HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: HAKUNAGA KUCHELEWA


CHOCHOTE kikutokee, katika yako maisha,

Kikitaka upotee, kama vile umeisha,

Sitake uteketee, hali unayo maisha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Ngojea nikuchochee, uweze jichangamsha,

Usibaki ulegee, pale walipokuosha,

Inuka ujitetee, ikibidi kwa kukesha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Kitaka uendelee, katika haya maisha,

Mtu na asitokee, atake kukukwamisha,

Eti akuongelee, kwamba muda umekwisha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Mistari itokee, ambayo yatufundisha,

Ngoja niielezee, niweze kufahamisha,

Na wewe uendelee, usije kujiangusha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Dinari uipokee, unavyojishughulisha,

Muda ni wako pekee, ukitaka lianzisha,

Acha wakuongelee, wao wajichelewesha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Ngoja nimuongelee, shamba alolianzisha,

Wakulima apokee, aweze kuwalimisha,

Asubuhi watokee, wajipatie maisha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Mchana watokezee, aende kuwalimisha,

Jioni wasichezee, kujipatia maisha,

Wote hao wapokee, mshahara wa maisha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Elimu uipokee, usitake jikwamisha,

Mbele wewe utokee, mradi kuuanzisha,

Na wala asitokee, nyuma wa kukurudisha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Njia yako ya pekee, ambayo itakuvusha,

Na mbele uendelee, ufanye ya kuridhisha,

Mwenyewe ujitetee, mbali utajifikisha,

Hakunaga kuchelewa, kitaka kuanza tena.


Shairi hili limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments