HEADER AD

HEADER AD

FURAHA YA WANANCHI WA BUJINGWA , KILABELA BAADA YA KUPATA MAJI YA BOMBA

>>Ni wale waliokosa maji safi na salama licha ya kupitiwa na bomba la maji

>>Walitumia maji yasiyo salama wakichangia pamoja na mifugo, wadudu

>> Wanyama wakali waliwatia hofu wakati wakisaka maji usiku

Na Dinna Maningo, Mwanza

WASWAHILI wanasema hayawi hayawi yamekuwa. Ni baada ya serikali  kutatua kero ya maji kwa wananchi wa mtaa wa Bujingwa na Kilabela katika kata ya Bugogwa, wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, iliyowakumba kwa miaka mingi bila mafanikio.

Ukosefu wa maji safi na salama maarufu maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria ulisababisha wananchi wa mitaa hiyo kupata magonjwa ya homa ya matumbo, kutembea umbali mrefu kufuata maji visimani, ziwani , kuamka usiku wa manane kwenda kupanga foleni kusotea maji .

        Wananchi wa mtaa wa Bujingwa wakichota maji kisimani yasiyo safi na salama

Kipindi cha kianzi kilikuwa ni maumivu kwa wananchi kwakuwa visima vilikauka na maji kukosekana huku wengine wakilazimika kuamka usiku kwenda kusubiri maji yaliyovuja kidogokidogo kisimani hali ambayo ilileta ugomvi kwa wanandoa pindi walipochelewa kurudi nyumbani.

Septemba, 20, 2022 katika chombo hiki cha habari iliripotiwa makala yenye kichwa cha habari kisemacho ' BOMBA LA MAJI LIMEPITA MTAA WA BUJINGWA, KILABELA LAKINI WANANCHI HAWAJANUFAIKA NA MRADI ' .

Ni baada ya mwandishi wa chombo hiki cha habari kufika mtaa wa Bujingwa na Kilabela kufahamu hali ya huduma ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa mitaa hiyo kama inaendana na Sera ya Maji ya Taifa ya mwaka 2002 ambayo imetokana na mapitio ya Sera ya mwaka 1991.

Sera ya maji inaeleza kuwa maji ni muhimu kwa viumbe vyote duniani, bila maji hakuna uhai, maji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya maji yoyote kinategemea kuwepo kwa maji ya kutosha yenye ubora unaotakiwa.

Wananchi wa mtaa huo licha ya bomba kubwa la maji kupita kwenye ardhi yao lakini hawakunufaika na maji ya bomba na badala yake kuendelea kutumia maji ya sio safi na salama ya visima vinavyomilikiwa na wananchi, wakichangia na wanyama wa kufugwa, wakiwemo ng'ombe, mbuzi, mbwa, kondoo na wanyama wa porini kama fisi, wadudu, watambaao na ndege.

         Maji yaliyotumiwa na wananchi, mifugo kabla ya mradi wa maji ya bomba

Shaban Nkungu ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Bujingwa akaeleza kuwa, suala la uhitaji wa maji ya bomba kwenye mtaa ni la muda mrefu na wamekuwa wakifuatilia kwenye mamlaka zinazohusika na huduma ya maji lakini hupewa ahadi ya kuvutiwa maji isiyotekelezeka.

Pia ukosefu wa maji uliwaathiri wanafunzi na hivyo kurudisha nyuma taaluma ya wanafunzi kwakuwa muda mwingi walikuwa wakishinda kisimani kusubiri maji. Hali hiyo ikasababisha wachelewe shule na kukosa baadhi ya vipindi na wengine kuwa watoro.

      Watoto wakisubiri maji yavuje kisimani ili wachote ambapo wakati mwingine uchelewa kwenda shule au kutokwenda kabisa wakienda kusotea maji kisimani huku ndoo nyingi zikiwa zimepangwa foleni zikisubiri maji 

Furaha baada ya kupata maji

Hivi karibuni wananchi wakizungumza na DIMA ONLINE iliyofika katika mitaa hiyo, wanasimulia namna maji ya bomba yalivyoondoa karaha na kurejesha furaha kwa wananchi wakiwemo wanandoa.

Shaban Nkungu ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Tawi la Bujingwa , anaishukuru serikali kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kufikisha huduma ya maji ya bomba kwenye mitaa hiyo.


 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Tawi la BujingwaShaban Nkungu akizungumza

" Tunaishukuru serikali ya chama cha Mapinduzi kwa kusikiliza kilio cha siku nyingi, sasa hivi maji yamefika mtaani. Awali wakati wa kiangazi watu ununua ndoo moja ya maji sh. 500 kutoka kwa watu walioyafuata ziwani kwa usafiri wa basikeli na mkokoteni.

"Lakini sasa hivi wanayapata maji hapahapa mtaani ndoo moja Tsh. 100 japo nayo hayatoshelezi. Tunaomba watuongezee Gati tano, zilizopo ni mbili tu na ziko mbali na makazi ya watu japo sio mbali sana kama ilivyokuwa kabla ya kupata mradi huu wa maji.

"Nawaomba wananchi wangu huu mradi wa maji ya bomba wautumie vizuri, walinde miundombinu ya maji, na watu wa maji watakapopita basi wajitahidi kujaza fomu ili wavutiwe maji majumbani" anasema Mwenyekiti.

Scolastica Pamba anasema " Huko nyuma tulikesha kwenye visima kusubiri maji , jambo lililoleta ugomvi , waume zetu wakidhani labda tunatumia changamoto hiyo kwenda kuchepuka na wanaume wengine .

       Scolastica Pamba akieleza maji ya bomba yalivyowapa unafuu.

" Angalau maji ya bomba yapo unaweza kuchota ukatunza maana kuna wakati yanaweza kukatika yakamaliza siku mbili au wiki ila yakija unachota vyombo vyako vyote" anasema Scolastica.

Anna Seleman anasema " Nafurahi maji yapo jirani na nyumbani , kwa sasa sitofata maji umbali mrefu. Haya maji ni safi na salama tunayanywa hata bila kuchemsha" anasema Anna.

Grace Michael anasema kwa sasa wana unafuu wa maji tofauti na awali walitegemea maji kwenye visima na madimbwi yasiyo safi na salama huku akiomba serikali kuwavutia maji majumbani kwa gharama nafuu.

Furaha Peter mkazi wa mtaa wa Kilabela anaeleza kuwa " Kabla ya haya maji ya bomba tulikuwa tunaamka saa kumi asubuhi kwenda kusotea maji visimani .Maji yalikuwa ni ya kusubiria yavuje ndipo uchote, una ndoo tano unachota ndoo mbili unasubiri wenzio nao wachote ndipo uchote ndoo zako zilizobaki.

      Furaha Peter  mkazi wa mtaa wa Kilabela ( kulia) akichota maji safi na salama 

" Sisi wageni tulipata changamoto ukienda kuchota maji wenyeji wanakwambia uchote ndoo moja lakini wao wanachota ndoo tano tano, wakisikia ndoo ni za fulani unabaguliwa , wakati mwingine tulilazimika kunywa maji ya madimbwi" anasema Furaha.

Anaongeza kuwa wakati wa shida ya maji walikutana na wanyama wakali nyakati za usiku hasahasa fisi na hivyo kuishi maisha ya uoga ikizingatiwa mitaa hiyo nyakati za usiku ni Giza Nene kwakuwa haijafikiwa na huduma ya umeme.

" Maji yalitutesa sana tuliamka usiku,  tukiwa njiani tulikutana na fisi zinatutisha, zinaunguruma wakati huo unatembea usiku umbali wa kilomita moja hadi mbili kufuata maji kisimani.

" Ilitubidi wakati wa kufuata maji tunaamshana tunapitiana tunaondoka pamoja, maji yalikuwa sio safi na salama , tuliyatumia hivyo hivyo watu wakawa wanaugua matumbo, minyoo, kichocho na kipindupindu.

" Wenye pesa walikuwa wanaagiza watu wa pikipiki wanawafuatia maji ndoo moja Tsh. 500. Ili upate maji ya kutosha kwa siku ni ndoo zisizopungua tano maana unakuta una familia kubwa maji kidogo hayatoshi na wakati mwingine tulilala bila kuoga kwa sababu ya ukosefu wa maji" anasema .

Elvida Lucus  mkazi wa mtaa wa Kilabela anaongeza " Tunafurahi kupata maji ya bomba, maana unafungua bomba maji yanatoka ndoo yako inajaa bila kuhangaika kuchotachota na vibakuli.

        Elvida Lucus  mkazi wa mtaa wa Kilabela

" Awali tulitumia maji machafu ambayo unayasotea kwa kuamka usiku saa sita kwenda kuchota, maji ambayo wanyama wanaingia kunywa, vinyesi vinabaki majini, wadudu wanatambaa majini.

" Watu tukapata magonjwa ya matumbo, Amiba, Kipindupindu na minyoo ilituathiri sana, walau saizi maji ni safi na salama japo Gati hazitoshelezi maji yakikatika wakati mwingine yanakaa wiki nzima ndio yanarudi na kuna watu wanaishi mbali na hizo Gati" anasema.

Serikali yaombwa kusambaza maji

Wananchi wa mitaa hiyo wanaiomba serikali iendelee kusambaza maji  majumbani kwani Gati zilizopo ni chache hazitoshelezi jambo ambalo linasababisha msongamano wa watu bombani wakisubiria maji.

Revocatus Malendeka anasema " Miundombinu ya maji imepita ila wameweka mabomba machache hayakidhi mahitaji , mtaa wa Bujingwa yapo mabomba mawili na yako mbalimbali. Yaliwekwa mbali na makazi ya watu yapo mashambani. Tunaomba watu wa idara ya maji watuwekee maji karibu na makazi yetu" anasema.

Amos Kuyunga anawaomba wananchi kijitahidi kuvuta maji majumbani kwao  huku akipongeza mtaa kupata maji ya bomba. " Tunashukuru kwa mwanzo huu ni hatua nzuri ,maji yamesaidia kupunguza changamoto iliyokuwa kubwa. Wakati wa kiangazi tunakosa maji inabidi wake zetu waamke saa saba usiku kwenda visimani, wakienda kurudi ni saa tano asubuhi kwa sababu ya foleni.

       Ndoo za maji zikiwa kwenye foleni zikisubiri maji

" Akitoka huko ndio afanye maandalizi ya chakula inabidi mimi baba na watoto tuvumilie yaani ilikuwa kero. Lakini sasa hivi foleni sio kubwa hata maji yakikatika yakitoka watu wanachota foleni inakuwa sio kubwa kama ilivyokuwa zamani wakati walipochota maji ya visima.

" Gati za maji zimesaidia maana mtu anapata maji kwa wakati mzuri ambayo sio maji ya kusotea sana , hata yakikatika yakirudi unakuwa na uhakika wa kupata maji, na wengine wamevuta majumbani kwao, sio kama unavyosotea visimani kusubiri maji yavuje uchote" anasema Amos.

Ever Misalaba anaiomba serikali kutatua changamoto ya maji " Maji ya bomba yapo ila yanakatika mara kwa mara, yakikatika tunaenda kuchota ya visimani , japo baada ya mabomba haya ni watu wachache ndio wanaenda kuchota maji kisimani hasa wale wasio na vyombo vingi majumbani vya kutunzia maji ili hata yanapokatika basi unakuwa bado una maji ndani yakitoka unachota mengine" anasema .

        Mwananchi mkazi wa mtaa wa Bujingwa akiwa bombani akisubiri maji baada ya kukatika

Vumilia Bukoga ni msimamizi wa maji anasema walianza kupata huduma hiyo ya maji mwezi wa tatu mwaka jana. " Tunashukuru kupata maji ya bomba. Maji yanatoka japo yanaweza kukatika yakatoka baada ya siku mbili, yakikatika tunaenda kuchota kwenye majeruba.

" Tumeweka utaratibu wa kuchota maji, tunachota saa 12 hadi saa moja asubuhi, alafu yanafungwa, yanafunguliwa tena  saa tisa hadi saa kumi jioni yanafungwa . Ikifika saa kumi na saa 12 na nusu yanafunguliwa wanachota hadi saa moja usiku yanafungwa mpaka kesho asubuhi saa 12"  anasema.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kilabela John Jonathan Mang'ombe anasema mtaa wake una wakazi zaidi ya 1500 na kaya zaidi ya 300.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kilabela John Jonathan Mang'ombe akiwa amesimama kwenye Gati mtaani kwake

Anaishukuru serikali kuwapatia maji Gati nne ambayo yamewasaidia wakina mama " Huko nyuma akina mama walikuwa wanateseka wanaamka usiku na kurudi kesho yake lakini sasa hivi hali hiyo imepungua .

" Changamoto iliyopo sasa magati manne hayatoshelezi inatakiwa yaongezwe magati mengine mawili yawe sita. Gati ziliwekwa karibu na makazi ya watu wengi na yako karibu na miji ya watu kwa ajili ya kusaidia kulinda miundombinu hiyo" anasema John.

Anasema  pamoja na unafuu huo wa maji bado upatikanaji wa maji ni wa kusuasua " Mara yapo mara hayapo ,watu kununua maji sio shida ilimradi yapatikane .

Anaongeza " Usambazaji wa maji mitaani unahitajika tunaomba maji yaendelee kusambazwa yawafikie wananchi kwa ukaribu. Changamoto watu wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za kuvuta maji ambazo ni zaidi ya laki mbili kulingana na umbali" anasema.
 
Kimya cha MWAUWASA 

Mwandishi wa chombo hiki cha habari akafika hadi ofisi ya Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mwanza ( MWAUWASA) na kuonana  na Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka hiyo, Nelly  Msuya ili kufahamu je nini mkakati wa MWAUWASA kuhakikisha gati zinaongezwa katika mitaa hiyo?.

Je nini tatizo la maji kukatika na kukaa zaidi ya  siku tatu au hadi wiki moja bila kutoka kwenye gati ?. Mradi wa maji kilabela na Bujingwa umegharimu kiasi gani cha fedha?.


Je MWAUWASA ina mpango gani kuhakikisha wananchi wa Kilabela na Bujingwa wanapata maji toshelezi na ya uhakika pamoja na kusambaza majumbani ili wananchi wengi wapate huduma hiyo ya maji?.


Je ili mwananchi aweze kupata huduma ya maji ya bomba yafike nyumbani kwake anatakiwa afuate taratibu zipi na kiasi cha gharama endapo mtu anataka kuvutiwa maji majumbani. 


Mkurugenzi huyo alimwomba Mwandishi kumtumia maswali hayo kupitia email ya Mamlaka hiyo, Septemba, 2024, Mwandishi wa DIMA Online aliyatuma maswali na siku chache zilizopita alipowasiliana na Mkurugenzi huyo kumkumbusha majibu ya maswali , mkurugenzi alimpatia mawasiliano ya afisa habari wa Mamlaka hiyo Vivien Temu akimwomba awasiliane naye ili ampatie majibu ya maswali hayo.


Hata hivyo Mwandishi kila alipomkumbusha afisa habari huyo juu ya kumpatia majibu ya maswali hayo, Vivien aliahidi kuyafanyia kazi, lakini hadi sasa imepita zaidi ya miezi mitatu mamlaka hiyo haijaweza kumjibu mwandishi maswali hayo.

Chama Tawala cha Mapinduzi (CCM) kina Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 -2025 inayoielekeza Serikali kutekeleza yale yaliyomo kwenye Ilani ikiwemo Ibara ya 9 inayosema kuwa Chama kitaielekeza Serikali kuimarisha upatikanaji wa huduma bora ya Afya, Elimu, Maji, Umeme na makazi Vijijini na Mjini.

Pia kuongeza kasi ya usambazaji maji safi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya asilimia 85 Vijijini  na zaidi ya asilimia 95 kwa mjini kwa upande wa Tanzania Bara ifikapo mwaka 2025 imeeleza Ilani ya CCM.

Ilani hiyo Ibara ya 10 inasema kuwa CCM itahakikisha Serikalini yake inatekeleza mambo yote yaliyoahidiwa katika ilani.

      Aliyekuwa Mwenyekiti wa mtaa wa Bujingwa, Shija Habari akiwa kwenye Gati mtaani kwake.

         Wananchi wakieleza faida ya maji ya bomba na changamoto za ukosefu wa maji.


      Kisima kilichozungushiwa mabingobingo huku binti akifunga kufuli 

       Maji yaliyotumiwa na wananchi, mifugo kabla ya mradi wa maji ya bomba.


No comments