TAHADHARI YA BENKI KUU KWA WANAOTOBOA PESA KUZITUNDIKA KWENYE KOFIA, NGUO
>> Ni pamoja na pesa zinazotobolewa na pini kutundikwa kwenye kofia wakati wa Saro (Tohara, ukeketaji)
>>Faini ni Tsh. 500,000 kwa kila pesa moja inayoharibiwa, Kifungo mwaka mmoja au vyote pamoja
Na Dinna Maningo, Tarime
KILA inapofika mwaka unaogawanyika kwa mbili katika jamii ya kabila la Wakurya waishio mkoani Mara, ikiwemo wilaya ya Tarime, hujulikana kama ni mwaka wa kufanya ukeketaji kwa wasichana na tohara kwa wavulana.
Itambulike kwamba kitendo cha ukeketaji wasichana ni haramu, kinapigwa vita na serikali kwa sababu kinaathiri afya za wasichana na wanawake kwa ujumla, hata hivyo, kitendo hicho bado kinaendelea kufanyika katika baadhi ya sehemu.
Ukeketaji na tohara huchukuliwa na wanajamii wa kabila hilo kama ni kudumisha mila na desturi za kabila hilo la Wakurya na ni mila ambayo imekuwa ikidumishwa kizazi hadi kizazi.
Wanajamii wakicheza burudani ya litungu wakati wa sherehe za ukeketaji na tohara wilayani Tarime. Picha na mtandao
Wilayani Tarime, mwaka huu wa 2024 ni msimu wa ukeketaji na tohara, ambapo jamii ya kabila hilo hufanya maandalizi mapema ikiwemo utoaji wa kadi za mialiko za kushiriki sherehe za ukeketaji kwa wasichana na tohara kwa wavulana.
Wilaya ya Tarime ina koo 12 za jamii ya kabila la Wakurya ambazo ni Wahunyaga, Watobori, Wairege, Warenchoka, Wakira, Watimbaru, Wanyamongo, Wanyabasi, Wasweta, Wamera, Wahunyaga na Wanchari.
Kila koo hujipangia tarehe ya kuanza tohara na ukeketaji kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba, ambapo baadhi ya koo kama Wamera, Wakenye wao hutangulia mapema na koo zingine wao hufanya tukio hilo mwezi wa 12. Mwezi huo, wasichana wengi hukeketwa na wavulana kutahiriwa kwa kuwa shule zinakuwa zimefungwa na wanafunzi wanakuwa likizo.
Katika sherehe hizo wanajamii huwasindikiza vijana wao kwenda kutahiriwa na kukeketwa. Na wanaporudi nyumbani njiani hupokelewa kwa shangwe, nderemo na vifijo wakiwa njiani, huku wakicheza ngoma ya asili ya ritungu.
Wasichana waliokeketwa na wavulana waliotahiriwa vichwani mwao zinaonekana pesa zikiwa zimetundikwa juu ya kofia kwa kuunganishwa na pini huku mwilini wakiwa wamezungushiwa kanga na shuka, vichwani mwao wakiwa wamefunikwa miamvuli ili wasiweze kuungua jua au kunyeshewa mvua.
Mwalikwa hutoa zawadi yake ya pesa, khanga, au shuka. Pesa hiyo kama zawadi hutobolewa kwa pini na kisha pini zenye noti hizo zilizotobolewa kuvishwa juu ya kofia na nguo aina ya shuka, gauni, au kanga wanazovalishwa mwilini msichana aliyekeketwa na mvulana aliyetahiriwa.
Pesa zilizotundikwa kwa pini na kuvishwa juu ya nguo na kichwani kwa msichana ambaye akikeketwa. Picha na mtandao
Kitendo hicho cha kutoboa noti kwa pini na kuzitundika kwenye kofia au nguo kinapigwa marufuku na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwamba ni uharibifu wa pesa hizo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya fedha ambapo kwa kila pesa moja inayoharibiwa, mtuhumiwa anaweza kupigwa faini Tsh. laki tano au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote pamoja.
Isemavyo sheria ya fedha
Afisa Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), Omary Kitojo, anasema Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code) ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho 2022 sura ya 16, kifungu Namba 332 A, inatoa faini ya shilingi laki tano (500,000) za Kitanzania kwa kila pesa moja inayoharibiwa au kufungwa jela kwa mwaka mmoja au adhabu zote mbili kwa pamoja.
Afisa Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), Omary Kitojo akionesha namna ya utunzaji wa fedha wakati wa semina ya waandishi wa habari Kanda ya Ziwa iliyofanyika Benki kuu Tawi la Mwanza Mwezi Novemba, 2024.
Pia, anasema Sheria ya Bendera ya Taifa na Nembo (National Flag and Coat of Arms Act) ya mwaka 1971 kifungu cha namba 6 (1) inakataza matumizi ya sarafu kwa kazi nyingine isipokuwa kwa kufanyia miamala pekee.
"Hizi hela zinalindwa na sheria za nchi kwa hiyo matumizi yote ambayo yanaenda kinyume na makusudio ya kutengenezwa kwa pesa yote hayaruhusiwi kwa mujibu wa sheria," anasema Omary.
Namna bora ya utunzaji wa hela
Omary anaeleza namna ya utunzaji wa sarafu na kwamba utunzaji vibaya wa pesa unasababisha serikali iingie gharama za ziada kutengeneza pesa nyingine.
"Shika pesa kwa mikono safi, hakikisha mikono inayotumika kushika hela ni misafi na haina uchafu, mafuta, majimaji. Epuka kukunjakunja au kuandika kwenye noti. Mikunjo kwenye noti inaweza kuharibu ngozi ya karatasi na kupunguza maisha yake.
"Weka pesa katika sehemu safi na kavu. Pochi au mikoba iliyo na sehemu maalumu za fedha husaidia kuzilinda. Epuka kuhifadhi hela katika sehemu ambazo zinaweza kuharibika kwa urahisi, kama vile mifuko ambayo inaweza kupondwa au kunyeshewa," anasema afisa huyo.
Omary anaongeza kusema, "usiunganishe noti pamoja kwa kutumia pini zinaweza kusababisha hela kuharibika na kuchakaa mapema. Punguza kukunja noti. Kukunja noti kupita kiasi kunadhoofisha karatasi na kuweza kusababisha kukatika," anasema Omary.
Msimamizi huyo wa sarafu hakusita kuwaonya wanaotumia hela kama mapambo hususani kwenye sherehe za jando au wanaorusha hela chini wakati wa harusi au harambee kuacha tabia hiyo.
" Kuna wale wanaotoka jando wanaweka noti kama mapambo, wapo wanaorusha hela zinaanguka chini, au wanaweka chini. Hizo sio njia halali za matumizi na utunzaji wa hela. Tumetoa elimu kwa baadhi ya maDJ, washereheshaji na viongozi wa dini. Ukimwelimisha mmoja nae ataelimisha wengi," anasema Omary.
Anaeleza kuwa kwa mujibu wa utafiti wa Benki kuu ya Tanzania, pesa zote zinazotengenezwa zina muda wake wa kuisha kama zikitumika vizuri. Kwa mfano, kwa kawaida noti za TZS .5,000 na 10,000 , inaweza kuishi kwa wastani wa miezi 18 hadi 24, wakati Tsh. 1000, inaishi kwa wastani wa miezi 12 hadi 15.
'" Utakapoitumia vibaya pesa unatulazimisha tuingie gharama ya ziada ya kutengeneza pesa nyingine kabla ya muda wa kutengeneza haujafika. Pesa zinatumika kutengeneza pesa bajeti ambayo ilitakiwa itumike kwenye mambo mengine kama afya, elimu itatumika kutengeneza pesa.
" Hizi pesa kituo cha mwisho ni Benki Kuu. Zitatumika wee lakini mwisho wa siku zitafika benki, benki zitazileta BoT; zikifika BoT kuna mchakato. Zikifika kwenye mashine zikiwa na alama zozote zile mashine zinatambua na kuzisaga kwa sababu ni chafu haziwezi kurudi tena kwenye mzunguko, " amesema Omary.
Afisa huyo anasema ni muhimu wananchi kutunza hela kwasababu serikali kupitia Benki kuu inatumia gharama kubwa kuzitengeneza na kwamba fedha ni tunu na nembo ya Taifa ambayo kisheria inakataza kutumia kwa matumizi mengineyo isipokuwa yale yaliyokusudiwa.
" Kuharibu hela ni kufanya matumizi tofauti na ilivyokusudiwa, mikunjo ya noti inaweza kuharibu nyuzi za kwenye noti na kupunguza maisha yake. Ukiitunza vibaya na yule akatunza vibaya kila anayeipokea akaitunza vibaya, haitadumu;
"Lakini ikitunzwa kwenye pochi ikiwa imenyooka na mwingine anayeipokea akaitunza hivyo hivyo itadumu muda mrefu. Tunza pesa ikiwa imenyooka hiyo ndio njia salama ya kutunza pesa," anasema.
Msimamizi huyo wa sarafu anawaomba waandishi wa habari nchini kupitia kalamu zao wasaidie kutoa elimu kuwaelimisha wananchi utunzaji wa fedha ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Mwanza, Benki inayohudumia mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, Gloria Mwaikambo, anawaonya wananchi wanaotumia pesa kama urembo kwamba anayebainika kuharibu pesa huchukuliwa hatua za kisheria.
"Kwa wale wanaoharibu pesa wakibainika huwa wanachukuliwa hatua. Kuna mwingine Musoma alikuwa ametoka jandoni kavalishwa pesa kichwani hadi nguoni tulifuatilia na hatua zikachukuliwa dhidi yak. Wapo pia wengine wanatengeneza pesa kama mapambo ya maua.
"Tushatoa elimu kwa baadhi ya washehereshaji na tunaendelea kutoa elimu maana huko kwenye sherehe unakuta watu wanarusha pesa, zinatupwa chini wanaona kama ni fahari hawajui kama ni makosa, baada ya kuwapa elimu wameanza kuelewa sasa hivi wanaweka pesa kwenye vyombo kama vikapu," anasema Gloria.
Je wananchi wakiwemo Wazee wa mila wilayani Tarime wanasema nini juu ya utunzaji wa hela ikiwemo uharibifu wa hela kwa kuzitoboa na pini na kuwavalisha vichwani kwenye kofia wasichana waliokeketwa na wavulana waliotahiriwa?
........Itaendelea
Post a Comment