HEADER AD

HEADER AD

WAFANYAKAZI TANROADS PWANI WAADHIMISHA SIKU YA UHURU KWA KUFANYA USAFI HOSPITALI YA TUMBI


Na Gustaphu Haule, Pwani

WAFANYAKAZI wa ofisi ya Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani (TANROADS) wameadhimisha miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania kwa kufanya usafi katika maeneo ya Hospitali ya Rufaa Tumbi iliyopo Kibaha mjini .

Wafanyakazi hao wakiongozwa na Meneja wa mkoa wa Pwani, Baraka Mwambage wakiwa hospitalini hapo wamefanya usafi wa kufyeka vichaka vya majani yaliyozunguka majengo ya hospitali hiyo pamoja na kupanda miti katika maeneo mbalimbali.

           Meneja TANROADS Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage akishiriki kufanya usafi katika maeneo ya Hospitali Teule ya Rufaa Tumbi iliyopo Kibaha Mjini ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Pwani Baraka Mwambage akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo amesema kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa ulitoka na maazimio ya kufanya usafi katika eneo hilo.

Mwambage amesema kuwa utekelezaji wa shughuli hiyo ni kuunga mkono maelekezo ya Serikali kuwa sherehe za Uhuru wa Tanzania zinazofanyika siku ya Uhuru 9, Disemba zifanyike kwa utaratibu wa kijamii na ndio maana Mkoa wa Pwani umejikita katika kufanya usafi wa mazingira ya hospitali ya Tumbi.

      Wafanyakazi TANROADS Mkoa wa Pwani wakiwa katika Siku ya maadhimisho ya miaka 63  ya Uhuru wa Tanzania ambapo wametumia siku hiyo kufanya katika maeneo ya Hospitali Teule ya Rufaa Tumbi iliyopo Kibaha Mkoani Pwani.

Mwambage amesema kuwa TANROADS mkoa wa Pwani imekuwa na utaratibu  wa kila mwaka ambapo yanapokaribia maadhimisho hayo huwa inatenga Juma nzima kwa ajili ya kufanya shughuli zinazogusa jamii.

"Leo ni siku ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania ndio maana TANROADS imeungana na uongozi wa Mkoa wa Pwani kuja hapa Tumbi kufanya usafi na kupanda miti lakini sisi TANROADS kila mwaka kipindi cha maadhimisho haya huwa tunatenga Juma nzima  kufanya shughuli za kijamii ,"amesema Mwambage.

Kwa upande wake afisa raslimali watu wa TANROADS Mkoa wa Pwani Pamela Mchonde amesema shughuli walizozifanya katika maadhimisho hayo ni zakimazingira ambazo zinahamasisha usafi na  utunzaji wa mazingira.

        Afisa raslimali watu wa TANROADS Mkoa wa Pwani Pamela Mchonde akishiriki kupanda miti katika eneo la Hospitali Teule ya Rufaa Tumbi iliyopo Mjini Kibaha Mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania.

Mchonde amesema kutokana na umuhimu wake wananchi wanatakiwa kuendelea kufanya usafi katika maeneo yao na hata katika maeneo yote yanayogusa jamii kama vile hospitali,Shuleni  na sehemu nyingine .

"Sisi TANROADS tumeonyesha mfano kupitia maadhimisho haya ya Siku ya Uhuru wa miaka 63 ya Tanzania ,tumekuja hapa tumefanya usafi na kupanda miti hivyo tunawaomba wananchi wajenge tabia ya kusafisha na kutunza mazingira bila kusubiri wakati wa maadhimisho haya",amesema Mchonde. 

Mchonde ameongeza kuwa jamii inatakiwa kuachana na tabia ya kukata miti hivyo ili kuepukana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi inayotokana na kukata miti hivyo kwa ajili ya kuchomea mkaa na kuni.

Nae Maselina Paulo mfanyakazi wa TANROADS amefurahishwa kuungana na Wafanyakazi wenzake katika kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanzania kwa kufanya usafi katika hospitali ya Rufaa ya Tumbi huku akiwaomba wadau wengine kuiga mfano huo.

        Meneja TANROADS Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage akiwaongoza Wafanyakazi wa  ofisi yake kufanya usafi katika maeneo ya Hospitali Teule ya Rufaa Tumbi iliyopo Kibaha Mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania.

No comments