HEADER AD

HEADER AD

RC KAGERA ASHIRIKI CHAKULA NA WATOTO WENYE UHITAJI


>>Apika chakula na kula nao Ikulu ndogo

Na Alodia Dominick, Bukoba

MKUU wa mkoa wa Kagera 
Fatma Mwassa amefanya tendo la huruma kwa watoto wenye uhitaji na kuandaa chakula cha mchana katika sikukuu ya kristmas na kushiriki pamoja nao.

Mwassa amewaalika watoto kutoka katika vituo vinne vya kulelea watoto yatima,wanaoishi mazingira magumu na wenye uhitaji wanaoishi Manispaa ya Bukoba. 
      Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akigawa chakula kwaa watoto yatima, chakula ambacho amekiandaa yeye mwenyewe.


Mwassa amepika chakula na kisha kula na watoto hao zaidi ya 200 mlo wa mchana katika sikukuu ya kristmas Ikulu ndogo ya mkoa wa Kagera kwa kupika mwenyewe, kupakua, kula na kunywa na watoto hao.

Ametaja lengo la kushiriki na watoto hao kuwa ni kutaka kusherehekea nao sikukuu hiyo muhimu, ili nao wajione kuwa wanayo haki ya kufurahi na kuungana na wengine katika sikukuu kama hizo.
          Watoto wakila chakula

"Tumezoea kubeba vyakula, nyama na vinywaji kupeleka vituoni lakini mimi nimeona tendo hili la huruma nilitekeleze kwa njia hii, nimepika mwenyewe hapa Ikulu ndogo ya mkoa wa Kagera kisha kupakua, kula na kunywa na watoto hawa wenye uhitaji na yatima tumefurahi wote katika sikukuu hii" amesema Mwassa 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya Bukoba Joas Zachwa amempongeza Mwassa kwa kuandaa hafla hiyo na kushiriki na watoto hao.

Zachwa amesema mkuu huyo wa mkoa ameonyesha upendo na hekima kubwa kwani watu wamezoea kununua nyama na vyakula na kupeleka nyumbani kisha kula na watoto wao.

       Wa kwanza kutoka kushoto ni mwenyekiti wa CCM Bukoba mjini Joas Muganyizi na kulia kwake ni katibu tawala mkoa waa Kagera Stephen Ndaki.

Ameeleza kuwa, ameonyesha upendo mkubwa kwa wanakagera kwani angeamua kukaa na familia yake ila ameonyesha ni jinsi gani ana upendo wa kweli na watu, hasa hawa vijana wahitaji

 "CCM inakupongeza na kukushukuru sana maana huu ni utekelezaji wa ilani yetu pia umeonyesha tabia aliyojijengea Rais wetu Samia Suluhu Hassan ya kufanya matendo ya huruma kwa kusaidia wahitaji kama hawa"amesema Zachwa 

Pia amesema wananchi wa wilaya ya Bukoba na mkoa mzima wana imani na kazi anazofanya za kuleta maendeleo hivyo zinaonyesha taswira ya Rais Samia ya kuteua watu makini, wenye upendo na huruma kwa Watanzania.

Mwenyekiti wa jumuiya ya vijana wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kagera (UVCCM) Faris Buruhan amesema mkuu huyo wa mkoa amefanya tendo la huruma na lenye baraka ambalo limewagusa watoto ambao pia ni vijana.
 Watoto wakila chakula

Buruhan amesema tendo hilo ni la kuigwa na kila mmoja kwani limekuwa la kipekee kwa sababu haijawahi kutokea watoto hao wenye uhitaji kukaribishwa Ikulu ndogo na kupikiwa,kuhudumiwa chakula na mkuu wa mkoa na kujumuika nao.

Baadhi ya watoto waliopata mlo huo wamepongeza upendo wa dhati aliouonyesha Mwassa kwao na kumuomba aendelee kuwakumbuka pia apeleke salamu zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan. 

 Rewina Pius Paulo kutoka kituo cha kulelea watoto Nusuru yatima kata Kashai Manispaa ya Bukoba ni mmoja watoto hao ambapo amesema, wao hawakupenda kukosa wazazi bali ni mapenzi ya Mungu.

Ameshukuru kwa tendo hilo la huruma na kuchukua dakika kadhaa kuwaombea viongozi wetu kuanzia ngazi ya chini hadi taifa.

Pia ametoa shukrani kwa Rais Samia kwa huruma yake anayoonyesha kwa Watanzania wenye mahitaji mbalimbali ambapo pia ametoa shukrani kwa mkuu wa mkoa  Mwassa kwa upendo alioonyesha kwa watoto hao.




No comments