FISI AUA MTOTO MASWA
Na Samwel Mwanga, Maswa
MTOTO mwenye umri wa miaka minne ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Ilambambasa Kata ya Senani wilayani Maswa mkoani Simiyu amefariki dunia baada ya kujeruhiwa na fisi huku sehemu ya viungo vyake vya mwili vikiwa vimeharibiwa na mnyama huyo.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo aliyefika katika kijiji hicho Januari 23 mwaka huu amesema kuwa mtoto huyo alijeruhiwa akiwa nje ya nyumba yao.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungunza na wananchi wa kijiji cha Ilambambasa kufuatia mtoto kuuawa na fisi
Amesema kuwa tukio hilo limetokea Januari 22 mwaka huu majira ya saa 1:00 jioni katika kitongoji cha Ilambambasa, mtoto Khija Ntubanga (4) alifariki baada ya kujeruhiwa na mnyama mkali fisi na baadhi ya viungo vya mwili wake kuharibiwa vibaya hasa sehemu za kichwa,
“Tukio hilo limetokea wakati akiwa nje ya nyumba huku mtoto mwenzake akiwa ameingia ndani ya jiko kwa ajili ya kuchochea moto wakati huo mama mzazi wa mtoto huyo alikuwa amekwenda kutafuta mahitaji ya nyumbani kwenye eneo la senta ya kijiji palipo na maduka,”
“Fisi huyo alitokea ghafla katika eneo la nyumba hiyo na alifanikiwa kumkamata na kumshambulia na kumjeruhi vibaya baadhi ya viungo vya mwili wa Khija Ntubanga na kumtoa ngozi ya kichwa,”amesema.
Amesema kuwa baadhi ya wananchi walimuona fisi huyo akimshambulia mtoto mita 15 kutoka katika nyumba yao ndipo walipopiga kelele ya kuomba msaada alimuachia mtoto huyo na kukimbia katika shamba na kutoweka na hadi sasa hajapatikana.
“Mara baada ya kelele za watu kuzidi kwa lengo la kuomba msaada, fisi huyo alimuachia mtoto huyo huku akiwa amejeruhiwa vibaya na alikimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Maswa na alifariki wakati akipatiwa matibabu,”amesema.
Kufuatia tukio hilo mkuu huyo wa wilaya amewaagiza askari wa wanyamapori kushirikiana na jeshi la jadi la Sungusungu kumsaka fisi huyo, usiku na mchana na akipatikana auawe kwani tayari amezua taharuki katika kijiji hicho.
Askari wa jeshi la jadi Sungusungu katika kijiji cha Ilambambasa wilaya ya Maswa wakiwa kwenye mkutano wa kuweka mkakati wa kumsaka fisi aliyeua mtoto katika kijiji hicho.
“Ninatoa wito kwa wananchi wote wa wilaya ya Maswa kuendelea kuchukua tahadhari kwa watoto pamoja na wazazi wao dhidi ya wanyama wakali kwenye maeneo yao, hasa vijijini pia kuwaepusha watoto kutembea pekee yao kwenye maeneo yasiyokuwa na makazi,”amesema.
Naye Baya Shinu ni mkazi wa kijiji cha Ilambambasa amesema kuwa msako wa kumtafuta fisi huyo uanze mara moja kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori kwa bila kufanya hivyo watashindwa kufanya kazi zikiwemo za shambani kwa kuhofia kushambuliwa na fisi.
“Baada ya tukio hili kutokea tumeanza msako wa kumtafuta huyo fisi lakini hatukumpata ila kwa sasa tukishirikiana na askari wa wanyamapori tuanze msako mara moja maana wao wana bunduki na sisi tuna silaha za jadi ili tuhakikishe anapatikana na kuuawa,”amesema.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungunza na wananchi wa kijiji cha Ilambambasa kufuatia mtoto kuuawa na fisi.
Post a Comment