BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA MWANASHERIA MKUU WAKUTANA KUJADILI UTENDAJI KAZI
>>Katibu mkuu Maswi atia neno
Na Gustaphu Haule, Pwani
BARAZA la Wafanyakazi la ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali limekutana katika kikao chake cha kwanza kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yatakayosaidia kurahisisha utendaji kazi na kutoa huduma za kisheria kwa wananchi.
Kikao hicho kimefanyika Januari 24, 2025 katika Chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa Mkoa wa Pwani kwa kuwashirikisha wajumbe mbalimbali wakiwemo wakuu wa vitengo,wakurugenzi wasaidizi ,wakuu wa divisheni,mawakili wa Serikali na wajumbe wa Tughe.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Hamza Johari, amesema kuwa lengo la kukutana katika kikao hicho ni kufanya tathmini ya namna ambavyo utendaji kazi wao ulivyokuwa katika kipindi cha mwaka uliopita na namna wakatavyoendelea mwaka 2025.
Johari amesema kuwa ni wazi kuwa mwaka uliopita wamefanya vizuri katika eneo la sheria ikiwemo kuweka kliniki za Sheria ambazo zimetolewa bure kwa wananchi ambapo lengo lake ni kusogeza huduma za kisheria karibu na Wananchi.
Amesema kuwa kwasasa huduma hiyo inaendelea kufanyika katika Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba kazi hiyo ni mpango wa ofisi ya AG ambayo itaendelea kuwekewa mkazo juu ya huduma ya Sheria kwa wananchi pamoja na huduma nyingine za masuala ya kisheria.
"Mbali na kliniki za kisheria lakini ofisi ya AG inafanyakazi ya kupitia mikataba inayoletwa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha na kutoa ushauri wa kisheria kazi ambayo imefanyika kuanzia Julai hadi Disemba mwaka 2024."amesema Johari.
Johari ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kazi hiyo imekuwa ikifanyika vizuri na pale ambapo panahitajika kutoa maoni yao wamekuwa wakifanya hivyo kwa maslahi ya Taifa.
Aidha Johari amesema ofisi ya AG pia imekuwa ikifanyakazi ya kuhakikisha mawakili na wanasheria wao wanaendelea kuwa vizuri na uwezo wa kutoa huduma za kisheria hapa Nchini.
Kutokana na hali hiyo kikao hicho kimeangalia namna ya kuwawezesha mawakili na wanasheria hao kwa kuwapa mafunzo mbalimbali licha ya kuwa zipo baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo uhaba wa fedha.
"Lengo la mkutano huu pia ni kuangalia changamoto zao na kuzipatia majibu hasa katika suala la mafunzo stahiki ambayo yanahitaji fedha na sisi tutaangalia na kuweka Mkakati wa namna gani ili tuweze kutoa mafunzo Kwa wanasheria na mawakili,"amesema Johari
Amesema pamoja na mambo mengine lakini kikao hicho kimeangalia namna ya kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari ( TEHAMA)katika kuboresha hutoaji huduma za kisheria ili kuweza kuendana na wakati pamoja na kuleta urahisi katika kuwafikia Watanzania .
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi, ameipongeza ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanya kazi zao vizuri sambamba na kuona umuhimu wa kuitisha Baraza hilo.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi watatu kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Baraza la ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Maswi amesema kuwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kiungo muhimu kwa maendeleo ya nchi na Serikali imekuwa na imani kubwa na ofisi hiyo na kwamba Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa ofisi na watumishi wote wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu.
Amesema anatambua ofisi ya AG imekuwa na majukumu mazito sambamba na changamoto ya uchache wa raslimali lakini Wizara ya Katiba na Sheria itaona namna ya kusaidia katika utatuzi wa baadhi ya changamoto ikiwemo kuajiri Wafanyakazi na vitendeakazi.
Maswi ameiomba ofisi hiyo kuendelea kuishughulikia mikataba mbalimbali yenye maslahi kwa nchi yetu na lazima mikataba hiyo ijulikane ambapo kutokana na umuhimu wa mikataba hiyo lazima kufanyakazi kwa bidii.
Mbali na hayo amemuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kushirikiana na ofisi yake kuhakikisha wanafuatilia na kuboresha mikataba ya Serikali kwa maslahi mapana na Taifa.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Samwel Maneno akizungumza katika mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu uliofanyika katika Chuo cha uongozi wa Mwalimu Nyerere Kibaha Mkoani Pwani.
"Mikataba hii ya Serikali ni muhimu sana , kwahiyo niiombe ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuanza kutoa mafunzo kwa watumishi juu ya upekuzi wa mikataba ya Serikali ili kusudi tuweze kulinda maslahi ya Taifa na hata katika kutoa huduma za kisheria kwa wananchi," amesema Maswi.
Awali Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Samwel Maneno,amesema katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Jumla ya mikataba 1799 ilifanyiwa upekuzi ambapo kati ya hiyo mikataba 1,639 ya manunuzi,120 imehusu fedha,mkataba (1) kuhusu Maliasili na 39 ni ya ushirikiano wa kimataifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi watatu kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Baraza la ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali mara.
Post a Comment