REACTS IN KUSAIDIA KUONDOA TATIZO LA UTAPIAMLO NA UDUMAVU SIMIYU
Na Samwel Mwanga, Maswa
WAKULIMA wa wilaya za Meatu na Maswa katika mkoa wa Simiyu wameanza kupatiwa mbegu za mazao yenye virutubisho mahindi lishe, viazi lishe na maharagwe lishe ili wazipande katika musimu huu wa kilimo.
Lengo la kusambazwa kwa mbegu hizo ni juhudi za mkoa huo kupambana na utapiamlo na udumavu hasa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Afisa Kilimo Wilaya ya Maswa, Masalu Lusana(kushoto)akimkabidhi mbegu ya mahindi lishe Mkulima mmoja katika kijiji cha Malekano.
Kaya 10,500 kwa mwaka huu zinatarajiwa kunufaika, na hii inaweza kusaidia kupunguza tatizo la utapiamlo na udumavu miongoni mwa watoto wa mkoa huo.
Mradi wa REACTS IN unatekelezwa katika wilaya hizo, mbegu za mazao hayo hutolewa kwa wakulima ngazi ya familia kupitia vikundi vyao vilivyobainishwa na shirika la world vision Tanzania.
Esther Simfukwe, Mratibu wa mradi huo akizungumza Desemba,16 mwaka huu na baadhi ya wakulima katika vijiji vya Buyubi na Malekano wilayani Maswa amesisitiza umuhimu wa usimamizi wa maafisa ugani ili kuhakikisha mbegu hizo zinapandwa kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya ya lishe kwa jamii.
Mratibu wa mradi wa Reacts In,Esther Semfukwe akizungumza na wakulima wa kijiji cha Buyubi wilayani Maswa(hawapo pichani).
“Mradi huu tunaoutekeleza hapa mkoa wa Simiyu ni mpango unaolenga kuhakikisha usawa wa kijinsia na kuboresha mifumo ya lishe kwa wanawake, wasichana, na watoto walio chini ya miaka mitano.
“Pia tunalenga kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hasa kilimo, kuvunja vizuizi vya kitamaduni vya kijinsia, na kuboresha mifumo ya afya na lishe,”amesema.
Amesema kuwa sababu kuu za utapiamlo zinahusishwa na lishe duni, mila za kitamaduni, ukosefu wa elimu ya lishe bora, pamoja na upatikanaji mdogo wa huduma za afya bora na maji safi na ndiyo maana wameamua kusambaza mbegu hizo.
Joyce Joseph ni mkulima mkazi wa kijiji cha Malekano amesema kuwa upungufu wa virutubisho muhimu katika mwili wa binadamu kama vile chuma, zinki, na vitamini husababisha udumavu wa mwili na akili hivyo watazipanda mbegu hizo ili kukabiliana na tatizo hilo.
“Kuna vitu tunavikosa katika miili yetu kama vile vitamin, chuma na zinki kupitia chakula tunachokula hivyo kupitia mbegu hizi ambazo tumepatiwa nitahakikisha nazipanda na kutunza mashamba nitakayolima ili tuweze kukabiliana na suala hili la utapiamlo na udumavu.”amesema.
Ofisa Kilimo wilaya ya Maswa , Masalu Lusana amesema kuwa mkoa huo unakabiliwa na changamoto kubwa ya utapiamlo na udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano na takwimu zinaonyesha kuwa tatizo hili linaathiri takribani asilimia 30 hadi 40 ya watoto katika mkoa wa Simiyu.
Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Buyubi wilaya ya Maswa wakiwa wamebeba mbegu zilizoongezewa virutubisho za mahindi lishe na maharage lishe wazizogawiwa na Mradi wa Reacts in.
“Wananchi wengi wanategemea vyakula vya wanga pekee, bila kuchanganya na protini na mbogamboga, jambo linaloendeleza hali hii. Ili kukabiliana na tatizo hili.
"Juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika, zikiwemo miradi ya kilimo cha mazao yenye virutubisho kama haya yanayosambazwa na mradi huu wa Reacts In pamoja na utoaji wa elimu ya lishe kwa jamii,”amesema.
Mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha miaka saba unafadhiliwa na serikali ya Canada kupitia kupitia Global Affairs Canada kwa gharama ya dola milioni 44, katika Vijiji 146 vilivyoko katika Kata 25 za wilaya ya Maswa.
Pia katika Vijiji 50 Kata 25 wilaya ya Meatu kwa kushirikiana na mashirika mengine ambayo ni pamoja na HarvestPlus, World Vision, na Nutrition International.
Post a Comment