Home
/
HABARI KITAIFA
/
WALIMU KAGERA WATAKIWA KUWAPOKEA WANAFUNZI HATA KAMA HAWAJAKAMILISHA MAHITAJI YA SHULE
WALIMU KAGERA WATAKIWA KUWAPOKEA WANAFUNZI HATA KAMA HAWAJAKAMILISHA MAHITAJI YA SHULE
Na Alodia Babara, Bukoba
WALIMU waliopo katika shule mbalimbali mkoani Kagera wametakiwa kuwapokea wanafunzi wanaokwenda kuanza masomo katika shule wanazopaswa kwenda hata kama wana changamoto mbalimbali.
Hayo yamesemwa Januari 17, 2025 na Afisa elimu mkoa wa Kagera mwalimu Michael Ligola wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza awali pamoja na kidato cha kwanza.
“Mimi nikiwa kama msimamizi wa elimu katika eneo langu kwa niamba ya mkoa nitoe wito kwa wazazi kwamba, sisi uandikisha mashuleni tunaendelea nao mpaka sasa hivi, ninachowaomba wazazi wawapeleke watoto wao katika shule zilizopo karibu za msingi pamoja na sekondari ambazo wamechaguliwa” amesema mwalimu Ligolau.
Mwalimu Ligola ameongeza kuwa, inawezekana wazazi wana changamoto mbalimbali watoto hawajapata sale za shule, inawezekana hawana mahitaji kama daftari na vitu vingine lakini hivyo ni vitu vidogo vidogo visimuzuie mzazi kutompeleka mtoto shule yeye ampeleke atakutana na walimu shuleni alafu walimu watatoa maelezo kwamba mzazi afanye nini.
Amewasisitiza wazazi wenye watoto wa kuanza kidato cha kwanza kama mzazi ameamua kumpeleka shule za binafsi basi atoe taarifa katika shule aliyokuwa amepangiwa mwanafunzi ili upande wa elimu wawe na takwimu sahihi kwamba mwanafunzi alipangiwa shule fulani na amepelekwa shule nyingine iliyopo sehemu Fulani.
Amewahimiza wazazi kushirikiana na walimu, kamati za shule pamoja na bodi za shule katika kuchangisha fedha ya chakula ili mwanafunzi aweze kupata chakula shuleni.
“Ni vigumu kwa mzazi kumpatia fedha mwanafunzi ya kununua chakula shuleni kila siku na ndiyo maana nimesema mzazi ashirikiane na walimu, bodi ya shule na kamati ya shule kuhakikisha wanakubaliana kuchangishana chakula na hatimaye kukipeleka shuleni ili waweze kuwahudumia wanafunzi”
“Tunajua kabisa huu ubongo wa kawaida kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tisa kama hajapata kitu wakati anaenda kujifunza somo la kiingereza, hesabu, biolojia, kemia ni ubongo gani utakubali kupokea masomo hayo ni ngumu” amesema Ligola
Akizungumzia uandishaji wa kidato cha kwanza darasa la kwanza, awali na elimu ya watu wazima amesema kwa kidato cha kwanza wanapokea ripoti kila Ijumaa.
Ametoa takwimu za uandishaji kwa darasa la kwanza kuwa hadi Janauri 17,2025 mkoa umeandikisha asilimia 74.43, awali wameandikisha asilimia 68 na elimu ya watu wazima na nje ya mfumo rasmi (MEMKWA) wanafunzi 263.
Amesema kuwa, maoteo ya mkoa yalikuwa ni kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza wapatao 87,739 wasichana 44,288 na wavulana 43451, awali maoteo yalikuwa ni kuandikisha 61,404 wasichana 31,239 na wavulana 30,165.
Halmashauri ya manispaa ya Bukoba inaongoza kwa uandikishaji wa wanafunzi watakaoanza darasa la kwanza kwa asilimia 99.24 ikifuatiwa na halmashauri ya Biharamlo kwa uandikisha wa asilimia 80.95.
Adha, manispaa ya Bukoba maoteo yalikuwa wanafunzi 3,561 wavulana 1,740 na wasichana 1,821, waliokwisha andikishwa ni wanafunzi 3,534 wavulana 1,799 na wasichana 1,735 sawa na asilimia 99.24.
Halmashauri ya wilaya ya Biharamlo ilipanga kuandikisha wanafunzi wa darasa kwanza wapatao 16,284 wasichana 8,157 na wavulana 8,127 hadi sasa wameandikishwa wanafunzi 13,182 wavulana 6,481 na wasichana 6,701 sawa na asilimia 80.95.
Halmashauri ya wilaya ya Ngara maoteo yalikuwa kuandikisha wanafunzi 12,920 wavulana 6,355 wasichana 6,565, waliokwisha andikishwa wanafunzi 9,878 wavulana 4,887 na wasichana 4,991 sawa na asilimia 76.46.
Pia halmashauri ya Bukoba maoteo yalikuwa ni kuandikisha wanafunzi 8,947 wasichana 4,404 na wavulana 4,543, waliokwisha andikishwa ni 6,786 wasichana 3,399 na wavulana 3,387 sawa na asilimia 75.85.
Halmashauri nyingine ni Kyerwa ambayo maoteo yalikuwa kuandikisha wanafunzi 11,869 wavulana 5,795 na wasichana 6,074, waliokwisha andikishwa wanafunzi 8,998 wavulana 5,696 na wasichana 3,302 sawa na asilimia 75.81.
Aidha halmashauri nyingine ni Misenyi maoteo yalikuwa ni kuandikisha wanafunzi 6,667 wavulana 3,258 na wasichana 3,409, waliokwisha andikishwa wanafunzi 4,630 wavulana 2,267 na wasichana 2,363 sawa na asilimia 69.45.
Pia maoteo katika halmashauri ya Muleba yalikuwa kuandikisha wanafunzi 17,247 wavulana 8,503 na wasichana 8,744, waliokwisha andikishwa wanafunzi 11,494 wavulana 5,601 na wasichana 5,893 sawa na asilimia 66.64.
Alitaja uandikishaji kwa halmashauri ya Karagwe maoteo yalikuwa ni kuandikisha wanafunzi 10,244 wavulana 5,130 na wasichana 5,114 waliokwisha andikishwa wanafunzi 6,802 wavulana 3,432 na wasichana 3,370 sawa na asilimia 66.40.
Aidha, mwalimu Ligola amesema, maoteo ya wanafunzi wa awali yalikuwa ni kuandikisha wanafunzi 61,404 wavulana 30,165 na wasichana 31,239 na hadi leo hii wanafunzi walioandikishwa walikuwa 41,799 sawa na asilimia 68.
Post a Comment