SHAIRI : KESHO HUYO NI MKWEO
Mtoto wa mtu wako, kumfunda kitabia,
Kama ufanyavyo wako, nakumsisitizia,
Na wa mwenzio ni wako, vema kumsaidia,
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Usemi huu mbaya, ambao tunausikia,
Wazee wasio haya, vile utawasikia,
Waongoza kwa ubaya, watoto kuwafanyia,
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Eti mtoto wa mwenzio, vile unamwangalia
Eti mkubwa mwenzio, waweza jichukulia,
Kuenenda hivyo sio, wazazi ninawambia,
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Kama wewe ulifundwa, hadi hapo wafikia,
Kwanini wewe kushindwa, kufunza nzuri tabia?
Hujui hao wawindwa, ili waweze ishia?
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Kuna mambo maadili, ambayo nafikiria,
Kwa watoto ni halali, wapate kujifunzia,
Popote pale ni mali, pasipo kuwaachia,
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Kama kusema asante, sote tunakujulia,
Endapo kitu apate, afaa kuitumia,
Hilo funzo lisipite, ili aweze tumia,
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Wewe unampa kitu, naye ajichukulia,
Unaona siyo kitu, vizuri wajisikia,
Hivi wewe una utu, au umeshaishia?
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Mengi yanasemwasemwa, mebadilika dunia,
Mtoto mtu kusemwa, shida itakuzukia,
Wewe bila ya kusemwa, hapo ungepafikia?
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Kafurahisha mzazi, kulea anajulia,
Asante ni kama kazi, watoto wanamwambia,
Na ya kwake matumizi, mengine yanavutia,
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Mempa kitu mtoto, asante inafwatia,
Mpe adhabu mtoto, asante inakujia,
Ni wazi siyo mateto, nidhamu inaingia,
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Vile tulivyolelewa, na hapa tukafikia,
Na sisi tunatakiwa, watoto kuwafikia,
Na tusipofanikiwa, kizazi kinaishia,
Kesho huyo ni mkweo, ni faida kwa mwanao.
Mtunzi wa Shairi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment