UJENZI WA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA WAFIKIA ASILIMIA 80
Na Suzy Butondo, Shinyanga
UWANJA wa ndege unaoendelea kujengwa katika kata ya Ibadakuli manispaa ya Shinyanga mkoani hapa, umekamilika kwa asilimia 80, ambapo tayari Ndege za dharura zimeanza kutua katika uwanja huo.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mhandisi Ruburi Kahatano kutoka Kampuni ya CHICO, ambao wanajenga uwanja huo, baada ya kutembelea waandishi wa habari mkoani Shinyanga,kuona maendeleo ya upanuzi wa ujenzi wa uwanja huo wa ndege amesema asilimia 80 uwanja huo umekamilika ambapo ndege zinaweza kutua nyakati za mchana.
Mhandisi wa ujenzi wa upanuzi uwanja wa ndege Shinyanga Ruburi Kahatano akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea uwanja huo."Kweli uwanja huu umekamilika kwa sehemu kubwa na tayari kuna ndege mbili za dharura zimeshatua katika uwanja huu , ambapo moja ilitua kwa ajili ya kubeba mgonjwa kumpeleka hospitali ya Mlonganzila Dar es Salaam kwa matibabu zaidi ya kibingwa na kuokoa maisha yake, na sasa mtu huyo ni mzima"amesema Kahatano .
Mhandisi Chiyando Matoke kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)Mkoa wa Shinyanga, ambao ndiyo wasimamizi wa ujenzi wa uwanja huo, amesema ulianza kujengwa Aprili mwaka jana, na unatarajiwa kukamilika Aprili mwakani, kwa gharama ya sh.bilioni 44.8 bila VAT, na kwamba umekamilika kwa asilimia 80.
Mhandisi Chiyando Matoke kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga akizungumzia upanuzi wa ujenzi wa uwanja wa ndege Shinyanga.“Tunamshukuru Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha kwa ajili ya matengenezo ya uwanja huu na matokeo yake tumeanza kuyaona.
"Ndege kubwa na ndogo zitatua hapa kwasababu uwanja ni mkubwa na kwa sasa zinaruhusiwa kutua mchana, lakini usiku haziweze sababu bado hatujafunga taa tukishamaliza zoezi la kufunga taa zinaweza kutua,”amesema Matoke.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru, amesema katika ziara hiyo, wameshuhudia kazi kubwa ambayo inafanywa na serikali, juu ya ujenzi wa miradi ya kimkakati.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru akizungumza baada ya kutembelea uwanja wa ndege."Tumejionea kazi nzuri iliyofanyika hapa ya ujenzi wa uwanja wa ndege, ambapo wamesema imekamilika kwa asilimia 80 na kukamilika kwa uwanja huu wa ndege, utafungua fursa za kiuchumi katika mkoa wa Shinyanga, hivyo tunaamini kwamba wananchi watasafiri kwa wakati na watafika kwa wakati"amesema Kakuru.
Meneja mradi wa upanuzi ujenzi wa uwanja wa ndege Shinyanga Shi Yinlei kutoka Kampuni ya CHICO akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea uwanja wa ndege
Post a Comment