushukuru Katibu mkuu Maswi kuja hapa umeweza kuyasema na mbunge ameyasema na tumeona kuna watu wanatuchonganisha.
" Ninyi nyote mnafanya kazi nzuri kila mmoja ametema nyongo na leo ambulance imetuunganisha, tukitoka hapa tuongee pamoja na ninajua watashirikiana. Mmewaona wamekaa pamoja kama mapacha ndicho tunachotaka. Katibu wa CCM nina kushukuru sana yawezekana wewe ndio ulikuwa mchokoza mada" amesema DC.
Amehimiza kuwa maendeleo hayawezi kuja pasipo ushirikiano na viongozi na kutowabagua na kwamba kukiwa na umoja wa pamoja Tarime itakuwa na maendeleo makubwa.
DC Edward amewaonya wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii huku akiwataka wananchi kuwapuuza wanaochonganisha viongozi kwenye mitandao.
Kulia ni mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara akiteta jambo na Katibu mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi aliyesimama katikati.
" Wale ambao wanatuchonganisha hasa kwenye mitandao ya kijamii hebu tuwapuuze lakini naomba niwaonye tunaotumia vibaya mitandao kuna sheria ya mitandao , tunakoelekea kwasababu wanatuchonganisha wanawagawa viongozi wetu lazima tuwashughulikie tutalisimamia vizuri" amesema DC Edward.
Post a Comment