SHAIRI : FUNDI CHUMA
ANAITWA Fundi Chuma, ndege anayesifika,
Nyumba yake kama hema, kubwa kuliko Afrika,
Ndege huyu huchagama, ujenzi akiushika,
Huyu ndiye Fundi chuma, jina lingine Msingwe.
Watafiti wanasema, kiota kukamilika,
Kwa uzito kama gema, kwa ukubwa utachoka,
Kilo hamsini soma, uzito kikamilika,
Huyu ndiye Fundi Chuma, jina lingine Msingwe.
Msingwe yule mzima, uzito wake tacheka,
Nusu kilo Fundi Chuma, uzito akizeeka,
Nyumba yake Fundi Chuma, ni nzito kubwa hakika,
Huyu ndiye fundi chuma, jina lingine Msingwe.
Kiota kinasimama, vitu vingi vyahusika,
Udongo vijiti hima, kukijenga vyatumika,
Mdogo akiwa wima, kwa ujenzi asifika,
Huyu ndiye Fundi Chuma, jina lingine Msingwe.
Kwa ujenzi kama mama, kiota kinatumika,
Bata maji na wanyama, wakiwema hata nyoka,
Hutumia kwa salama, malazi wakiyataka,
Huyu ndiye Fundi Chuma, jina lingine Msingwe.
Bundi kwa Msingwe noma, anavyowambia toka!
Na ndege wakubwa pima, kiota wakikitaka,
Hana noma Fundi Chuma, pengine anakisimika,
Huyu ndiye Fundi Chuma, jina lingine Msingwe.
Kifukuzwa Fundi Chuma, wengine wafurahika,
Yawa makao salama, kuingia na kutoka,
Msingwe hashiki tama, kujenga awajibika,
Huyu ndiye Fundi Chuma, jina lingine Msingwe.
Kwenye maji Fundi Chuma, ndiko anafaidika,
Apata chakula chema, na samaki wahusika,
Ujenzi wa Fundi Chuma, uzazi unahusika,
Huyu ndiye Fundi Chuma, jina lingine Msingwe.
Wewe usishike tama, huyu ndege kimtaka,
Hapa nchi wasema, kwa Msingwe yanemeka,
Kwenye mbuga anavuma, tembelea changamka,
Huyu ndiye Fundi Chuma, jina lingine Msingwe.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment