SHAIRI : KIKULACHO KI NGUONI
MBU wa ndani ya neti, huyo wa kumwangamiza,
Usijempa tiketi, aweze kukuumiza,
Wewe ulokuwa fiti, apate kukulegeza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Wa nje abaki nje, hata akikuchokoza,
Hawezi kugusa punje, ndani umejituliza,
Akitaka akuonje, neti itamkimbiza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Ninarudia rudia, mfano wajieleza,
Indira Gandhi sikia, wale walimuumiza,
Ni walinzi nakwambia, ndiyo walimmaliza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Yule Thomas Sankara, kumtaja yaumiza,
Yule aliyemchora, hata kumteketeza,
Jirani yule hasara, ni kama kujimaliza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Una mpenzi nyumbani, yote unamueleza,
Yeye aenda uani, yote anayasambaza,
Huo mkuki moyoni, jinsi unavyoumiza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Kumtambua adui, vigumu nakueleza,
Sio kondoo ni chui, ndivyo ajibaraguza,
Ahakikishe hujui, jinsi anakumaliza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Ona hata Bwana Yesu, yule aliyemuuza,
Ni yule alimhusu, hata Neno kueneza,
Rushwa akairuhusu, Yesu kumuangamiza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Hakuna pa kukwepea, ndivyo ninakueleza,
Kama yakikutokea, na moyo yakaumiza,
Walikwisha elezea, kikulacho chaumiza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Unayoweza kuficha, mtu usijemweleza,
Hadi kutakapokucha, yenyewe kujitokeza,
Kama hutafichaficha, unaweza jiumiza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Hadhara iwe hadhara, siri isijetokeza,
Ukayapata madhara, ushindwe kujieleza,
Yatakayotoka bora, yawe yasiyoumiza,
Kikulacho ki nguoni, hicho ni hatari sana.
Shairi hili limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment