HEADER AD

HEADER AD

TARIME WAIOMBA BoT KUWAPA ELIMU YA UTUNZAJI WA PESA

>>Wasema ukosefu wa elimu umesababisha jamii kuendelea kutoboa pesa na kutundika kwenye kofia wakati wa Saro (Tohara, ukeketaji)

Na Dinna Maningo, Tarime

BENKI Kuu ya Tanzania, imekuwa ikitoa elimu ya utunzaji wa pesa, lengo likiwa ni kuziwezesha pesa kudumu kwa muda mrefu, lakini kuwaelekeza watu kuzitunza ili wasijekumbwa na adhabu kwa wale wanaobainika kuharibu pesa.

Katika chombo hiki cha habari, Desemba 5, 2024, imechapishwa makala yenye kichwa cha habari ' 'TAHADHARI YA BENKI KUU KWA WANAOTOBOA PESA KUZITUNDIKA KWENYE KOFIA, NGUO'.

        Benki kuu ya Tanzania

Makala hiyo imeeleza namna bora ya utunzaji wa pesa, sheria na adhabu kwa mtu ambaye ataharibu hela ikiwemo faini ya 500,000 kwa kila pesa moja iliyoharibiwa na kifungo cha mwaka mmoja jela.

Je, wananchi wakiwemo wazee wa mila wilayani Tarime wanasema nini juu ya utunzaji wa hela ikiwemo uharibifu kwa kuzitoboa na pini na kuwavalisha vichwani juu ya kofia wasichana waliokeketwa na wavulana waliotahiriwa?

Wasemavyo wananchi

Mwandishi wa DIMA Online amezungumza na wananchi, baadhi wanaiomba Benki Kuu ya Tanzania kufika Tarime kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa fedha, na Wazee wa mila nao wanasema Benki Kuu ikiwapa elimu wao ni rahisi kuielimisha jamii kupitia koo zao za jamii ya kabila la Wakurya.

Pendo Munata mkazi wa Nyamongo anasema, "Binafsi sijawahi kupata elimu ya utunzaji wa pesa, sikuwa nafahamu kwamba ukitoboa pesa kwa pini ni makosa au ukimvalisha pesa kichwani au kwenye nguo kijana au msichana ni kosa.

    Pendo Munata mkazi wa Nyamongo

"Mi nachokifahamu binti akikeketwa au mvulana akitahiriwa lazima pesa anayopewa kama zawadi awekewe kwenye kofia kichwani, zikiwa nyingi zinatundikwa kwenye nguo.

" Jambo hili ni mila na utamaduni wa Mkurya.  Pesa hizo hutumiwa na msamba tu yaani kijana aliyetahiriwa na msichana aliyekeketwa kwa matumizi yake haziguswi na mtu mwingine.

"Pesa ya msamba haina mibaraka na haitumiki kwa kufanyia biashara, msamba anaitumia kwa matumizi ya kuvaa na kula basi. Tunaomba Benki Kuu ije Tarime itupatie elimu zaidi. Waandishi wa habari wana nafasi yao kutuelimisha na vilevile Benki ina nafasi yake kuelimisha wananchi," anasema Pendo.

Ghati Chacha mkazi wa Rebu senta anasema uvaaji wa pesa kichwani kwa mvulana na msichana ni mila na desturi lakini jamii inaweza kuelimishwa badala ya kuweka pesa kwenye kofia na nguo ziwekwe kwenye pochi ama mkoba.

          Pesa zilizotungikwa kwa pini na kuiningi'nizwa kwenye kofia na nguo 

"Mi nadhani wanafanya hivyo kwa sababu hawana elimu ya utunzaji wa pesa. Wanajamii wakielimishwa madhara yake kisheria na uwajibishwaji ukawepo wataacha. Wanafanya hivyo kama kudumisha mila ila sidhani kwamba wasipofanya hivyo itawaathiri ni vile hawana elimu ya utunzaji wa pesa," anasema Ghati.

Mwita Matiko mkazi wa Kijiji cha Matongo anasema: "Watu wanafanya makosa kwa sababu wengi hawakusoma na hawajui sheria. Mimi naomba Benki Kuu ianze kutoa elimu kwa wazee wa mila. Kila koo ya jamii ya Wakurya ina wazee wa mila na hawa ndio wanaopanga taratibu zote za kimila ukiwemo ukeketaji na tohara, ndio wanaotangaza tarehe za tohara na ukeketaji.

"Hawa Wazee wa mila wakielimishwa kuhusu utunzaji wa hela na adhabu yake kwa anayekiuka, basi watawazuia wanajamii; maana hawa wanasikilizwa sana na jamii kuliko hata polisi au mahakama, kwa sababu nao wana sheria zao kwa mwanajamii yeyote akienda kinyume na taratibu zao na wanawaadhibu kimila hivyo wanaogopwa sana kwenye jamii," anasema Mwita.

Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Kata ya Nyarokoba, anasema katika koo yao ya Wairege, kwa sasa, vijana wao hawaweki pesa kwenye kofia, pesa huwekwa kwenye pochi au mkoba. 

"Zamani mvulana akitoka kutahiriwa kwenye kibhaga (jandoni) au msichana akikeketwa wakiwa njiani walitunukiwa zawadi ya pesa au khanga ama shuka. Kama ni pesa unakuta kavaa kofia wanachukua pesa wanaitoboa kwa pini inakuwa kwenye ile pini kisha inatundikwa juu ya kofia, zikijaa kichwani zinawekwa kwenye nguo aliyoivaa, walifanya hivyo kama urembo na kama zawadi.

Anasema koo ya Wairege wameshaacha huo utamaduni na kwamba kwa sasa kijana akitoka kutahiriwa au binti akitoka kukeketwa hawekewi pesa kwenye kofia, isipokuwa yule aliyetengwa kwa ajili ya kumshika kichwa wakati msichana akikeketwa au mvulana akitahiriwa ndiye anayebeba mkoba wa nguo na pesa.

           Jamii ya kabila ya wakurya wilayani Tarime wakiwa katika burudani ya asili

"Wamefanya hivyo baada ya kuona vijana na wasichana wanarogwa, mtu anaona mtoto wa fulani kapewa pesa nyingi kuliko wake wanamchezea anapoteza maisha. Hii imesaidia sana maana kijana alipomuona mwenzake ana pesa nyingi yeye hajapewa pesa nyingi alisononeka sana," anasema Bhoke.

Wazee wa mila waomba kupewa elimu

Kama tujuavyo Wazee wa mila katika koo 12 za jamii ya kabila la Wakurya wilayani Tarime ndio wasemaji wakuu ndani ya jamii na ndio watoa matamko ya kimila, na ni watu wanaosikilizwa sana na jamii. Wazee hao wa mila wanaiomba Benki kuu ya Tanzania kuwapa elimu ya utunzaji wa hela

Mzee wa mila ambaye ni mwenyekiti wa koo 12 za jamii ya kabila la Wakurya wilayani Tarime, Mwikwabe Makabe, anayetoka koo ya Wahunyaga, mkazi wa Kijiji cha Turugeti ameiomba Benki Kuu ya Tanzania kutoa elimu ya utunzaji wa hela kwa wazee wa mila.

                 Pesa za Tanzania

"Sio lazima kuweka pesa kichwani na sio kwamba wasipoweka pesa kichwani wanakuwa wamefanya makosa, isipokuwa wanafanya hivyo kwa kuwa walikuta watu wanafanya hivyo nao wanadumisha mila hiyo. Wanaweka tu hela kichwani ili zionekane wazi kuwa wamezawadiwa ni kama urembo. 

"Ila wakipata elimu ya utunzaji wa pesa wataacha na wote watakuwa wakiweka kwenye mikoba au waleti, bado itakaa kwa usalama, akiwa na wasiwasi atanunua mkoba wenye mkanda mrefu halafu atavishwa begani kwake au shingoni, pesa zake atakaa nazo mwenyewe hivyo haziwezi kuibiwa.

"Tukipata elimu vizuri kutoka kwa wahusika wa Benki Kuu nasi tutawaelimisha watu kwa msichana aliyekeketwa au mvulana aliyetahiriwa hakuna kutoboa pesa kuweka kwenye kofia bali kila mtu azipokee na kuzitunza kwenye mkoba wake aliovalishwa begani kwake.

Boniface Meremo ni Katibu wa Wazee wa Mila koo 12 za jamii ya Wakurya wilayani Tarime mkazi wa Kijiji cha Nyamirambaro, kata ya Komaswa anasema wazee wa mila wakielimishwa watasaidia sana kuielimisha jamii ya Wakurya kuachana na mila ya kutoboa pesa kwa pini na kuiningi'niza kwenye kofia.

        Boniface Meremo ni Katibu wa Wazee wa Mila koo 12 za jamii ya Wakurya wilayani Tarime mkazi wa Kijiji cha Nyamirambaro, kata ya Komaswa

"Zile huwa ni zawaidi anapokuwa amekeketwa au ametahiriwa na akawa hajalia hupewa pesa kama zawadi akichukuliwa kama shujaa, pia akiwa na ukoo mkubwa hupewa pesa nyingi kiasi cha kulazimika kuzining'iniza kwenye nguo aliyovaa.

"Tulikuta wanaweka pesa vichwani na sisi tukafuata hivyo hivyo. Tangu nizaliwe hadi nimezeeka hatujawahi kufundishwa kwamba ukitoboa hela na pini ni kosa. Tunaomba Benki Kuu itupe elimu sisi wazee wa mila na mangariba, watu wapewe semina ya utunzaji wa fedha nasi tutaelimisha wengine," anasema Boniface.

Itambulike kwamba kitendo cha ukeketaji wasichana ni haramu, kinapigwa vita na serikali kwa sababu kinaathiri afya za wasichana na wanawake kwa ujumla, hata hivyo, kitendo hicho bado kinaendelea kufanyika katika baadhi ya sehemu.

Benki Kuu ya Tanzania ilianzishwa mwaka 1966 kwa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1965. Benki Kuu ina makao makuu yake jijini Dodoma, ofisi mbili za makao makuu ndogo Dar es Salaam na Zanzibar na matawi manne yaliyoko Arusha, Mwanza, Mtwara na Mbeya. Tawi la Mwanza, lililoko Kanda ya Ziwa lilianzishwa tarehe 5 Februari 1980.

      Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) , Emmanuel Tutuba

Jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa taifa.

Kazi nyingine za Benki Kuu ya Tanzania ni kutoa sarafu ya nchi ambayo ni Shilingi ya Tanzania, kusimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha, kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo nchini, kuhifadhi akiba ya nchi ikiwemo fedha za kigeni.

Ni Benki ya Serikali, ni Benki ya Mabenki; na inatoa ushauri juu ya masuala ya uchumi na fedha kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Afisa Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), Omary Kitojo anasema sheria ya kanuni ya adhabu (penal code) ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho 2022 sura ya 16 kifungu Namba 332 A, inatoa faini ya shilingi laki tano (500,000) kwa kila pesa moja inayoharibiwa au kufungwa jela kwa mwaka mmoja au adhabu zote mbili.

     Afisa Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), Omary Kitojo.

Pia anasema Sheria ya Bendera ya Taifa na Nembo (National Flag and Coat of Arms Act) ya mwaka 1971 kifungu namba 6 (1) inakataza matumizi ya sarafu kwa kazi nyingine isipokuwa kwa kufanyia miamala pekee.

"Hizi pesa zinalindwa na sheria za nchi kwa hiyo matumizi yote ambayo yanaenda kinyume na makusudio ya kutolewa kwa fedha hayaruhusiwi kwa mujibu wa sheria," anasema Omary.

Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Mwanza, linalohudumia mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, Gloria Mwaikambo anawaonya wananchi wanaotumia pesa kama urembo kwamba wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.

         Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Mwanza, linalohudumia mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, Gloria Mwaikambo.



No comments