HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI YA MJI WA KIBAHA KUZINDUA SOKO LA KISASA



Na Gustaphu Haule, Pwani

HALMASHAURI ya Mji Kibaha inatarajia kufanya uzinduzi wa Soko kubwa la Kisasa (Kibaha Shopping Mall) ambalo ni mradi wa kimkakati likiwa na lengo la kuinua uchumi wa wafanyabiashara.

Uzinduzi huo utafanyika Desemba 7, 2024 katika eneo la Soko hilo lililopo karibu na stendi kubwa ya mabasi.

Afisa  masoko wa Soko la kibiashara Kibaha ,(Kibaha Shopping Mall)Sabrina Kikoti amewaambia Waandishi wa habari kuwa maandalizi ya uzinduzi huo yamekamilika na kwamba mgeni rasmi wa uzinduzi huo anatarajia kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimoni.

      Afisa Masoko wa Soko la Kibiashara Kibaha Mjini ( Kibaha Shopping Mall) Sabrina Kikoti akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Soko hilo utakaofanyika  Kesho Desemba 7,2024 .lililopo karibu na stendi Kuu ya mabasi Mjini Kibaha

Amewaomba wafanyabiashara wote waliopo Kibaha Mjini ,wadau na Wananchi kujitokeza katika uzinduzi huo kwa ajili ya kujionea fursa zilizopo na hata kupata urahisi wa kununua bidhaa zinazopatikaka katika Soko hilo.

Sabrina amesema kuwa soko hilo ni mradi mkubwa wa kimkakati lililojengwa kwa ajili ya kutoa fursa ya  wafanyabiashara wakubwa na wadogo sambamba na kupanua uchumi wa Kibaha Mjini.

Amesema, Soko hilo lina vyumba 74 ikiwemo sehemu ya Super Market ,biashara za jumla , biashara ndogondogo,benki,maduka ya madawati sehemu ya michezo Kwa watoto,eneo la maegesho ya magari pamoja na mambo mengine mbalimbali muhimu.

        Soko la Kisasa la Kibaha Mjini linalotarajia kuzinduliwa kesho Desemba 7,2024.

"Kibaha inakwenda kufunguka kiuchumi kutokana na uzinduzi wa Soko letu kubwa la Kisasa kwahiyo tunawakaribisha watu mbalimbali kuja katika uzinduzi huu muhimu ambao unatoa fursa za kiuchumi na fursa za ajira kwa Watanzania,"amesema Sabrina.

Ameongeza kuwa katika uzinduzi huo kutapambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wa Bongofleva akiwemo Maarifa na Smatta kutoka Kibaha Mjini pamoja na kundi la wasanii la Weusi kutoka Jijini Dar es Salaam.

Amempongeza Rais Dkt .Samia kwa kuridhia kutoa fedha nyingi za kukamilisha mradi huo lakini pia amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kusimamia vizuri mradi huo mpaka kukamilika.

Amesema mgeni rasmi katika uzinduzi wa Kibaha Shopping Mall ni mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimoni ambaye katika uzinduzi huo.

Afisa Mapato wa Halmashauri ya mji Kibaha Luna Kakuru ,amesema kuwa soko hilo ni Soko la kimkakati na limetumia Jumla ya Tsh.bilioni 8 fedha ambazo zimetoka Serikali Kuu.

        Afisa Mapato wa Halmashauri ya Mji Kibaha Luna Kakuru akizungumza na waandishi wa habari juu ya matarajio ya mapato katika Soko kubwa la Kisasa linalotarajia kuzinduliwa kesho Desemba 7,2024 lililopo Stendi Kuu ya mabasi Kibaha Mjini

Amesema kuwa Soko hilo linakwenda kuwa sehemu ya mapato ya Halmashauri ya Mji Kibaha ambapo wanatarajia kukusanya Kodi ya Sh.milioni 660 kwa mwaka .

"Soko hili limetumia Tsh.bilioni 8 kutoka Serikali Kuu na matarajio yetu ni kukusanya mapato ya milioni 660 Kwa mwaka hivyo tuwaombe wadau mbalimbali kujitokeza katika uzinduzi huu muhimu,"amesema Luna.

Aidha ,baadhi ya wafanyabiashara akiwemo Lidya Vicent, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Soko hilo kwakuwa limesaidia kufungua fursa kwa wafanyabiashara wa Mji wa Kibaha.

        Mfanyabiashara wa Kibaha Shopping Mall Lidya Vicent akizungumza na waandishi habari kuhamasisha vijana kutumia fursa la uwepo wa Soko la Kisasa la Kibiashara lililopo Mjini Kibaha (Kibaha Shopping Mall) linalotarajia kuzinduliwa kesho Desemba 7,2024.

Lidya, amesema awali walilazimika kusafiri umbali mkubwa mpaka kufika Soko la kimataifa la Kariakoo lililopo Jijini Dar es Salaam lakini kwasasa kila kitu kitapatikana Kibaha na hivyo kuondoa usumbufu wa kwenda Dar es Salaam.

Nae Charles Chandika,mfanyabiashara wa dawa za mifugo na Kilimo,amefurahi kuwepo kwa Soko hilo kwakuwa litakwenda kuwa Soko kubwa la kibiashara na hivyo kutoa fursa kwao katika kuendeleza biashara zao.

       Mfanyabiashara wa Soko la Kisasa lililopo Kibaha Mjini (Kibaha Shopping Mall) Charles Chandika akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa Soko hilo katika Mji wa Kibaha

Chandika ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kukamilisha mradi huo huku akisema Rais Samia anapaswa kuungwa mkono kwa kazi nzuri anazozifanya.

          Soko la Kisasa la Kibaha Mjini

No comments