DC BUKOBA KUWAFUATILIA WANAFUNZI KUHAKIKISHA WANARIPOTI SHULE
Na Alodia Dominick, Bukoba
MKUU wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Sima amesema kuwa ofisi yake itahakikisha inafanya ufuatiliaji ndani ya wiki mbili ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaopaswa kwenda shule waende kwa asilimia 100.
Sima ameyasema hayo leo Januari 13, 2025 wakati akitoa takwimu ya wanafunzi wanaopaswa kuanza kidato cha kwanza, darasa la kwanza na awali ambao tayari wamechukua fomu na wengine kujisajiri kwa ajili ya kuanza shule katika muhula wa kwanza kwa mwaka huu.
Amesema asilimia 75 ya wanafunzi watakaoanza kidato cha kwanza mwaka huu walikuwa wameishachukua fomu katika halmashauri ya Bukoba ambapo wanafunzi 6,339 walishinda na kupangiwa shule mbalimbali.
Amesema hadi Januari 10, 2025 wanafunzi 4,780 walikuwa wamechukua fomu sawa na asilimia 75 na manispaa ya Bukoba waliopangiwa kwenda kidato cha kwanza wanafunzi 3,269 na waliokwisha chukua fomu wanafunzi 2,075 sawa na asilimia 63.4
Aidha amesema wazazi wanao uhuru wa kupeleka watoto shule za binafsi na kuwa wazazi watakaopeleka watoto wao katika shule hizo watoe taarifa kwa maafisa elimu ili watoto hao waweze kufuatiliwa kwa karibu.
Ametaja takwimu za maoteo ya wanafunzi wanaopaswa kuanza awali kwa halmashauri ya Bukoba kuwa walikuwa wanafunzi 8,959 waliokwisha jiandikisha wanafunzi 6,543.
" Kwa upande wa darasa la kwanza matokeo yalikuwa ni kuandikisha wanafunzi 8,947, walioandikishwa ni wanafunzi 6,188 sawa na asilimia 69.4 na kwa manispaa ya Bukoba wanakamilisha takwimu ya uandikishaji awali na darasa la kwanza" amesema Sima
Ametoa wito kwa wazazi ambao watoto wao wanapaswa kwenda shule kupeleka watoto wao kuanza masomo katika shule wanazopaswa kwenda ndani ya wiki hii ya kwanza.
Post a Comment