WAZIRI MHAGAMA AWATAKA WAJAWAZITO KUJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA AFYA
Na Samwel Mwanga, Uyui
WAZIRI wa Afya, Jenister Mhagama amewataka wanawake wajawazito kwenda kujifungua katika vituo vya afya ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.
Ametoa rai hiyo Desemba, 21 mwaka huu wakati akifungua zahanati ya kijiji cha Simbodamalu pamoja na wodi ya wazazi katika zahanati ya kijiji cha Lutende wilaya ya Uyui mkoa wa Tabora.
Waziri wa Afya,Jenister Mhagama akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sibodamalu wilaya ya Uyui mara baada ya kufungua zahanati ya kijiji hicho.
Amesema kuwa serikali kwa kuonyesha dhamira ya dhati imehakikisha kuwa huduma za afya za uzazi zinapatikana kwa urahisi na kwa ubora katika vituo hivyo.
Amesema kuwa kujifungulia kwenye vituo vya afya kunapunguza hatari za kiafya zinazoweza kutokea kwa mama na mtoto wakati wa kujifungua, kwani huduma za dharura na wataalam wa afya hupatikana kwa haraka.
“Mama mjamzito unapokwenda kujifungulia kwenye kituo cha afya unapunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kiafya ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa kujifungua pale hata inapotokea huduma ya dharula utapata kutokana na kuwepo kwa wataalam wa afya,”amesema.
Amesema kuwa pia serikali imekuwa ikihamasisha kwa jamii na wadau mbalimbali wa maendeleo hususani katika sekta ya afya kuboresha miundombinu ya afya maeneo ya vijijini na mijini ili kuongeza upatikanaji wa huduma hizo.
“Leo tumefungua hapa zahanati katika kijiji hiki ni hitaji muhimu sana kwa wananchi wa eneo hili ambao walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya, katika kukamilisha tumeshirikiana na wadau wetu wa maendeleo shirika la world vision kupitia mradi wa maendeleo Lutende,”amesema.
Leah Malale ni mkazi wa kijiji cha Simbodamalu amesema kuwepo kwa zahanati hiyo kutawasaidia hasa wakina mama wajawazito ambao walikuwa wakifuata huduma ya kiliniki katika zahanati ya Lutende umbali wa kilomita 14.
“Tulikuwa tukitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika zahanati iliyoko katika kijiji cha Lutende na wakati mwingine inakubidi utembee umbali wa kilomita 40 kwenda katika kituo cha afya cha Ndala kupata huduma za afya,”amesema.
Naye Uholo Said mkazi wa kijiji hicho amesema kuwa changamoto kubwa waliyokuwa wakiipata ni huduma za afya za mama na mtoto na kuwalazimu wengine kujifungulia majumbani hali ambayo si salama kwa afya ya mama na mtoto.
Bi Uholo Said mkazi wa kijiji cha Simbodamalu wilaya ya Uyui akielezea adha walizokuwa wakipata kabla ya ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho.
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Uyui, Masanja Manani akisoma taarifa mbele ya Waziri Mhagama amesema juu ya ujenzi huo amesema kuwa zahanati hiyo inategemea kuwahudumia wananchi wapatao 12,000 na hadi kukamilika kwake jumla ya Tsh. Milioni 357 zimetumika huku shirika la World Vision likichangia kiasi cha Tsh Milioni 334.
Amesema kuwa kuwa wilaya hiyo imefanikiwa kuimarisha huduma ya akina mama wajawazito katika kliniki chini ya wiki 120, yameongezeka kutoka asilimia 33 kwa mwaka 2023 hadi asilimia 40 kwa mwaka huu.
“Hii ni hatua muhimu katika kuboresha viwango vya afya ya uzazi na kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga katika wilaya yetu,”amesema Masanja.
Post a Comment