RC KIHONGOSI ATOA SIKU SABA KIPINDUPINDU KITOKOMEZWE SIMIYU
Na Samwel Mwanga, Simiyu
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi, ametoa maagizo madhubuti kwa wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kumaliza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ndani ya siku 7.
Lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha kipindupindu kinatokomezwa kabisa mkoani humo kwa usimamizi thabiti wa kanuni za usafi wa mazingira na afya ya jamii.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Kenan Kihongosi(aliye kati)wakati wa kikao na wataalam wa mkoa juu ya kujadili kumalizwa ugonjwa wa kipindupindu.
Agizo hilo lilitolewa Desemba, 17 mwaka huu kwenye kikao kilichofanyika mjini Bariadi katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria kwa lengo la kujadili mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Ameagiza kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayekiuka kanuni za afya na usafi wa mazingira, akisisitiza kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
Amesema kuwa viongozi wa kisiasa wanaokwamisha juhudi za kutokomeza kipindupindu ambao umechukua muda mrefu na kusababisha vifo kwa wananchi.
Sehemu ya wajumbe katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu kujadili kumaliza ugonjwa wa kipindupindu.
" Kuna baadhi ya wanasiasa mkoani hapa wamekuwa wakikwamisha mapambano ya ugonjwa wa kipindupindu jambo linalochangia kuendelea kushamiri ugonjwa huu,”
“Sitawavumilia viongozi wa namna hiyo watakaoshindwa kuwajibika katika jitihada za kulinda afya ya wananchi,”amesema.
Amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kusimamia sheria ndogo za halmashauri kwa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka kanuni za afya na usafi wa mazingira ili kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu .
“Hakuna aliye juu ya sheria, tusioneane aibu,tuwajibike kutokomeza ugonjwa huu wa kipindupindu,”amesema.
James John ni mkazi wa Mwandoya wilaya ya Meatu amesema kuwa kauli ya mkuu huyo wa mkoa imechelewa kutokana na kutowepo kwa uwazi wa mawasiliano na taarifa sahihi kutoka kwa viongozi na wataalamu wa afya.
“Ugonjwa huu ulipoingia viongozi wetu hawakuwa wazi walizificha sijui kwa manufaa gani wakisema ni ugonjwa wa kuhara na kutapika na ukisema ni kipindupindu wanakata,hivyo ni muhimu sana katika kushinda ugonjwa huu ni kuweka wazi tatizo lililopo,”amesema.
Naye Slivester Lugembe mkazi wa mjini Maswa amesema kuwa hakuna haja ya kuficha taarifa za afya ya umma, kwani usiri unaweza kusababisha madhara zaidi.
“Hali ya mlipuko wa kipindupindu katika mkoa wa Simiyu, ambapo awali iliripotiwa kama ugonjwa wa kuhara na kutapika, sasa mamlaka ya juu ya mkoa imethibitisha ni kipindupindu hivyo ni muhimu kwa mamlaka za afya kutoa taarifa sahihi kwa wakati ili wananchi wachukue tahadhari stahiki,”amesema.
Ugonjwa wa kipindupindu ni uliingia katika mkoa huo mwezi septemba mwaka 2023 baada ya mgonjwa wa kwanza kutambuliwa wilayani Meatu ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria Vibrio cholerae, na kuenea kwake kunachangiwa sana na matumizi ya maji au chakula kilichochafuliwa.
Katibu CCM mkoa wa Simiyu,Eva Degeleka(aliyesimama)akitoa maoni yake juu ya kumalizwa kwa ugonjwa wa kipindupindu.
Post a Comment