FIFA YAWATEUA VIJANA 16 PWANI KUTINGA KAMBINI TANGA
Na Gustaphu Haule, Pwani
CHAMA cha Mpira wa Miguu mkoa wa Pwani ( COREFA)chini ya mwenyekiti wake Robert Munisi kimekutana na wazazi wa vijana 16 walioteuliwa na FIFA pamoja na TFF kwa ajili ya kuwatakia heri ya kwenda kujiunga na kambi ya FIFA na TFF inayofanyika mkoani Tanga kuanzia Januari 12 hadi Januari 18 mwaka huu.
Kikao cha COREFA, wazazi, na vijana hao kimefanyika Januari 11,2025 katika ofisi za chama hicho zilizopo Kibaha kwa Mathias ambapo moja ya malengo ya kikao hicho ni kuwaaga vijana hao kwa heshima pamoja na kuwahakikishia wazazi usalama wa watoto wao na umuhimu wa Kambi hiyo.
Kikao cha pamoja baina ya viongozi wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani COREFA,wazazi na vijana 16 walioteuliwa na FIFA kushiriki Kambi maalum Mkoani Tanga .
"COREFA imepata heshima kubwa kutoka FIFA na TFF kwa kuchagua vijana wetu 16 kwenda katika Kambi ya Tanga kwahiyo tukaona sio vyema vijana hawa wakaondoka bila utaratibu,niwaambie tu vijana wenu wapo salama na kambi hiyo ni muhimu kwa maisha yao na familia kwa ujumla,"amesema Munisi.
Katika kikao hicho mwenyekiti wa COREFA Robert Munisi,amesema kuwa mpango wa kuendeleza vipaji kwa vijana umeanzishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani( FIFA) kwa ushirikiano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania ( TFF) ambapo Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa Pwani ( COREFA) ni watekelezaji wa mpango huo.
Munisi ,amesema kuwa FIFA na TFF walipita katika vituo mbalimbali vya michezo vilivyopo mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuangalia vipaji kwa vijana kuanzia miaka 11 hadi 14 na hatimaye kupata vijana 16.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani ( COREFA) Robert Munisi ( katikati) akizungumza na wazazi wa vijana 16 walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kushiriki Kambi maalum ya wiki moja Mkoani Tanga kuanzia Januari 12 hadi Januari 18,2025.
Upatikanaji wa vijana hao umepitia michakato mbalimbali ambapo kwa hatua ya awali walipita katika kila Wilaya kwenye vituo vya COREFA na kisha kuchagua vijana kulingana na vipaji vyao.
Amesema,baada ya kuchagua vijana hao walipelekwa katika Kanda mbili ambapo Kanda ya Kusini ilikuwa Kibiti na Kanda ya Kaskazini ilikuwa Kibaha katika viwanja vya Shirika la Elimu Tumbi.
Amesema kuwa,wakiwa katika vituo vya Kanda hizo mbili vijana hao walichaguliwa tena kulingana na vipaji vyao na hivyo kufanikiwa kupata vijana 16 ambao walituma majina yao COREFA.
"Mchakato wa kuwapata vijana hawa ni mpango maalum uliofanywa na FIFA pamoja na TFF na walikuja wazungu kutoka FIFA wakisaka vipaji hivyo na bahati nzuri Pwani tumebahatika kutoa vijana 16,"amesema Munisi
Munisi amesema kuwa baada ya kupata vijana hao FIFA wameamua kuwachukua na kuwapeleka katika Kambi maalum iliyopo Mkoani Tanga kambi ambayo ipo chini ya TFF.
"Vijana hawa sasa wanakwenda Tanga katika Kambi maalum ya FIFA na TFF mahali ambapo watakaa Kwa muda wa wiki Moja ikiwa kuanzia Januari 12 hadi Januari 18,2025 kwa ajili ya mchojo wa hatua ya mwisho",amesema Munisi
Amesema ,mtoto atakayebahatika kuchaguliwa Tanga itakuwa ni sehemu ya mafanikio ya maisha yake kwani upo uwezekano mkubwa wa kwenda kuendelezwa kipaji chake katika Bara la Ulaya.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani ( COREFA) Robert Munisi akiwa katika picha ya pamoja na vijana 16 walioteuliwa na FIFA kushiriki Kambi maalum ya vipaji iliyoanza kufanyika Januari 12 Mkoani Tanga.
Munisi ,ameishukuru TFF na FIFA kwa namna ambavyo waliona umuhimu wa kuendesha programu hiyo na hivyo kutoa vijana 16 mkoa wa Pwani na kwamba hiyo ni fahari kwa COREFA kuona vijana wao wanapata mafanikio kupitia vipaji vyao.
Munisi ametoa wito kwa wazazi wa mkoa wa Pwani kuhakikisha wanavitunza na kuviendeleza vipaji vya watoto wao kwakuwa michezo ni ajira na yenye kuleta mafanikio kwa urahisi.
Baadhi ya Vijana hao akiwemo Ibrahim Mohamed na Edmund Mwashambwa wamesema kuwa wanaishukuru FIFA,TFF na COREFA kwa namna ambavyo wanapambana kuibua vipaji vyao na kwamba wameahidi kuonyesha vipaji vyao kadri Mungu atakavyowajalia kwakuwa malengo yao ni kufika mbali.
Kijana Ibrahim Mohamed aliyeteuliwa na FIFA kujiunga Kambi maalum ya kituo cha Tanga kinachosimamiwa na TFF akizungumza na Waandishi wa habari katika ofisi za COREFA Januari 11,2025 kabla ya kuanza safari kuelekea mkoani Tanga
Mwakilishi wa wazazi wa vijana hao Azizi Mwashambwa,amesema kuwa jambo kubwa ni kuishukuru FIFA ,TFF na COREFA kwa kushusha programu ya kusaka vipaji kwa vijana katika ngazi za chini maana bila wao vipaji visingeonekana.
"Tunaipongeza COREFA kwa kupokea programu hii muhimu ya kusaka vipaji vya mchezo wa mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 maana bila wao leo hii tusingefika hapa tulipo leo ,nawaomba viongozi wa COREFA kuendelea kufanyakazi kwa moyo kwa ajili ya kuleta faida ya Vijana wa mkoa na Taifa kiujumla,"amesema Mwashambwa.
Mwashambwa amewaombea watoto hao ili waweze kufanikiwa kuchaguliwa katika Kambi ya Tanga na kwamba kuchaguliwa kwako ndio mwanzo wa mafanikio ya vipaji vyao kupitia mchezo wa mpira wa miguu.
Hatahivyo, Mwashambwa ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanafungua milango kwa vijana wa kiume na wakike kwa ajili ya kuonyesha vipaji vyao kwakuwa michezo inalipa na ni ajira na inachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa.
Post a Comment