HEADER AD

HEADER AD

CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI PWANI, COREFA WAKUTANA KUTANGAZA MICHEZO

Na Gustaphu Haule, Pwani

CHAMA cha Mpira wa miguu mkoa wa Pwani (COREFA) pamoja na  Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Pwani (CRPC) wamekutana katika kikao maalum kwa ajili ya kufungua ukurasa mpya katika kujenga mashirikiano ya kutangaza michezo mbalimbali inayofanyika ndani ya mkoa.


Kikao hicho kimefanyika Januari 4,2025 katika ofisi za COREFA zilizopo Kibaha kwa Mathias kikiongozwa na  mwenyekiti  Robert Munisi sambamba na makamu mwenyekiti Mohamed Lacha, Mohamed Masenga( Katibu), Mwenyekiti wa Soka la Wanawake(TWFA) Mkoa wa Pwani Asha Mbatta na mjumbe wa xcom Nassoro Mbilinyi.

      Viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Pwani mara baada ya kikao maalum kilichoketi Januari 4,2025 katika ofisi za Chama hicho .

Kwa upande wa Klabu ya Waandishi wa Habari kikao hicho kiliwakilishwa na wajumbe 10 akiwemo Makamu mwenyekiti wa Klabu hiyo Harold Shemsanga na Katibu wake Gustaphu Haule pamoja na waandishi wa habari wengine  nane kutoka Vyombo mbalimbali.

Kikao hicho ambacho ni cha kwanza kufanyika tangu uongozi huo mpya  uingie madarakani kimekuwa ni kikao cha mafanikio makubwa kwakuwa kimeleta taswira ya kujua COREFA imetoka wapi,ilipo sasa, na matarajio yake ya baadae.

Katika kikao hicho, Munisi ambaye mbali na kueleza mipango ya namna ya kushirikiana na Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Pwani lakini pia ametumia nafasi hiyo kueleza mafanikio ya COREFA yaliyopatikana ndani ya mwaka mmoja na miezi sita ya uongozi wake .

      Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Robert Munisi (Katikati)akizungumza katika kikao maalum na Waandishi wa Habari kilichofanyika Januari 4,2025 katika ofisi za Chama hicho zilizopo Kibaha kwa Mathias.

Munisi amesema kuwa, katika kipindi hicho chama hicho kimefanikiwa kuanzisha Kanda mbalimbali ikiwemo Kanda ya Kaskazini na Kusini ambapo kwa upande wa Kaskazini imejumuisha Wilaya ya Kisarawe,Kibaha na Bagamoyo huku Kusini ikijumuishwa Wilaya ya Mkuranga,Kibiti,Rufiji na Mafia.

Munisi amesema lengo la kuanzisha Kanda hizo ni kutaka kuhakikisha mpira unachezwa kama ambavyo Kauli Mbiu yake inavyosema "Pwani lazima mpira Uchezwe" .

Amesema kuanzishwa kwa Kanda hizo pia kumetokana na nguvu ya msukumo kutoka kwa Rais wa TFF Wallace Karia,ambaye ameelekeza vyama vya michezo kuwekeza nguvu zote katika maeneo matatu.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Soka la Vijana,Soka la Wanawake na Soka la Ufukweni(Soccer Beach).

Amesema katika kufikia malengo hayo, tayari COREFA imefanikiwa kuanzisha vituo vya michezo vinne kikiwemo kituo cha Kibaha,Kisarawe, Mkuranga na Rufiji na vyote vinafanya vizuri huku malengo yake ni kuhakikisha wanapata vituo Saba.

     Ofisi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani COREFA iliyopo Kibaha kwa Mathias.

"COREFA tumefanikiwa kuanzisha vituo vinne ambapo lengo lake ni kuinua vipaji kwa vijana na vituo hivyo vinafanya vizuri lakini bado kwasasa tunapeleka vituo vingine viwili katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na Kibaha Vijijini ",amesema Munisi

Amesema vituo hivyo vitashindana kwa ajili ya kupata timu ya Vijana ya umri wa miaka 15 ambapo hatahivyo amewashukuru wafadhili mbalimbali kwa kujitoa katika kusaidia michezo hiyo katika maeneo yao.

Ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuhakikisha ligi zote zinafanyika kwa asilimia 100 licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa fedha za kuendeshea mashindano hayo.

Amesema katika soka la wanawake timu 20 zimeshiriki na Mkuranga ndio Wilaya iliyofanya vizuri na kwamba hata ligi ya mkoa upande wa mpira wa Miguu imefanyika japo sio mabingwa wote waliweza kushiriki.

"Natoa wito kwa mabingwa wote kuhakikisha wanashiriki ligi ya Mkoa na mwaka huu bingwa wa Mkoa ni Nyika ambaye atashiriki mashindano ya ligi ya mabingwa wa Mikoa," amesema Munisi

Amesema pia COREFA imefanikiwa kupata eneo la ekari tano kwa ajili ya ujenzi wa ofisi yake na kwamba eneo hilo limepatikana Kata ya Viziwaziwa huku akiishukuru Halmashauri ya Mji Kibaha kupitia mkurugenzi wake Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa hatua kubwa ya kusaidia hupatikanaji wa eneo hilo.

Ameeleza kuwa kwasasa tayari mikakati imeanza ya namna ya kujenga ofisi hiyo na mwezi huu kamati tendaji itakaa kwa ajili ya kuteua kamati ya ujenzi wa ofisi hiyo huku akisema malengo ya COREFA ni kuhakikisha ndani ya mwaka huu inapata ofisi yake.

",Hapa niseme sio ofisi tu,bali tunataka COREFA hiweze kujitegemea kwa kumiliki mali zake wenyewe ndio maana tumejipanga vizuri na ikitokea tumepata eneo lingine hapa Mjini tutashukuru kwakuwa nalo tutaliendeleza kwa kuweka vitega uchumi,"amesema Munisi

Kuhusu suala la waamuzi ,Munisi amesema kuwa tangu waingie madarakani tayari wamefanikiwa kuhakikisha waamuzi zaidi ya 30 wanachezesha na kusimamia ligi za TFF ikiwemo ligi kuu, Lligi daraja la kwanza na ligi nyingine.

Amesema sio hao tu bali wamefanikiwa kuzalisha mechi kamishna wapya na kwamba kazi hiyo inaendelea kufanyika Kwa kutoa kozi mbalimbali za ukocha na waamuzi ambapo ametoa wito kwa wadau wa michezo kushiriki kozi hizo pale zinapotangazwa.

Amesema, baada ya kufanikiwa katika maeneo hayo ,kwasasa COREFA imejipanga kuhakikisha mkoa wa Pwani inapata timu itakayoshiriki  katika mashindano ya Ligi Kuu ambayo yatasaidia pia kuutangaza mpira wa Pwani,kuibua vipaji ,Kukuza uchumi kwa vijana na hata  Mkoa kwa ujumla.

Amesema kuwa , changamoto kubwa inayowakabili ni suala la viwanja lakini kwasasa taratibu zinaendelea na kwamba changamoto hiyo inakwenda kupata majibu kwakuwa vipo viwanja vinajengwa na vingine kukarabatiwa 

Munisi amesema kuwa COREFA inakazi kubwa ya kufanya katika kukabiliana na changamoto ya viwanja na kwamba miongoni mwa viwanja ambavyo COREFA inavitolea macho ni pamoja na Msoga.

Kiwanja cha Msoga kipo mbioni kukamilika na kitakuwa sehemu ya kuendeleza michezo ya Mkoa wa Pwani katika Ukanda wa Kaskazini lakini pamoja na hicho vipo vingine vingi .

Ametaja viwanja vingine kuwa kiwanja cha Bungu kilichopo katika Halmashauri ya Kibiti,kiwanja cha Mwanambaya kilichopo Halmashauri ya Wilaya  Mkuranga,kiwanja cha Shirika la Elimu Tumbi Kibaha, kiwanja cha Kiromo- Bagamoyo,kiwanja cha Kisarawe na kiwanja cha Ruvu ambacho kwasasa kinatumika katika ligi mbalimbali za TFF .

Amesema kuwa, COREFA imeweka nguvu katika kuhakikisha viwanja hivyo vinakarabatiwa ili viweze kutumika katika mashindano mbalimbali na kwamba kukamilisha kwa viwanja hivyo itakuwa imemaliza changamoto ya ukosefu wa viwanja Mkoa wa Pwani.

" Hivi viwanja vyote vikikamilika tutakuwa hatuna changamoto ya viwanja, lakini changamoto itakuwa ni upatikanaji wa timu za kucheza katika viwanja hivyo kwakuwa vitakuwa viwanja vingi timu chache,natoa wito kuhakikisha vilabu vinasajiliwa ili kuweza kutumia viwanja hivyo,"amesema Munisi.

Munisi ametumia kikao hicho kuwashukuru baadhi ya wadau ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia kufanikisha kuendesha mashindano ya Ligi ngazi ya Mkoa yaliyomalizika hivi karibuni na kupata mshindi wake Nyika FC.

Ametaja wadau hao kuwa ni pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( Tamisemi) Mohamed Mchengerwa, Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya COREFA ambaye ni Waziri wa Viwanda na Biashara Selemani Jafo, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka,Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Omar Kipanga,Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Michael Mwakamo na hata wadau wengine.

Makamu mwenyekiti wa COREFA Mohamed Lacha,amesema kuwa Chama kimefanikiwa kufanya mambo mengi japo wamepitia katika wakati mgumu wa kukosa fedha za kuendeshea shughuli zake.

Wa pili kushoto ni Makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) Mohamed Lacha akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mipango ya utekelezaji iliyojiwekea katika kipindi cha mwaka 2025.

Lacha amesema mpaka sasa COREFA haina chanzo halisi cha mapato lakini kikubwa wanachotegemea ni ada za wanachama na michango ya wadau mbalimbali ambayo hatahivyo haitoshi kuendesha shughuli zote za michezo .
 
Amesema mwaka 2025 wamejipanga kufanya vizuri zaidi na kwamba katika kipindi cha kalenda ya michezo ya Mwaka mzima COREFA imekadiria bajeti ya zaidi ya Sh .milioni 100 ambapo amewaomba wadau wa michezo na taasisi mbalimbali kujitokeza katika kusaidia michezo ya Mkoa wa Pwani.

Amewaomba Waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na COREFA katika kuhakikisha  wanaitangaza michezo sambamba na kusaidiana katika kuibua vipaji kwa vijana.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Soka la Wanawake Mkoa wa Pwani( TWFA) Asha Mbatta,amesema kuwa mwaka jana waliweza kucheza ligi katika Wilaya Sita isipokuwa Mafia.

 Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Pwani (TWFA) Asha Mbatta (katikati) akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi za COREFA kuhusu namna alivyojipanga kuendesha ligi ya Wanawake inayotarajia kuanza mapema mwaka huu.

Mbatta amesema kuwa ligi ya Mkoa ilifanyika katika kiwanja cha Mwanambaya katika Halmashauri ya Wilaya Mkuranga kwakuwa Ukanda huo ulikuwa na timu nyingi na hatimaye  Rufiji Queens kuibuka kuwa mshindi wa Mkoa.

Mbatta amesema kuwa ,mwaka huu kalenda ya matukio ya COREFA tayari imetoka na inataka Soka la Wanawake lianze katika kipindi cha Januari hadi Machi kipindi ambacho kinatakiwa bingwa awe amepatikana.

Aidha,amesema ligi hiyo itaanza kuchezwa katika ngazi ya Wilaya na baadae kufikia ngazi ya Mkoa lakini hatahivyo kabla ya kuanza mashindano hayo kamati ya utendaji itafanya ziara kila Wilaya Kwa ajili ya kuhamasisha wadau wengi kujitokeza kwa ajili ya kushiriki ligi hiyo.

",Kabla ya Ligi kuanza kamati tendaji itapita katika Wilaya zote Saba kuhamasisha wadau wajitokeze na Wilaya ya kwanza itakuwa Kibaha ,hivyo nawaomba viongozi wake wajipange vizuri kuhakikisha ligi hiyo inafanikiwa,"amesema Mbatta

Mbatta ,amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kwa ajili ya kusaidia ligi hiyo pale itakapoanza kwakuwa bila ushirikiano huo kunaweza kupunguza nguvu na hamasa katika kuinua Soka la Wanawake.


No comments