CHADEMA SIMIYU YATANGAZA KUMUUNGA MKONO LISSU, HECHE
Samwel Mwanga, Simiyu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Simiyu, kimetoa tamko la kumuunga mkono Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Tundu Lissu katika azma yake ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa .
Tamko hilo limetolewa leo , Januari , 13 mwaka huu, mjini Bariadi na Katibu wa CHADEMA wa mkoa huo, Johnstone Luzubukya, likiwa na uungwaji mkono wa Mwenyekiti wa mkoa, Mussa Onesmo wakati wakiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa Smart Lodge mjini Bariadi.
Katibu wa CHADEMA mkoa wa Simiyu Johnstone Luzubukya akitoa tamko mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kumuunga mkono mgombea. Tundu Lissu na John Heche.Amesema kuwa wapiga kura wa mkoa huo wako 32 na kwa kauli moja wameamua kuwaunga mkono wagombea hao kutokana na kile walichoeleza wanahitajika kwa wakati huu.
Anasema kuwa huo ni uchaguzi ndani ya chama hivyo ni vizuri kutumia kauli nzuri hasa katika kipindi hiki kwani viongozi wote wanamchango wao mkubwa katika kukijenga chama hicho hadi kufikia hapo kilipo.
"Maamuzi haya si yetu binafsi bali tumesukumwa na mawazo ya wanachama wetu ,sisi ni wawakilishi na tumetumwa kwenda kufanya maamuzi haya ndiyo maana tumejitokeza hadharani,'
"Hawa wagombea wote ni viongozi wetu na hasa Freeman Mbowe amefanya kazi kubwa ya kukiongoza chama hiki hivyo hatuwezi kutumia lugha ya matusi kwake kutokana na sisi kutumuunga mkono katika uchaguzi ujao.,"amesema Luzubukya.
Amesema walichokifanya ni demokrasia ndani ya chama hicho na wala hakuna kosa lolote walilolifanya kwa kutangaza uamuzi huo hadharani.
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Simiyu, Mussa Onesmo amesema kuwa wameamua kutangaza uamuzi huo hadharani lakini ni lazima wamshukuru Mbowe kutokana na kuitoa mbali taasisi hiyo na hasa kuwajenga vijana katika uongozi.
Mwenyekiti wa mkoa, Mussa Onesmo (aliyeshika katiba ya chama) akisisitiza jambo katika kikao na waandishi wa habari juu ya kutangaza nia yao ya kumuunga mkono mgombea Uenyekiti wa chama hicho Taifa,Tundu Lissu."Pamoja na mazuri aliyoyafanya Mwenyekiti Mbowe katika chama chetu lakini katika uchaguzi huu hatupepesi macho wala mdomo kusema kuwa tunawaunga mkono Lissu na Heche na huu ni msimamo wa wanachama walio wengi wa CHADEMA katika mkoa wetu wa Simiyu,"amesema.
Naye Mbunge mstaafu wa CHADEMA, Slivester Kasulumbayi, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki mwaka 2010 ameongeza kusema kuwa ni wakati muafaka kwa vijana walioandaliwa uongozi na Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Freeman Mbowe, kuongoza chama hicho kwa mikakati mipya.
Aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Silvestrer Kasulumbayi (Chadema) akiwa kwenye kikao cha wajumbe wa mkoa wa Simiyu waliotangaza nia ya Kumuunga mkono Tundu Liasu na John Heche."Matamanio yangu nikiwa mzee kuona vijana wetu ndani ya chama walioandaliwa na Mwenyekiti Mbowe wanachukua nafasi za uongozi ili waje na mawazo, mikakati na mbinu mpya katika kukiongoza chama chetu na hawa akina Lissu na Heche huu ndiyo muda wao,"amesema.
Msimamo huu unaashiria hatua mpya za mabadiliko ndani ya uongozi wa CHADEMA na uchaguzi huo unategemewa kufanyika Januari 21 mwaka huu.
Post a Comment