HEADER AD

HEADER AD

KIKUNDI CHA WAKULIMA KEGONGA-MATONGO NA MBIO ZA KUJIINUA KIUCHUMI

Na Dinna Maningo, Tarime

WASWAHILI wanasema kwamba jembe  halimtupi mkulima, ikamaanisha ya kwamba mtu yeyote anayekubali kushika jembe na kwenda kulima lazima atapata mazao.

Ili kuhakikisha kilimo kinasonga mbele na kinakuwa tija katika kuinua uchumi wa watu waishio vijijini hususani wakulima inahitaji nyenzo kuhakikisha mkulima hakwami katika shughuli za kilimo.

Katika Kijiji cha Matongo baadhi ya wakulima hususani wazawa, wakazi wa Kitongoji cha Kegonga A na Kegonga B ,wakiwemo wanawake na wanaume wameanzisha kikundi cha wakulima.

     Wanakengonga Group-Matongo wakiwa kwenye halfa ya kuvunja mzunguko wa mwaka iliyofanyika Kitongoji cha Kegonga A Kijiji cha Matongo-Nyamongo

Kikundi hicho kinajulikana kwa jina la Kegonga Group - Matongo kilichopo Nyamongo wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara, kikiwa na lengo kumkwamua mkulima kiuchumi na katika shida na raha.

Hivi karibuni Desemba, 19, 2024, wana Kegonga Group -Matongo walifanya sherehe ya kugawana fedha kutokana na hisa zao baada ya kuanzishwa kwa kikundi hicho, Septemba, 30, 2023.

Katibu wa Kegonga Group -Matongo , Fransisco Zakayo anasema kikundi hicho kilianza na wanachama 8 na hadi sasa kina wanachama 29.

   Katibu wa Kegonga Group -Matongo Fransisco Zakayo akizungumza

Anataja malengo ya kikundi hicho ni kuwawezesha wakulima waliomo katika kikundi hicho kujikwamua kiuchumi, kusaidiana kwa shida na raha, kukopeshana fedha kwa masharti nafuu, kuanzisha na kuendesha miradi ya kiuchumi, kilimo na biashara ili kukuza pato kwa kila mwanakikundi.

" Pia malengo yetu ni kununua uwanja kwa ajili ya kujenga ofisi ya kikundi . Tulianza kama kikundi tu cha kucheza mchezo wa kuchangishana fedha na sasa tunatoa hisa.

" Kikundi chetu tumekitambulisha ofisi ya mtendaji wa kijiji na tumeandaa katiba siku yoyote tutaipeleka kwa afisa maendeleo ya jamii na hatua zingine za kukisajili" amesema Francisco.

Ameongeza " Tunawakaribisha watu kujiunga na kikundi chetu bila kujali dini, kabila, chama . Tunaomba ushirikiano katika kulijenga Taifa, pia tunaomba zinapotokea fursa za vikundi kama vile mikopo ya vikundi , maonesho, tunaomba ushirikiano ili tuweze kusonga mbele" anasema Katibu.

Mhasibu wa kikundi cha Kegonga, Defroza Sadock ambaye ni mwanzilishi wa kikundi hicho anasema aliamua kuanzisha kikundi ili kusaidiana kujikwamua kiuchumi na katika shida mbalimbali .

     Mhasibu wa kikundi cha Kegonga, Defroza Sadock ambaye pia ni mwanzilishi wa Kengonga Group -Matongo 

" Mnapokuwa watu wawili, watatu, watano na zaidi mnapeana mawazo ya kutafuta uchumi wa kimaisha . Leo tumekutana kuvunja mzunguko wa mwaka, tumegawana fedha ambazo ni hisa tulizokuwa tunacheza kisha Januari, 2, mwaka ujao tutaanza tena kutoa hisa.

" Tumevunja mzunguko kwa kiasi cha Tsh. Milioni 13 na laki saba, kati ya fedha hizo kuna za hisa, mfuko wa jamii na adhabu.  " anasema.

Anasema kuwa mhasibu anatakiwa kuwa mwaminifu kwani asipokuwa mwaminifu ni rahisi watu kujiondoa kwenye kikundi.

Mhasibu wa kikundi cha Kegonga, Defroza Sadock  wa poli kulia , kushoto ni Katibu wa Kegonga Group -Matongo Fransisco Zakayo, kulia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kegonga A, Ibrahimu Ngea wakiwa kwenye hafla ya kuvunja mzunguko wa kikundi hicho

" Mhasibu ukiwa mwaminifu wakati wa kuvunja mzunguko wanakikundi wakipata fedha zao bila dhuluma hufurahi sana na kuhamasika kuendelea na kikundi. Tumegawana hela kila mtu amevuna alichopanda na kupata haki yake kulingana na pesa zake za hisa alivyokuwa akitoa.

" Tulikubalina kila mwanakikundi aje na mme wake au mke wake kwenye sherehe tumejumuika na waume zetu. Kikundi kimemvutia mme wangu na amesema ana eneo la kuuza hivyo kama kikundi tunataka ardhi tuzungume nae .

" Mimi binafsi nimetoa zawadi kwa wanakikundi 15 waliofanya vizuri kwenye kikundi, waliokuwa na mawazo mazuri kwenye vikao, nidhamu. Tumapeta watu wapya watatu wanaohitaji kujiunga na kikundi chetu, tunawakaribisha na wengine waje wajiunge" anasema Defroza.

Josephina Steven ni mtunza nidhamu wa kikundi hicho  anasema changamoto alizokutana nazo ameweza kukabiliana nazo na kuwekana sawa.

         Mtunza nidhamu kikundi cha Kegonga, Josephina Steven akizungumza

" Huwa tuna adhabu simu ikiita faini ni Tsh sh. 2000, ukiongea kilugha badala ya kiswahili faini ni sh. 2000,  ukichelewa Tsh. 2000 maana muda wa kufika kwenye kikundi ni saa 9:00 alasiri hadi saa 9:6,  utoro faini ni 5000 . Hadi tunavunja mzunguko tumepata faini 232,000" anasema Josephina.

Ester Maseke anawashukuru wanakikundi kwa kumjali wakati wa shida kwamba kijana wake alipopata ajali ya pikipiki wanakikundi walimtembelea nyumbani kwake na kumfariji na kumpatia kiasi cha fedha kama pole zilizochangwa na wanakikundi.

  Mwanakikundi cha Kegonga Ester Maseke

Anasema hivi karibuni kijana wake alipata ajali ya pikipiki, wanakikundi walifika nyumbani kwake kumfariji na kumpatia fedha kama mchango wa pole.

Mkami Daud amefurahi kupokea fedha kiasi cha Tsh. 860,000 " Nitaenda niangalie kama ntanunua tofari au mawe nirekebishe mji wangu ,pesa hii itanipunguzia changamoto ya kiuchumi" anasema Mkami ".

            Mwanakikundi Mkami Daud

Mme wa Defroza, ambaye ni Katibu na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Matongo, Sadock Maningo anasema akina mama wakiwezeshwa wanaweza na kwamba anafurahi mkewe kujiunga na vikundi.

" Ili ufanikiwe lazima umshirikishe mke katika maamuzi, namshirikisha mke wangu kwenye mawazo , kila anachonielekeza kinaenda sawa, hata nikimshirikisha kwenye matumizi mambo yanaenda sawa.

        Katibu na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Matongo, Sadock Maningo

" Nimeweka chini wivu nina wivu wa maendeleo. Ukishakuwa na wivu wa maendeleo nina imani mke atatafuta na ataleta. Namwamini mke wangu nikisahau pesa kwenye mfuko wa suruali wakati anafua huniambia nimesahau pesa na kunipatia hafichi , nikimwachia hela kutunza naipata kwa wakati" anasema Sadock .  

Anasema yeye hana wasiwasi na mkewe huku akiwaomba wanawake wanapopata uwezo wasiwadharau waume wao na badala yake washirikiane katika kila jambo kwa ajili ya maendeleo yao.

Baadhi ya wanaume huwazuia wake zao kujiunga katika vikundi kwa madai kuwa pesa wazipatazo hazisaidii familia zaidi ya kujinufaisha wao wenyewe na wengine kutumia vikundi kijihusisha na mapenzi nje ya ndoa zao.

Fikra hizo zinakuwa tofauti kwa Zakayo Sadock ambaye ni mme wa mwanakikundi Mariam Meshaki yeye anasema kuwa mwanamke kujiunga kwenye kikundi ni njia moja wapo ya kumpima akili.

                 Zakayo Sadock

" Kabla mke hajashika hela huwezi kumtambua akili yake ikoje , anapokuwa ameshika hela ndio unatambua akili yake ikoje, akichukua pesa akabadilika hapo utatambua kuwa mwanamke akiwa na hela si mwanamke mwenye tabia njema.

" Ninamwamini mke wangu na wakati mwingine asipokuwa na hela ya kikundi huwa nampatia hela yangu apeleke kwenye kikundi. Siku wanafunga hesabu pesa aliyopata alikuja akaniambia na leo amenialika kwenye sherehe nimekuja.

Zakayo anasema kuwa amefurahishwa na kikundi na kwamba pesa aliyoipata mkewe wameipangia matumizi huku akiwaomba wanaume wenzake kuwaruhusu wake zao wafanye biashara na kujiunga kwenye vikundi.

       Baadhi ya waume wa wanakikundi cha Kegonga wakishiriki halfa ya kikundi

" Huyu akiwa anatafuta huku na mwingine anatafuta ni moja wapo ya maendeleo hujui nani ndiye atakayepata , mwanamke akiwa kwenye kikundi na wewe unatafuta mnawekeza huku na kule huko ndio kupiga hatua mnasonga mbele" anasema Zakayo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kegonga A, Ibrahimu Ngea amefurahishwa na kikundi hicho kutokana na umoja wao na ushirikiano.

     Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kegonga A, Ibrahimu Ngea akizungumza wakati wa halfa ya kikundi cha Kegonga.

" Nimeona jinsi wanavyofanya sherehe yao, kugawana hisa zao, kitendo hicho kimenifurahisha , nimeona malengo yao yatakayowainua yenye maendeleo endelevu. Pia wanalenga kuwasaidia wasio jiweza kama wazee, vijana, wanawake.

" Nimefurahi kuona watu hawa wanavyofanya kazi kwa umoja, wanafanya kazi kwa kushirikiana kila mtu anawajibika kulingana na nafasi yake aliyopewa kwenye kikundi" anasema Ibrahimu.

    Wanakikundi cha Kegonga wakimkabidhi vitu mke wa mwanakikundi baada ya mmewe kupata madhira hivi karibuni walipomtembelea nyumbani kwake .

Wanakikundi wakiwa kwenye hafla ya kuvunja mzunguko iliyofanyika wiki iliyopita. 

















No comments