TAKUKURU PWANI YASAIDIA KUOKOA ZAIDI YA MILIONI 314
Na Gustaphu Haule ,Pwani
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Pwani imesaidia kuokoa fedha zaidi ya Tsh. Milioni 314 zilizokuwa zinapotea kwa mwaka katika Kizuizi cha Maliasili kilichopo Wilayani Kibiti.
Awali kabla TAKUKURU hawajafanya ufuatiliaji katika kizuizi hicho makusanyo ya mapato kwa wiki kwa kutumia mashine ya POS yalikuwa kiasi cha Sh.milioni 4.6 ambapo kwa mwaka ukusanya kiasi cha sh. Milioni 166.7.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Alli Sadiki amewaambia Waandishi wa habari Januari 31,2025 katika mkutano uliofanyika ofisini kwake Mjini Kibaha kuwa walifanya ufuatiliaji katika kituo hicho na kubaini fedha nyingi kupotea katika Kizuizi hicho.
Amesema kuwa katika kipindi cha Oktoba na Desemba, 2024 Takukuru ilifanya uzuiaji katika mfumo wa ukusanyaji mapato kwa kutumia POS mashine kwa kuongeza makusanyo kutoka kiasi cha Tsh . Milioni 4.6 kwa wiki hadi kufikia kiasi cha Tsh .milioni 12.
Amesema Kutokana na ukusanyaji uliofanywa na Takukuru imeonyesha kuwa katika Kizuizi hicho kinatakiwa kukusanya kiasi cha Tsh .Milioni 480 kwa mwaka tofauti na makusanyo ya Tsh. Milioni 166.7 yaliyokuwa yakipatikana.
Amesema kuwa uzuiaji huo ulifanyika baada ya tathmini ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia POS mashine kutoridhisha kwa kukusanya mapato kiasi kidogo licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa Kizuizi cha Maliasili Kibiti.
Amesema TAKUKURU iliamua kusimamia ukusanyaji wa mapato katika kituo hicho kuanzia tarehe 5/11/2024 hadi tarehe 11/11/2024 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh .Milioni 12,089,760 ikiwa ni katika kipindi ambacho ukusanyaji wa mapato huwa chini ukilinganisha na miezi mingine ya makusanyo kwa mwaka.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Alli Sadiki, akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli zao katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba,2024, Mkutano huo umefanyika Januari 31 katika ofisi za Takukuru Mjini Kibaha
"Hii inaonesha tofauti ya makusanyo ya Tsh. Milioni 7,378,940.08 ambapo kwa wiki Halmashauri endapo kunakuwa na usimamizi mzuri wa makusanyo na itapata wastani wa chini wa Sh.milioni 10 na kuwa na uhakika wa kukusanya kiwango cha chini cha Sh.milioni 480 badala ya Tsh. Milioni 166.776,579 Kwa mwaka .
Aidha,Sadiki amesema kuwa katika ufuatiliaji huo, TAKUKURU imebaini kuwepo kwa mbinu na ujanja wa aina mbalimbali wakuchepusha mapato katika Kizuizi hicho ikiwemo baadhi ya wakusanyaji ushuru kuletewa fedha na wenye mizigo ili wasitozwe malipo ya ushuru wa Serikali.
Amesema baadhi ya wenye magari yenye mizigo kuwasiliana na wakusanyaji ili wapite bila kukaguliwa na wasilipie mizigo waliyoibeba huku magari mengine wakati wa ukaguzi walikuwa wakifungua buti na kuweka fedha za Rushwa ili wakusanyaji wachukue na hivyo wasiendelee na ukaguzi.
Ameongeza jambo lingine ni kwamba wakusanyaji wamepewa mwanya mkubwa wa kukadiria kiasi cha malipo cha kulipia katika mizigo inayopita na hivyo kusababisha Baadhi ya mizigo mikubwa kutozwa Ushuru mdogo.
Amesema baadhi ya bidhaa ambazo haziruhusiwi kusafirishwa zimekuwa zikipitishwa usiku na kutoa fedha kwa wakusanyaji ushuru ili wasichukuliwe hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU katika kipindi cha kuanzia Oktoba hadi Desemba 2024 imepokea jumla ya malalamiko 60 ambapo kati ya hayo malalamiko 37 yalihusu Rushwa na taarifa hizo zimeshughulikiwa kwa mujibu wa sheria kwa kuanzisha uchunguzi.
Amesema taarifa 23 hazikuhusu rushwa lakini zimeshughulikiwa kwa njia ya uelimishaji ,uzuiaji , ushauri, na kuhamishiwa idara nyingine ikiwemo Tamisemi(11), Michezo (1),Utalii(1),Polisi (4),Ardhi (10),Maji(1), Mahakama(2),Binafsi(3), Elimu(8),Viwanda(5), Ujenzi (4), Afya(4), Siasa(2), Maendeleo ya Jamii( 3), na ushirika (1).
Amesema katika kipindi hicho pia TAKUKURU mkoa wa Pwani imefungua jumla ya kesi mpya 24 Mahakamani ambapo kati ya hizo washtakiwa 13 wametiwa hatiani.
Sadiki ametoa wito kwa Wananchi wa mkoa wa Pwani kuendelea kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa kwa kufichua wale wote wanashiriki kufanya vitendo vya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika.
Hatahivyo, amewaasa wananchi kufuata sheria ,kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuwa salama na kuepuka migogoro yenye kuleta viashiria vya rushwa na kusisitiza kutoa taarifa za rushwa kupitia namba 113 sambamba na kufika ofisini kwao.
Post a Comment