HEADER AD

HEADER AD

TCRA YAWAKUMBUSHA WAANDISHI WA HABARI KUZINGATIA SHERIA, WANAPOANDIKA HABARI ZA UCHAGUZI

Na Alodia Dominick, Bukoba

WAANDISHI wa habari mkoani Kagera wamesisitizwa kuzingatia taratibu, sheria na kanuni katika kuandika habari za uchaguzi mkuu ujao.

Hayo yamesemwa Desemba 17,2024 na Meneja kitengo cha mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) makao makuu, Mhandisi Kadaya Baluhye katika mafunzo yaliyotolewa na Mamlaka hiyo kwa waandishi wa habari na wadau wa habari mkoani Kagera.

      Aliyeshika kipaza sauti, ni Meneja kitengo cha mawasiliano TCRA makao makuu Mhandisi Kadaya Baluhye akizungumzia taratibu, kanuni na sheria katika uchaguzi mkuu ujao

"Sheria, kanuni na taratibu tuzizingatie ili zitupunguzie ushabiki katika kuandika habari za uchaguzi mkuu ujao, jukumu letu kama waandishi wa habari ni kuzisoma kanuni kila eneo, sheria ya uchaguzi wa vyama vya siasa pamoja na sheria za nchi hii" amesema Mhandisi Baluhye.

Meneja wa mamlaka ya mawasiliano TCRA Kanda ya ziwa, Mhandisi Imelda Salum amesisitiza waandishi wa habari kupenda kusoma kwani taaluma ya habari msingi wake ni kusoma.

        Meneja wa TCRA kanda ya ziwa Mhandisi Imelda Salum akizungumza na wadau pamoja na waandishi wa habari

Wakati huo huo, Mhandisi Salum amewataka waandishi wa habari, wahariri na wamiliki kutimizi wajibu wao kama ulivyo wajibu wa vyombo vya habari.

Amesema kuwa, vyombo vya habari vinatakiwa kuwafikishia usikivu wananchi katika maeneo ambayo TCRA imetoa leseni pamoja na kuwa na vipindi mchanganyiko vya habari, michezo na burudani ambavyo vina akisi utamaduni wa mtanzania na  taifa kwa ujumla.

Aidha, amewasisitiza waandishi wa mitandao ya kijamii kulinda watoto dhidi ya programu zinazokiuka haki zao pamoja na kuepuka urushwaji wa vipindi vinavyohamasisha uharifu,kamali na ramli chonganishi na kujiepusha na lugha za matusi na zenye kukashifu ambazo zinaweza  kusababisha mtafaruku.

        Waandishi wa habari na wadau waliohudhuria mafunzo

Naye mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Kagera (Kagera Press Club), Mbeki Mbeki ameshukuru TCRA kwa kukutana mara kwa mara na waandishi wa habari mkoani humo na kutoa mafunzo kwao na akawaomba kabla ya uchaguzi mkuu mwaka kesho kukutanisha waandishi wa habari pamoja na wanasiasa.

Aule Kileo kutoka kitengo cha leseni TCRA makao makuu ametambulisha mada mbili  zilizotolewa katika mafunzo hayo ambazo ni maudhi ya habari na utangazaji pamoja na maswala ya leseni.

No comments