HEADER AD

HEADER AD

TCB YATOA BAISKELI 218 KWA WAKULIMA WAWEZESHAJI MASWA

Na Samwel Mwanga, Maswa

BODI ya Pamba Tanzania (TCB) imekabidhi baiskeli 218 kwa wakulima wawezeshaji wa zao la pamba katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu ili zitumike kutembelea na kuhamasisha wakulima wa zao hilo kuongeza uzalishaji na kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.
 
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amekabidhi baiskeli hizo Desemba 16 mwaka huu, katika hafla fupi iliyofanyika katika kiwanda cha kuchambua pamba cha Kahama Oil Mill kilichopo kijiji cha Hinduki wilayani humo.

       Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(aliyepo mbele)akizungumza na Wakulima wawezeshaji wa zao la pamba wa wilaya hiyo kabla ya kuwakabidhi baiskeli.
 
Amesema kuwa mkoa wa Simiyu unazalisha zao hilo zaidi ya asilimia 50 ya pamba inayozalishwa hapa nchini lakini bado kuna dosari moja ya wakulima kuzalisha kwa tija.
 
“Wataalamu wa kilimo cha pamba wanasema hivi,wewe mkulima  mmoja ukiamua kulima  pamba kwa ajili ya ustawi wa familia yako na akili yako yote ukaielekeza kwenye kilimo hicho kwa kufuata taratibu na kanuni za kitaalamu wanasema kwa ekari moja unaweza kuzalisha kilo 800 hadi 2500,”amesema.
 
Dc Kaminyoge amesema hilo linawezekana kwani katika musimu uliopita wa kilimo waliweza kushuhudia baadhi ya wakulima wa zao hilo katika wilaya ya Meatu mkoani humo waliweza kuzalisha kilo 1500 hadi 2000 kwa ekari moja.
 
Amesema baiskeli hizo walizopata zikatumike kuhakikisha wanawafikia  kwa wakati wakulima katika maeneo yao kuwaelekeza kufuata kanuni bora za kilimo cha zao hilo ili kiweze kuongeza mavuno na kuboresha maisha ya wakulima.
 
Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wilayani humo, Ally Mabrouk amesema kuwa lengo la ugawaji wa baiskeli hizo ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa zao la pamba kwa kuwapatia usafiri rahisi, hivyo kuimarisha uwezo wa kufuatilia shughuli za kilimo kwa karibu zaidi na kuhakikisha mafunzo ya kilimo bora yanafika kwa wakulima wengi.

      Baadhi ya wakulima wawezeshaji wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge(hayupo pichani)kabla ya kuwakabidhi baiskeli zilizotolewa na Bodi ya Pamba Tanzania(TCB)

Amesema kuwa hiyo ni sehemu ya jitihada za bodi hiyo kusaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa wakulima ili waweze kuinua uchumi wao binafsi, wa wilaya na mkoa na taifa kwa ujumla.
 
“Leo tumefanya zoezi la kukabidhi baiskeli kwa wakulima wawezeshaji wa wilaya hii  ni kwenda kuwasaidia wakulima kwenye shughuli za uzalishaji wa zao pamba kuanzia kwenye uandaji wa shamba, upandaji,utunzaji wa mashamba kwa kuua wadudu wanaoshambulia zao hilo hadi uvunaji ili waweze kuzalisha kwa tija,”amesema.
 
Veronika Paul mkulima mwezeshaji kutoka katika Kata ya Jija wilayani humo amesema kuwa ataitumia baiskeli hiyo kuwatembelea wakulima katika eneo lake ili waweze kuzalisha zao hilo kwa tija kwa kufuata kanuni bora za kilimo cha zao la pamba.

      Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(kulia) akimkabidhi baiskeli, Veronika  Paul(kushoto)mkulima mwezeshaji kutoka Kata ya Jija

Lupande Nhila mkulima mwezeshaji kutoka kijiji cha Senani ameishukuru bodi ya pamba kwa kuwapatia baiskeli hiyo ambayo itamsaidia kuwafikia wakulima kwa urahisi kwani alikuwa anashindwa kuwafikia wote kwa wakati kutokana na kutokuwa na chombo cha usafiri.
 
“Hii baiskeli kwa sasa itanisaidia kuwafikia wakulima kwa wakati kwani nilikuwa natembea kwa miguu hivyo nilikuwa siwezi kuwafikia wote ila baada ya bodi ya pamba kutuwezesha kupata chombo hiki cha usafiri nitawafikia wote tena kwa wakati,”amesema.
 
Naye Malita sasa ambaye ni mkulima mwezeshaji katika kijiji cha Ipililo amesema kuwa kwa hatua ya bodi ya pamba kuwapatia baiskeli imeonyesha dhamira ya dhati ya bodi hiyo kuhakikisha inalisimamia zao hilo ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija ili kuinua uchumi wao na wilaya kwa ujumla.
 
      Baadhi ya wakulima wawezeshaji wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(hayupo pichani)kabla ya kuwakabidhi baiskeli zilizotolewa na Bodi ya Pamba Tanzania(TCB)
 

No comments