HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI YAFUNGUA MAABARA YA KUPIMA SAMPULI 651 HOSPITALI YA RUFAA CHATO

Na Daniel Limbe, Chato

KATIKA kile kinachoonekana ni kujiimarisha katika tiba za kibingwa na bobezi kwenye hospitali ya rufaa kanda ya Chato(CRZH) serikali imefungua maabara kubwa ya kisasa yenye uwezo kwa kupima sampuli 651 kwa siku moja.

Hatua hiyo inatajwa kuwa mapinduzi makubwa ya kimatibabu ikilinganisha na awali ambapo ililazimika mgonjwa kusubiri majibu kwa zaidi ya mwezi mmoja.

        Mwonekano wa mbele wa hospitali ya rufaa kanda ya Chato

Mbali na hilo,mtambo mkubwa wa tiba hewa (Oksijeni) umeweza kupunguza adha kubwa kwa baadhi ya hospitali na vituo vya afya vilivyopo ukanda wa ziwa Victoria kutumia fedha na muda mwingi kutafuta huduma hiyo jijini mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari,Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya kuambukiza kutoka hospitali hiyo,Dkt. Lameck Mabirika,amesema kuanzishwa kwa hospitali ya rufaa kanda ya Chato imesaidia sana jamii kupata matibabu yenye uhakika pasipo kulazimika kwenda hospitali ya Bugando jijini mwanza na hospitali ya taifa Muhimbili.

     Mtaalamu wa maabara akitoa maelezo ya ubora wa mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kupima sampuli 651 za magonjwa mbalimbali kwa siku moja.

Aidha imewasaidia wananchi kutumia gharama kidogo za matibabu  na kunusuru muda mrefu ambao walikuwa wakiutumia kusafiri na kuuguza wagonjwa wao badala ya kutumia muda huo kuzalisha mali.

Dkt. Mabirika amesema kutokana na hali hiyo,serikali imelazimika kufunga mitambo mikubwa ya kisasa yenye kusaidia kupatikana huduma  za matibabu yenye uhakika na kwa haraka ili kunusuru kupotea kwa nguvu kazi ya taifa na badala yake kuwa na jamii yenye afya bora na yenye furaha.
       Mashine ya kuzalisha hewa tiba kwenye hospitali ya rufaa kanda ya Chato

"Tunazo mashine mpya na za kisasa za maabara ambazo zinauwezo wa kupima sampuli 651 kwa siku moja,ambapo mpaka sasa tunatoa huduma ya kupima na kutoa majibu ya sampuli za wingi wa virusi vya ukimwi kwa haraka zaidi ukilinganisha na awali ambapo mgonjwa walipaswa kusubiri zaidi ya mwezi mzima"amesema

"Kufungwa kwa mashine hizo kumesaidia sana baadhi ya hospitali na vituo vya afya vilivyopo kwenye mkoa wetu wa Geita, Kagera na mkoa wa Kigoma ambapo wanalazimika kuleta hapa sampuli za magonjwa na kupatiwa majibu haraka zaidi"amesema Dkt.Mabirika.

Akizungumza na viongozi pamoja na baadhi ya wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali hiyo, kwa lengo la kuhamasisha huduma bora,utunzaji wa mazingira, utunzaji wa vyanzo vya maji na kutoa faraja kwa wagonjwa, Katibu tawala wa wilaya ya Chato,Thomas Dimme, amewataka watanzania kuendelea kuwaenzi waasisi wa taifa letu kuelekea miaka 63 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania bara) disemba 9 ,2024 kutokana na mafanikio makubwa ya kimaendeleo.
Katibu tawala wilaya ya Chato,Thomas Dimme(DAS) akiwa na wataalam wa afya  alipotembelea hospitali hiyo

"Haya maendeleo yote tunayojivunia leo ni jitihada kubwa zilizofanywa na waasisi wetu pamoja na wapigania uhuru wengine ambao baadhi yao walipambana kwa jasho na damu ili kuhakikisha tunapata uhuru ili tujitawale wenyewe badala ya kukaliwa na wakoloni".

"Huduma na miundombinu hii tunayoiona leo ndiyo tafsiri sahihi ya uhuru tulioupata mwaka 1961, mambo mengi na makubwa yamefanyika  kwa kipindi hiki cha miaka 63 ya uhuru wetu,nami nitumie fursa hii kusisitiza kuendelea kulinda amani,umoja na mshikamano tuliokabidhiwa na waasisi wetu"amesema Dimme.

Hellena Busumilo(mgonjwa) ameipongeza serikali kwa kuendelea kudumisha amani na kutekeleza miradi mbalimbali inayohusu maisha ya wananchi moja kwa moja hasa waliopo vijijini ambao awali walikuwa wakipoteza maisha kutokana umbali na gharama kubwa kufika kwenye matibabu ya kibingwa na bobezi.

Hata hivyo, katika ziara yake katibu tawala wa wilaya hiyo kwenye hospitali ya rufaa kanda ya Chato imeambatana na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa ikiwemo fedha taslimu, sabuni za kufulia na kuongea,miswaki na dawa za meno,mafuta ya kupaka pamoja na kutoa salaam za rais Samia Suluhu Hassan kuelekea miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara.

Katibu tawala wilaya ya Chato,Thomas Dimme(Das) kimjulia hali mgonjwa.

                        

No comments