DC AWAOMBA WANANCHI KUPATA BIDHAA SOKO LA KISASA MJI WA KIBAHA
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimoni amezindua Soko la kisasa la Halmashauri ya Mji Kibaha ( Kibaha Shopping Mall) huku akiishukuru Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyoweza kutoa pesa nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Soko hilo.
Saimoni amezindua soko hilo Desemba 7,2024 hafla ambayo imefanyika kwa kuwajumuisha wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa Mji wa Kibaha,Wananchi ,watumishi wa Halmashauri pamoja na wadau wengine wa maendeleo.
Katika uzinduzi huo Saimoni amesema kuwa Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha fedha za ujenzi wa soko hilo zinapatikana na kufanya kazi iliyokusudiwa ndio maana limekamilika kama ilivyopangwa.
Ameongeza kuwa bila mkono wa Rais kukubali na kutoa fedha hizo ni wazi kuwa soko hilo lisingekamilika ambapo amewataka wafanyabiashara wa mji wa Kibaha, Wananchi na wadau kuendelea kumuunga mkono Rais ili aweze kutekeleza mipango yake ya maendeleo Kwa wananchi.
"Kibaha tumepata soko la kisasa la kimkakati ambalo linakwenda kuinua uchumi wa Kibaha,wafanyabiashara na hata kuongeza pato la Halmashauri na Taifa kwa ujumla hivyo ni vyema tukamshukuru Rais Samia kwa kazi hii kubwa aliyoifanya,"amesema Saimoni
Aidha Saimoni amesema kuwa kwa sasa haina haja ya kwenda Mlimani City wala Kariakoo kwakuwa kila kitu kitapatikana katika soko hilo ambapo amewaomba wananchi kutembelea soko hilo ili kujionea bidhaa zilizopo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa amesema kuwa ujenzi wa soko hilo lililopo eneo la kitovu cha mji Kibaha (CBD) karibu na stendi ya mabasi ya mkoani ulianza kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 2018 na 2019 na limekamilika katika bajeti ya mwaka 2023/ 2024 .
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa wa pili kutoka kulia,akikata keki katika sherehe za uzinduzi wa Soko kubwa la Kisasa lililojengwa kwa gharama ya Sh.zaidi ya bilioni 8.hafla ambayo imefanyika Desemba 7, 2024Amesema kuwa soko hilo limejengwa chini ya mkandarasi Elerai Construction Co .Ltd gharama ya Sh.bilioni 8 huku mhandisi mshauri akilipwa zaidi ya Tsh. Milioni 352 na kufanya jumla ya gharama kufikia zaidi ya Bilioni 8.3.
Shemwelekwa amesema kuwa fedha za ujenzi wa soko hilo zimetoka Serikali Kuu,Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo (UNCDF), na mapato ya ndani ya Hlhalmashauri .
Amesema halmashauri imekuwa ikipata fedha hizo kupitia bajeti ya Halmashauri ya kila mwaka ambapo mpaka sasa zaidi ya Sh.bilioni 7.3zimelipwa kwa mkandarasi Elerai sawa na asilimia 91.5 na Tsh Milioni 308.6 zimelipwa kwa mkandarasi mshauri.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimoni wa kwanza Kulia akikata utepe kuzindua Soko kubwa la Kisasa la Halmashauri ya Mji Kibaha (Kibaha Shopping Mall) hafla iliyofanyika Desemba 7,2024Mkurugenzi huyo amesema soko hilo linahuduma mbalimbali za kibiashara ambazo zimegawanyika katika mfumo wa aina tofauti kulingana na ukubwa wa huduma inayotolewa yakiwemo maduka, Super Market, kumbi za benki,ATM,eneo la kuchezea watoto, maeneo ya chakula,kutazama michezo na kumbi za mikutano.
Amesema huduma nyingine ni pamoja na kuwepo maeneo ya maegesho ya pikipiki 50,Taxi 10, magari 100 na bajaji 30.
Baadhi ya Wananchi walioshiriki uzinduzi wa Soko kubwa la Kisasa la biashara lililojengwa katika Halmashauri ya Mji Kibaha eneo la stendi Kuu ya mabasi iliyopo Mjini Kibaha , uzinduzi huo umefanyika Desemba 7,2024 Mjini Kibaha."Mradi huu unamanufaa makubwa kwani utaiwezesha halmashauri kuendelea kuongeza kiwango cha ukusanyaji mapato ya ndani zaidi ya milioni 660 kwa mwaka fedha ambazo zitasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa halmashauri ikiwa ni ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya,"amesema Dkt.Shemwelekwa
Aidha ,pamoja na mambo mengine lakini pia mradi wa soko hilo unakwenda kutoa ajira zaidi ya 120 kwa wakazi wa mji wa Kibaha na maeneo jirani ambapo ajira hizo zitatoka katika usimamizi wa maduka,usafi na usalama.
Shemwelekwa ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha anatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo mkubwa wa kimkakati ndani ya halmashauri ya mji Kibaha.
Post a Comment