HEADER AD

HEADER AD

MGANGA MKUU TARIME ATOA ELIMU KWA WAGANGA WA TIBA ASILI, WAKUNGA WA JADI



>>Dkt. Vasomana atoa maelekezo

>> Asema atakapoanza kuchukua hatua asilaumiwe 

>> Jacob Sira awasisitiza waganga wa tiba asili kusajili dawa zao

Na Dinna Maningo, Tarime

MGANGA mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Amin Vasomana amewataka waganga wa tiba asili , tiba mbadala na wakunga wa jadi kuzingatia taratibu na miongozo ya serikali katika utoaji huduma za afya.

Amewataka waganga wa tiba asili na wakunga wa jadi ambao wanafanya kazi bila kusajiliwa kuhakikisha wamesajiliwa na kutozalisha wajawazito majumbani badala yake wawaelekeze wakapate huduma katika vituo vya kutokea huduma ya afya na kwamba atakapoanza kuchukua hatua asilaumiwe.

    Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Amin Vasomana akizungumza na waganga wa tiba asili, tiba mbadala na wakunga wa jadi

Mganga huyo ameyasema hayo Desemba, 05, 2024 wakati alipokutana na waganga wa tiba asili na wakunga wa jadi kwa lengo la kufahamiana, kuwakumbusha kuzingatia mwongozo wa afya wanapotoa huduma zao za afya pamoja na kuwapa maelekezo ili kuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wananchi.

"Niwaombe mliyojifunza mkayafanyie kazi . Mimi natamani sana sisi wote tuliokuja leo waganga wa tiba asili na tiba mbadala, wakunga wa jadi mjisajili muwe na vyeti halali ili msipate usumbufu, tufanye kazi zilizo na usalama na ubora unaotakiwa.

" Kuna watu wamevunjika miguu sehemu nyingi nyingi lakini mganga bado analazimisha kukaa nae. Wakati mwingine tufanye kitu ambacho tunakiweza. Ukifanya kitu ambacho huna uwezo nacho mgonjwa atakufia. Usitake kujipatia mafao ya fedha wakati mwenzako anakufa" amesema Dkt. Amin.

Amewataka wakunga wa jadi kutowapa wajawazito dawa za kuongeza uchungu kwani ni hatarishi ikiwa ni pamoja na kutozalisha wajawazito waliofanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua na badala yake wawasaidie kuwapeleka vituo vya kutolea huduma ya afya.

   Baadhi ya waganga wa tiba asili, tiba mbadala na wakunga wa jadi halmashauri ya wilaya ya Tarime wakiwa kwenye mafunzo

" Ushaona mama mjamzito ana kovu ameshafanyiwa oparesheni wewe unakaa nae nyumbani, ushaona damu zinatoka ,unaona mgonjwa ana watoto wawili tumboni kwakuwa alishaambiwa wakati wa kliniki bado unakaa nae ili akupe Tsh 30,000.

" Mgonjwa anakuja unamwongezea dawa ya uchungu badala ya uchungu aliopewa na Mungu wewe unamwongezea uchungu unaenda kwa kasi matokeo yake tumbo la uzazi linapasuka kwasababu umempa dawa bila kipimo matokeo yake anapata matatizo" amesema.

Dkt. Amin amesema hakuna haja ya kujifungulia majumbani kwani Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikijenga vituo vingi vya afya na kuongeza watoa huduma.

       Baadhi ya waganga wa tiba asili, tiba mbadala na wakunga wa jadi halmashauri ya wilaya ya Tarime wakiwa kwenye mafunzo

" Zamani tulisumbuka kupata vipimo kwasababu ya umbali lakini saizi vipimo vipo kwenye vituo vyetu. Niwaombe wenzangu sisi hatuna nia mbaya, mnachokifanya hakipo kwenye mwongozo wa tiba asili na kikao kingine tutakaa na wale waliosajiliwa tu kwahiyo mkajisajili.

" Serikali inatambua tiba asili inawatambua waganga wa tiba asili na wakunga wa jadi lakini zingatieni taratibu. Tumeitana hapa tufahamiane tupeane maelekezo na vikao hivi vitakuwa endelevu ,tutapanga bajeti walau tuwe tunakutana mara nne kwa mwaka au mara mbili kwa mwaka ili tuelekezane na tujadili changamoto mnazokutana nazo kwenye kazi" amesema Amin.

Mratibu wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto halmashauri ya wilaya ya Tarime, Beatrice Luomba amesema kwa sasa vituo vya afya, zahanati, hospitali zimeongezeka huku akiwataka kupiga simu ya huduma namba 115 endapo watahitaji msaada wa haraka wa mgonjwa kufuatwa na gari kupelekwa kupata huduma ya afya.

      Mratibu wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto halmashauri ya wilaya ya Tarime, Beatrice Luomba akizungumza na waganga wa tiba asilia na wakunga wa jadi

Mwakilishi Taifa wa chama cha tiba asili kanda ya ziwa (CHAWATIATA) na Mjumbe wa kamati ya maadili baraza la tiba asili na tiba mbadala , Jacob Sira amewahimiza waganga wa tiba asili na tiba mbadala kuhakikisha wanasajiliwa na wasajili dawa zao ili ziweze kuuzika na kupata soko.

Mwakilishi huyo wa chama cha tiba asili na tiba mbadala ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia kwa kujenga hospitali ya tiba ya asili nchini pamoja na kuruhusu dawa za asili ziuzwe kwenye maduka ya dawa katika hospitali za serikali.

     Mwakilishi Taifa wa chama cha tiba asili kanda ya ziwa(CHAWATIATA) na Mjumbe wa kamati ya maadili baraza la tiba asili na tiba mbadala , Jacob Sira akizungumza na waganga wa tiba asili na wakunga wa jadi

" Sasa hivi ukienda hospitali usipotaka dawa za hospitali utapata dawa za tiba asili, na hata hapa DMO anaweza kuruhusu tukawa na duka la tiba asili katika hospitali ya halmashauri. Mnachotakiwa ni kuhakikisha mnasajili dawa zenu.

"Ukiwa na dawa yako nzuri inatibu vizuri inaingizwa sokoni kutoa huduma. Nawaomba tusajili dawa zetu ili ziuzike zipate soko mataifa ya nje. Ukifika kwa mratibu wa halmashauri atakuelekeza hatua zote za kufuata kusajili dawa kama tulivyoelekezana hapa" amesema Jacob.

Ameongeza kuwa serikali imeanza kusajili mganga mmoja mmoja na wasaidizi wake hivyo ni vyema waganga wa tiba asili na wakunga wa jadi wakasajiliwa ili waweze kufanya kazi zao bila bughudha.

" Gharama za usajili ni Tsh. 35,000, vijijini, mjini ni Tsh 55,000 , kusajili eneo mganga wa tiba au mkunga analofanyia kazi ni Tsh 25000 wasaidizi Tsh 10,000. Lengo kujiwekea ulinzi wa kazi yake maana kuna waganga wanakuja wanafikia gesti wanatoa huduma wakiharibu wanaondoka alafu lawama zinabaki kwa waganga wenzake" amesema.

Mganga wa tiba asili mkazi wa Sirari, Hawa Nyakorema amemshukuru mganga mkuu kukutana nao kuwakumbusha jinsi watakavyofanya kazi kwa kufuata mwongozo wa wizara ya afya.

        Mganga wa tiba asili mkazi wa Sirari, Hawa Nyakorema

" Nimejifunza pindi mjamzito anapokuja kwako mpe ushauri wa kwenda kituo cha afya , vilevile nimejifunza endapo nikipata mgonjwa ambaye hali yake sio nzuri kuweza kutibiwa na mkunga wa jadi basi nimwambie aende hospitali kama hakuna usafiri nipige namba 115 gari litakuja litambeba " amesema Hawa.

Paul Shigolile mmiliki wa duka la dawa za tiba asili mkazi wa Sirari ameishukuru ofisi ya mganga mkuu kwa mafunzo waliyopewa  na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi.

     Paul Shigolile mmiliki wa duka la dawa za tiba asili mkazi wa Sirari

" Nimefurahi kupata mafunzo nitaenda kuwashauri wenzangu kuwaelekeza tuliyojifunza .Nimejifunza kwamba watu wakija kutoa huduma ambao hawana vibali tutoe taarifa. Hii itatusaidia waganga wa tiba tusisumbuliwe na Polisi pindi waganga wageni wanapokuja kutoa tiba hatarishi alafu wanaondoka lawama tunapewa sisi" amesema Paul.

Mkunga wa jadi mkazi wa Kijiji cha Nyamwigula kata ya Binagi, Anjerina Chacha ambaye amekuwa akitoa huduma ya ukunga kwa miaka 15 ametaja changamoto anayokutana nayo kwenye kazi.

        Mkunga wa jadi mkazi wa Kijiji cha Nyamwigula kata ya Binagi, Anjerina Chacha

" Ukimwambia mjamzito njia ya kujifungua sio nzuri aende hospitali hataki analazimisha ajifungulie kwa mkunga wa jadi. Wakati mwingine nalazimika kuwachukua kuwapeleka hospitali hata kwa gharama zangu" amesema.

Afisa ustawi halmashauri ya wilaya ya Tarime , Siwema Silvester amewasisitiza waganga wa tiba asili, tiba mbadala na wakunga wa jadi kuchangamkia fedha za mkopo zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya vijana.

      Wataalam wa afya na viongozi wa tiba asili

    Mwenyekiti wa Chama cha tiba asili wilaya ya Tarime, Edwini Simgukwe 





No comments