HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: ACHA KUKATA TAMAA


NDUGU sikate tamaa, hajamalizana nawe,

Na hiyo yako balaa, Mungu bado yuko nawe,

Wewe zidi kukomaaa, hujatoswa kama jiwe,

Mungu ana haja nawe, acha kukata tamaa.


Hapo hapo umekaa, tambua huko mwenyewe,

Mungu yupo amejaa, vile ana haja nawe,

Japo kama wachakaa, sikate tamaa wewe,

Mungu ana haja nawe, acha kukata tamaa.


Maisha yamefubaa, unakula na nguruwe,

Moyoni unashangaa, uchomwavyo changarawe,

Usije kata tamaa, hajamalizana nawe,

Mungu ana haja nawe, acha kukata tamaa.


Mbatizaji likaa, kifunge kile mwenyewe,

Akawa anashangaa, kama ni Yesu mwenyewe,

Kikazi alichakaa, akajifia mwenyewe,

Mungu ana haja nawe, acha kukata tamaa.


Ya Yohana yakikaa, kwenye kichwa chako wewe,

Utatambua ahaa, Mungu hajamalizana nawe,

La sivyo angekutwaa, mwili usiwe na wewe,

Mungu ana haja nawe, acha kukata tamaa.


Usikae unachakaa, hebu changamka wewe,

Simama acha kukaa, ng’ang’ana ufanikiwe,

Nyota yako inang’aa, ni muda uinuliwe,

Mungu ana haja nawe, acha kukata tamaa.


Umepigika balaa, kuteseka kote wewe,

Lakini hajakutwaa, bado wala njugumawe,

Wewe ni wa manufaa, hajamalizana nawe,

Mungu ana haja nawe, acha kukata tamaa.


Shairi hili limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments