SHAIRI : PIMBI UTAJIRI WETU
PIMBI binamu wa tembo, waulizwa je wajua?
Mdogo sana kwa tembo, ni ndugu ukiwajua,
Pimbi meno kama tembo, kama hujui tambua,
Huu utajiri wetu, hifadhi za Tanzania.
Hata na meno mengine, pimbi tembo tawajua,
Maumbile kivingine, pimbi hawezi kukua,
Tembo yuko kivingine, kwa ukubwa twamjua,
Huu utajiri wetu, hifadhi za Tanzania.
Pimbi ni aina mbili, ukitaka kuwajua,
Wengine kama tumbili, kwenye miti tawajua,
Wengine zao dalili, miamba ndiko watua,
Huu utajiri wetu, hifadhi za Tanzania.
Pimbi wa kwenye miamba, huotea sana jua,
Huko ndiko wanatamba, baridi kwao mvua,
Hujificha kwenye chemba, kukikosekana jua,
Huu utajiri wetu, hifadhi za Tanzania.
Hawacheui chakula, lakini upate jua,
Chemba tatu za chakula, kama vile wacheua,
Zinameng’enya chakula, kwa wale waliokua,
Huu utajiri wetu, hifadhi za Tanzania.
Ila watoto wa pimbi, kama wataka kujua,
Hula kinyesi cha pimbi, kumeng’enya yaumua,
Matumbo si kama pimbi, hadi pale wakikua,
Huu utajiri wetu, hifadhi za Tanzania.
Pimbi hukula mimea, kama tembo wawajua,
Tafiti zaelezea, kuimba pimbi wajua,
Nyimbo zinaelezea, matukio wayajua,
Huu utajiri wetu, hifadhi za Tanzania.
Mbuga za taifa zetu, zile unazozizijua,
Pimbi utajiri wetu, ukiwataka chagua,
Mikumi ni mbuga yetu, wengi utawatambua,
Huu utajiri wetu, hifadhi za Tanzania.
Mtunzi wa Shairi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment