SHAIRI : SALAMU ZA MWAKA MPYA
NIANZE na shukrani, kwa Mola wetu Karima
Kututia uzimani, kwa pumzi yake kuhema
Mwaka umetamatani, nasi bado tuwazima
Salamu za mwaka mpya, nawasalimu wapendwa
Nasalimu visiwani, bara siwaachi nyuma
Nawasalimu wandani, marijali wakuhema
Binda ninazisaini, zifike kwenu mapema
Salamu za mwaka mpya, nawasalimu wapendwa
Ni mapito duniani, wengine wameihama
Anatupenda Manani, pumzi haijasimama
Sisi tumlipe nini, ibada zije simama
Salamu za mwaka mpya, nawasalimu wapendwa
Changamoto mitihani, twashukuru kwa uzima
Ni mapito duniani, mwanadamu uwe mwema
Ukipata hamsini, uushukuru uzima
Salamu za mwaka mpya, nawasalimu wapendwa
Tupendane duniani,tusipeane lawama
Akikujia jirani,kwa jambo lime mkwama
Msaada ndio dini,sio kumpa kilema
Salamu za mwaka mpya, nawasalimu wapendwa
Tuombe ishilini tano, uwe mwaka wa neema
Tuzidishe mapambano, kazi iweze simama
Maisha yawe manono, tusiwe wenye kukwama
Salamu za mwaka mpya, nawasalimu wapendwa
Nimefika tamatini, uwe mwaka wa salama
Tumuombeni manani, tumalize kwa salama
Mabaya tusitamani, utu tukaja uzima
Salamu za mwaka mpya, nawasalimu wapendwa
Shairi limetungwa na Shomari Binda( Mvubula Vinongo) 0755487117/0672687117
Post a Comment