SERIKALI YAKABIDHI GARI LA WAGONJWA KITUO CHA AFYA MAGOTO
>>DC Tarime asema gari hilo litarahisisha usafiri kwa wagonjwa wa dharura
>> Ataka gari litoe huduma nzuri kwa wananchi bila ubaguzi
>> Wananchi wasema wamepata unafuu
Na Dinna Maningo, Tarime
MKUU wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele amekabidhi gari la wagonjwa wa dharura kituo cha afya Magoto, Kata ya Nyakonga lililotolewa na serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan huku akisisitiza gari hilo litumike vizuri bila ubaguzi.
Kutolewa kwa gari hilo (Ambulance) kutasaidia kuondoa kero kwa wananchi wa kata hiyo na kata za jirani wanaopata changamoto ya usafiri pindi wagonjwa wanapopewa rufaa kwenda hospitali ya wilaya ya Tarime.
Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele akiwa ndani ya gari baada ya kulikabidhi kituo cha afya Magoto.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo wakati akikabidhi gari la wagonjwa kituo cha afya Magoto, Desemba, 27, 2024 ambapo viongozi mbalimbali wa serikali na chama cha mapinduzi wameshiriki.
"Namshukuru Rais Samia kwa namna anavyoboresha sekta ya afya , niwaombe wasimamizi wale ambao tunaenda kusimamia gari tukatende haki, kusiwepo usumbufu wala ubaguzi wa mwananchi yeyote katika kupata huduma " amesema DC Edward.
Amewataka wasimamizi wa gari hilo kuhakikisha linatoa huduma ya afya na sio kufanya shughuli zingine na kusema kuwa gari hilo ni la wananchi sio la biashara lipo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.
Mkuu wa wilaya ya Tarime Meja Edward Gowele akikata utepe wakati wa kukabidhi gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha afya Magoto lililotelewa na serikali kuu.
"Gari hili sio la biashara kama gharama zitakuwepo mganga atatoa utaratibu na zitakuwa gharama ndogo za huduma na sio biashara. Rais amekuwa akifanya kazi kubwa kuleta vifaa tiba.
" Ameongeza watumishi. Rais anachapa kazi tukisema tuelezee kila kitu tunaweza tusimalize hadi kesho tuendelee kumuombea Rais " amesema Meja Edward.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, Simon Langoi amesema moja ya majukumu ni kuboresha huduma ya afya na kwamba kama halmashauri wataendelea kuboresha huduma za afya.
Amesema katika halmashauri hiyo kuna vituo 11 vya afya na kwamba kuna gari nne za gari za wagonjwa wa dharura na gari ya mganga mkuu.
Mbunge wa Jimbo la Tarime Mwita Waitara, amesema kuwa gari hilo itarahisisha usafiri kwa wagonjwa wanaopatiwa rufaa.
Kulia mwenye kipaza sauti ni Mbunge wa Jimbo la Tarime vijijini, Mwita Waitara akizungumza wakati wa kukabidhiwa gari la wagonjwa kituo cha afya Magoto.
" Tulikaa na madiwani tugawanya namna gari hizo zitakavyokuwa zinafanya kazi. Kuna gari la wagonjwa tumeweka kule kituo cha afya Nyangoto litakalohudumia katika zahanati na vituo kule Kwihancha, Kerende , Nyarwana, Mtana n.k .
"Gari la pili linakaa pale halmashauri ambalo litakuwa linabeba wagonjwa katika hospitali ya Halmashauri, na Zahanati, walipopewa rufaa kwenda Musoma au Mwanza.
Ameongeza " Gari nyingine Iko pale kituo cha afya Sirari itahudumia zahanati na vituo vya afya vilivyopo ukanda huo kama Bumera, Ganyange n.k wanaopewa rufaa kwenda hospitali ya wilaya ya Tarime. Hii gari ya hapa Magoto itahudumia Nyakonga , Binagi, Ganyange na maeneo jirani " amesema Waitara.
Mganga Mfawidhi
Mganga Mfawidhi kituo cha afya Magoto , Dkt. Hamisi Rossana ameishukuru serikali kwa kuwapatia gari na kwamba huduma ya usafiri wa dharura itapunguza usumbufu wa kusubiri kwa muda mrefu gari la wagonjwa pindi linapohitajika kupeleka rufaa ngazi nyingine ya matibabu.
Gari la wagonjwa lililotolewa na serikali ili kutoa huduma kwa wagonjwa katika kituo cha afya Magoto .
Amesema kituo hicho kinahudumia wakazi 20,547 . Amesema mahitaji ya kituo ni watumishi 37 , upungufu ni watumishi 22, ambapo kwa mwezi kina hudumia wagonjwa wa nje 700.
" Kituo kina watumishi 15 wa fani mbalimbali wenye ajira ya kudumu ( MD-1, AMO-1, CO-1, RN-4, LAB-2, MA-2), pia kituo kina watumishi wa mkataba 3 wanaolipwa kupitia mapato ya kituo na mfadhili AMREF ( Data ofisa (DO)-1 wa mkataba, mlinzi-1 wa mkataba, mfanya usafi 1 wa mkataba.
" Wagonjwa wa kulazwa 100, wakina mama wanaojifungulia kituoni kwa mwezi ni 80, wanaojifungua kwa upasuaji ni takribani akina mama 10 kwa mwezi" amesema.
Wananchi wakishiriki makabidhiano ya gari la wagonjwa lililotolewa na serikali kwa ajili ya kituo cha afya Magoto.
" Idadi ya zahanati zinazozunguka kituo hiki cha afya ni Zahanati ya Nyantira, Rosana, Kemakorere, urafiki, Kebweye, Borega, Kimusi na Ntagacha. Kituo kinaweza kutoa rufaa 3-6 kwa mwezi kwa wamama wajawazito , watoto wachanga 1-3 kwa mwezi" amesema Dkt. Hamis.
Diwani wa Kata ya Nyakonga Simon Kilesi ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime, amesema katika uongozi wake kituo hicho kilipatiwa fedha ikiwemo zaidi ya Tsh. Milioni 40 zilizokarabati maabara, Tsh. Milioni 115 za ujenzi wa nyumba ya mganga.
Diwani wa Kata ya Nyakonga Simon Kilesi ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime akizungumza
"Milioni 10 za kuchomea taka , Milioni 60 zimetengwa kwa ajili ya chumba cha uhifadhia maiti na zaidi ya Milioni 200 zimetengwa kujenga jengo la mama na mtoto litakalojengwa na mkandarasi kutoka mgodi wa Barrick North Mara na fedha hizo ni za mapato ya ndani na za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii CSR kutoka Barrick" amesema Simon.
Wananchi wamshukuru Rais
Wananchi wa kata ya Nyakonga wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kukipatia kituo gari na kusema kuwa kituo cha afya kutokuwa na gari wagonjwa waliteseka.
Mwenyekiti wa bodi ya kituo cha afya Magoto, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Magoto, Gabriel Matiko amesema " Akina mama waliteseka sana ilipohitajika matibabu zaidi Dkt. alilazimika kupiga simu kuita gari kutoka kituo cha afya Nyangoto-Nyamongo.
Mwenyekiti wa bodi ya kituo cha afya Magoto, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Magoto, Gabriel Matiko akizungumza.
" Unakuta mama kazidiwa gari Iiko mbali matokeo yake anapoteza maisha. Kwakuwa gari limekuja tunaomba wananchi tusichangishwe fedha za kusafirisha wagonjwa wa rufaa tukashindwa kuzimudu , watu wakikosa huduma kwa sababu ya gharama basi hili gari litakuwa halina faida kwetu" amesema Gabriel.
Elizabeth Mwita amesema ukosefu wa gari la wagonjwa akina mama walipata changamoto ya usafiri" Tunamshukuru Rais kwa kutuletea gari , ili uende hospitali ya wilaya unalazimika kupanda pikipiki sh. 3000 hadi Kemakorere kisha unalipa tena usafiri wa gari 3000 -5000 kwenda Tarime na kurudi hivyo hivyo.
" Mgonjwa alipozidiwa usiku ilikuwa shida mpaka utafute gari binafsi ukodi na ni moja linalofanya safari zake kwenda Tarime asubuhi kurudi hadi jioni, ukitaka kukodi kwenda Tarime ni 20,000 gharama zinazwashinda baadhi, hivyo wengine kupoteza maisha kutokana na kukosa usafiri kwa wakati na gharama za nauli" amesema Elizabeth.
Katika makabidhiano hayo ya Gari, Katibu Mkuu Wizara wa Katiba na Sheria , Eliakim Maswi na mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Simon Chacha ambao ni wazaliwa katika kata hiyo ya Nyakonga na wapo rikizo kijijini hapo wameipongeza Serikali kukipatia kituo gari ya wagonjwa ambayo itaondoa changamoto kwa wagonjwa wa dharura.
Katika makabidhiano hayo ya Gari, Katibu Mkuu Wizara wa Katiba na Sheria , Eliakim Maswi aliyevaa kofia akiteta jambo na mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele wa kwanza kulia aliyevaa suti nyeusi.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Simon Chacha akizungumza.
Post a Comment